Tuesday, February 26, 2013

CHADEMA yailiza tena CCM


KWA mara nyingine tena Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimekiliza Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya Mbunge wake wa Meatu, Meshack Opurukwa, kushinda kesi katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, kwa pingamizi la awali kutokana na mlalamikaji kutofuata sheria katika kukata rufaa.
Kesi hiyo iliyokuwa imefunguliwa na mpiga kura wa jimbo hilo, ambaye pia ni Katibu wa Mbunge aliyeshindwa, Masanja Salu, ilitupiliwa mbali na jopo la majaji, Edward Rutakangwa, Catherine Urio na Mbarouk Salum Mbarouk.
Katika kesi hiyo, mlalamikaji Salu, alikuwa na madai matatu tangu awali, la kwanza likiwa ni kutumia ukabila kwenye kampeni, tofauti ya kura zilizotangazwa na msimamizi wa uchaguzi na zile zilizopelekwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na mlalamikaji kudai kuwa Opurukwa alikiuka taratibu za kampeni kwa kujiendea bila utaratibu.
Awali katika kesi hiyo iliyokuwa inasikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, mbele ya Jaji Fredrick Wambali, mlalamikaji alishindwa kuthibitisha malalamiko yake, hivyo mahakama hiyo kumpa ushindi Opurukwa Mei 4 mwaka jana.
Kufuatia ushindi huo, mlalamikaji hakukubali na hivyo alikata rufaa, lakini jana mahakama iliitupitia kwa kuwa mlalamikaji aliikata nje ya muda.
Kesi hiyo ambayo upande wa mlalamikaji uliwakilishwa na wakili Jackson Brashi, huku Opurukwa akiwakilishwa na Godwin Muganyizi imefutwa kwa kuwa haikufuata sheria (null ab initio).
Desemba 21 mwaka jana, Mahakama ya Rufaa, nchini katika kesi za uchaguzi ilitoa mwongozo kuwa ‘mpiga kura hana haki ya kisheria kufungua kesi kuhoji matokeo ya uchaguzi pale ambapo haki zake hazikukiukwa’.
Mahakama iliongeza kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 26 (2) ya Katiba ya Tanzania, raia anakuwa na haki ya kisheria kufungua kesi kwa maslahi ya jamii, kama ilivyotokea katika kesi ya Mchungaji Christopher Mtikila dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya mwaka 1995.
Ilisema kesi dhidi ya wagombea wakitolea mfano kesi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), aliyeshtakiwa na wapiga kura hazikufunguliwa chini ya Ibara ya 26 (2) ambayo inampa fursa na haki raia yeyote kufungua shauri mahakamani lenye masilahi ya umma.

No comments:

Post a Comment