Mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu na Naibu Spika, Job Ndugai, ‘wameshikana mashati’ katika kile kinachotafsiriwa kama ni muendelezo wa ushindani unaotokana na kutofautiana bungeni.
Wawili hao walishiriki mjadala uliohoji, ‘je, kanuni za Bunge zinajenga demokrasia’ katika kipindi cha kipimajoto kilichotangazwa juzi kupitia kituo cha luninga cha ITV.
Ilimbidi Ndugai kuingilia kati mara kadhaa na kumkatisha Lissu, alipokuwa akizungumza na kutoa maelezo ya namna kiti cha Spika kinavyokiuka kanuni na kuvuruga mwenendo wa Bunge.
NDUGAI AKIRI MABUNGE YA MSEKWA, SITTA YALIKUWA BORA
Ndugai alisema hali ya sintofahamu ndani ya Bunge ni kubwa kuliko ilivyokuwa wakati wa uongozi wa Pius Msekwa na Samuel Sitta.
Alikuwa akijibu swali la Samson wa Mwanza, aliyehoji sababu za kuwepo mvutano na malalamiko bungeni tofauti na ilivyokuwa wakati wa Msekwa na Sitta.
Ndugai alisema kiti cha Spika (kinacholalamikiwa kwa upendeleo na ukiukwaji wa kanuni), kinajitahidi kuongoza vikao vya Bunge ikiwemo kusisitiza matumizi ya lugha ya staha kwa wabunge.
“Labda ni suala la wakati, baadaye kidogo mambo yatakaa vizuri. Mimi nawaomba Watanzania wawasiliane na uongozi wa Bunge kujaribu kuwaomba wabunge wetu kutulia na kushughulika na hoja,” alisema.
AWAASA WABUNGE
Ndugai alisema ipo haja kwa wabunge baada ya kuchangia bungeni, wakae ili kusikiliza maoni ya watu wengine, hata kama hawaipendi hoja iliyotolewa.
Pia alisema wabunge wanaowasilisha hoja binafsi, wanapaswa kutafuta kuungwa mkono na wenzao, badala ya kutegemea msimamo wa chama ama kambi zilizomo bungeni.
Ndugai alisema umma unapaswa kuelewa kwamba hoja ya mbunge inatambulika rasmi inapopangwa kwenye ratiba za Bunge na si vinginevyo.
Alisema hayo wakati akihalalisha kutosomwa bungeni kwa hoja za baadhi ya wabunge, baada ya kamati ya uongozi kubadili ratiba kwa mkutano wa Bunge uliomalizika hivi karibuni.
Alisema hoja ambazo hazikusomwa zinatoka kwa wabunge 12 kupitia CCM na upinzani, zinazotarajiwa kuwasilishwa bungeni katika vikao vitakavyofanyika baadaye.
Alisema kazi ya kudhibiti vurugu bungeni itafanikiwa zaidi ikiwa wanadhimu wa CCM (William Lukuvi) na upinzani (Tundu Lissu) watashiriki kuwatuliza wabunge wao.
LISSU ALIA NA UDHAIFU WA SPIKA
Lissu alisema moja ya mifano ambayo wabunge wa upinzani wamekuwa wakilalamikia ni udhaifu uliopo kwa uongozi wa Bunge hususani katika kukiuka kanuni zilizopo.
Alisema tuhuma ya kuwepo utovu wa nidhamu (akimnukuu Ndugai), inaweza kuwa ishara kuwa Naibu Spika huyo hazijui kanuni za Bunge.
Lissu alisema kuna matatizo ya kwenye kanuni, na kuna matatizo ya matumizi ya kanuni bungeni.
Alisema kwa kiasi kikubwa, kanuni zilizopo ni nzuri, isipokuwa kuna matatizo katika namna zinavyotafsiriwa na kutumiwa.
Kwa mujibu wa Lissu, kanuni kuu inasema walio wengi wanatoa kauli ya kuamua wakati wachache wanapata kauli ya kusema.
“Tunachopigania sasa hivi kusema. Sehemu kubwa tunayopigania ni haki ya kusema inapokonywa. Bunge linagezwa chombo ambacho mambo makubwa ya kitaifa hayawezi yakazungumzwa,” alisema.
Alitoa mfano wa matukio yaliyosababisha vifo vya watu, upotevu na uharibifu wa mali, lakini Bunge halikujadili badala yake wabunge walikwenda kupumzika.
Matukio hayo ni mlipuko wa mabomu uliotokea kwenye kambi ya Jeshi la Wananchi (JWTZ), Gongolamboto jijini Dar es Salaam na ajali meli ya Mv Scagit.
“Watu walikufa wengi kwa sababu ya mabomu ya Gongo la Mboto… kilichotokea tukaambiwa imetokea watu wameuawa, hatuwezi tukakaa tunajadili hapa, nendeni likizo,” alisema.
Aliongeza, “Gongo la Mboto…ajali ya MV Scagit iliua watu, inaweza kuwa kwa uzembe au kwa bahati mbaya…Bunge badala ya kusimamisha shughuli zingine zote kujadili, linapewa likizo, nendeni nyumbani.”
MAANDAMANO YA MTWARA
Lissu alisema maandamano yaliyofanywa na wakazi wa Mtwara kuhusiana na gesi, ni moja ya mambo yaliyopaswa kujadiliwa bungeni, lakini haikuwa hivyo.
Alisema suala hilo lilipaswa kuzungumzwa na kujadiliwa bungeni ili lieleweke kwa umma, badala yake likaelekezwa kutolewa kwa wabunge kupitia semina.
“Kanuni zinasema mambo makubwa yajadiliwe bungeni, lakini matumizi ya kanuni yanakwenda isivyo,” alisisitiza.
Lissu alisema wapinzani hawatendewi haki kama inavyotakiwa kwa mujibu wa kanuni zinavyomuelekeza Spika kutenda haki kwa uadilifu bila chuki wala upendeleo.
Alisema kutokana na kutotendewa haki, wabunge wa upinzani wamekata rufani kadhaa kwa kamati ya kanuni bila mafanikio.
“Wamefanya makosa mengi tu, tumelalamika, tumefuata kanuni, tumekata rufaa, wengine wetu tangu mwaka 2011 wengine mwaka jana, wengine juzi. Hizi rufaa, kanuni inasema Spika itaitisha…
Naye Regina akizungumza kwa njia ya simu, alisema Bunge linapaswa kutambua kuwa umma unafuatilia vikao vyake, na kwa sehemu kubwa hauridhishwi namna kwa uendeshaji wa chombo hicho cha uwakilishi wa wananchi.
“Mtawahukumu hao viongozi wengine, kwamba wanafanya fujo, lakini kuna namna fulani mnayotaka kuifanya ya kutotenda haki,” alisema.
Aliongeza, “kweli nisiwadanganye, Watanzania tunachoka, tunakosa imani na nchi yetu, tunakosa imani na serikali yetu.”
NDUGAI AKANA KUUNDAMIZA UPINZANI
Hata hivyo, Ndugai, alisema si sahihi kujenga dhana kwamba upinzani hautendewi haki, kwa vile Kiongozi wa Kambi ya Upinzani ni mmoja wa ‘viongozi wakuu’ wa Bunge.
Hata hivyo, Lissu alisema kasoro nyingine ni pale Mbunge asiyeridhika, anapotakiwa kukata rufaa kwenye kamati ya kanuni inayoongozwa na Spika.
Alisema kikao cha kamati ya kanuni sharti kiitishwe na Spika, hivyo kuwa kikwazo na sababu ya kutochukuliwa kwa hatua hizo na kuzifanya rufani ziendelee ‘kulala’.
Hata hivyo, Ndugai alisema Lissu ni mjumbe wa kamati ya kanuni anayepaswa kuwasilisha hoja hiyo kwa mamlaka husika.
Ndugai alisema inapotokea Spika amekatiwa rufaa, kikao cha kujadili kinaongozwa na Naibu Spika kama ilivyo anapokatiwa rufaa Naibu Spika, Spika anakuwa Mwenyekiti wake.
Hata hivyo, Ndugai alisema hajawahi kuona nakala ya ‘shtaka’ analotuhumiwa kwa kamati ya kanuni na kusema huenda malalamiko hayo yapo ofisi ya Bunge.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment