Thursday, January 31, 2013

Zitto: CCM inatuchonganisha


NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, amekishutumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba kinachonganisha viongozi wa chama chake kwa lengo la kukidhoofisha wakati huu kinapoelekea kushika dola mwaka 2015.
Zitto alisema hayo jana alipokuwa anazungumza na viongozi wa CHADEMA wa matawi na kata zote kutoka Jimbo la Kigoma Kaskazini ukiwa ni mkakati wake wa kuendelea kukijenga chama na kujua matatizo ya kisiasa na kijamii yanayowakabili wananchi wake.
Mbunge huyo ambaye ameamua kupiga kambi jimboni humo kwa lengo la kuwazuia CCM wasipotoshe wananchi wake wakati huu wanapoadhimisha miaka 36 ya kuzaliwa chama chao, alisema kuwa licha ya maneno na uvumi kuzagaa kwamba CHADEMA Taifa inakabiliwa na mgogoro baina ya viongozi, jambo hilo si kweli.
Zitto alibainisha kuwa hali hiyo inakuzwa na watu waliopandikizwa na kutumiwa na CCM kwa ajili ya kuleta mpasuko na kukigawa chama ili kupunguza kasi yake ya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“CHADEMA hakuna mpasuko wala migogoro kama inavyotafsiriwa na wengi, badala yake kuna kakundi kanataka kutuhujumu kwa kutugawa kwa kutumia itikadi za kidini, kimaeneo, kimitazamo na hata kiitikadi kama walivyotumwa na hicho chama chao.
“Ninachoweza kusema ni kwamba ndani ya chama chetu kuna majungu, fitina, kuoneana wivu, usaliti na hata kumalizana kisiasa, haya tutahakikisha tunayamaliza kikatiba kwa sababu hiyo ndiyo sheria mama inayotuongoza ili tufikie malengo tuliyojiwekea,” aliongeza Zitto.
Alidai kuwa wajibu wake ni kupigania misingi ya uwajibikaji na demokrasia ndani ya CHADEMA ili kuondokana na vitendo vya uongozi wa kutumia mabavu kama ilivyo kwa CCM, ambayo imekuwa ikitumia nguvu katika kuendesha mambo yake, sambamba na serikali iliyopo madarakani.
Hata hivyo, aliwashutumu viongozi wa jimbo lake kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo katika kujenga chama na badala yake kila kitu kumtegemea yeye kama mbunge ikiwa ni pamoja na vikao na mikutano ya hadhara.
“Ili tujenge chama chenye nguvu na heshima, ni lazima viongozi wote tushirikiane kuanzia ngazi ya matawi, kata na jimbo badala ya kila kitu kunitegemea mimi mbunge, lazima tuweke misingi imara ya chama ili mgombea ajaye wa CHADEMA asipate wakati mgumu wa kufanya kampeni,” alisisitiza.
Zitto aliongeza kuwa, wakazi wa Kigoma kwa miaka mingi wamekuwa hawana mtetezi katika ngazi za kitaifa, kiasi kwamba hoja za kuendeleza mkoa kwa kupatiwa miradi ya maendeleo zinapata upinzani mkubwa kwenye vikao vya uamuzi kama vile Baraza la Mawaziri na Bunge.
“Lazima sisi watu wa Kigoma tuwe na umoja kwa sababu tumekuwa wanyonge kwa miaka mingi, na daima nguvu ya wanyonge ni umoja baina yaoNa sisi tunapaswa kuwa na umoja kwa ajili ya maendeleo ya mkoa wetu na hata hii miradi inayoletwa Kigoma sasa ni kutokana na kelele tunazopiga,” alisema.
Aliongeza kuwa hata kama hatagombea nafasi yoyote ndani ya chama, bado ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu na ataitumikia CHADEMA kwa vile misingi aliyoshiriki kuitengeneza kwa ajili ya ustawi wa chama hicho bado haijakamilika na hawezi kuiacha ikiwa hivyo.

No comments:

Post a Comment