Wednesday, February 20, 2013

Chadema, NCCR Mageuzi wang’aka


VYAMA vya NCCR-Mageuzi na Chadema vimeng’aka kuhusu matokeo mabaya ya kidato cha nne, huku Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia akimtaka Rais Jakaya Kikwete kuunda tume yenye wataalamu mbalimbali wa elimu ili kulinusuru taifa.
Mbatia alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa matokeo hayo ni matunda ya nchi kuwa na mfumo mbovu wa elimu.
Mbatia ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa, alisema kama zinavyoundwa kamati za kuchunguza mauaji na ajali, hata sekta ya elimu inatakiwa kuundwa kamati kwa kuwa imeoza na kwamba ni janga kwani wanafunzi wengi wanafaulu kwa kukakiriri sio kuelewa.
“Umefika wakati wa kuweka tofauti zetu za kisiasa pembeni, tufanye kazi kwa pamoja ili kulinusuru taifa letu na elimu hii ya maafa, nilishangazwa sana na kitendo cha wabunge wa CCM kuipinga hoja yangu, haya ndio matokeo sasa,” alisema Mbatia na  kuongeza:
“Matatizo yapo mengi mfano ni kitendo cha kila waziri kubadilisha somo, kufuta mtihani au kuunganisha masomo mawili kuwa moja. Mawaziri wote waliopita tangu 1995 wanatumia mtalaa ule ule bila kuzingatia mabadiliko ya sayansi na teknolojia”.
Kwa upande wake, Chadema kimesema matokeo ya kidato cha nne ni janga la kitaifa ambalo limesababishwa na kupuuzwa kwa madai ya walimu.
Kutokana na Matokeo hayo, Chadema kimetaka Waziri Dk Kawambwa na watendaji wake wajiuzulu ili kuruhusu mabadiliko ya kimfumo katika wizara hiyo. Waziri Kivuli wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Suzan Lyimo alikizungumza na waandishi wa habari jana alisema:“matokeo haya ni janga la kitaifa ambalo serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kulitatua.”
Alisema janga hilo ni matokeo ya serikali kudharau madai ya muda mrefu ya walimu ambao ndiyo wadau wakuu wa elimu nchini.
Lyimo ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), alisema walimu wengi wenye uwezo wamekuwa wakiacha ualimu na kutafuta ajira katika maeneo mengine  
“Walimu wamekuwa wakipuuzwa kwa muda mrefu, wapo wanaoacha kazi ili kutafuta maslahi lakini wengine wako katika mgomo baridi na ndiyo maana ya matokeo haya,” alisema Lyimo.

No comments:

Post a Comment