Thursday, January 31, 2013

Spika aikoroga CCM


WABUNGE, CHAMA CHAKE WAMSHAMBULIA
HATUA ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kutangaza kuunda tume kuchunguza sakata la mzozo wa gesi mkoani Mtwara, limeikoroga serikali, Tanzania Daima limebaini.
Kutokana na hali hiyo, kauli ya Spika Makinda imepingwa na chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wabunge wengi wanaohudhuria mkutano wa kumi wa Bunge mjini hapa.
Katika mahojiano na gazeti hili, baadhi ya wabunge wakiwemo wa CCM, wameshangazwa na kauli ya Makinda kutaka kuunda tume wakati serikali kupitia waziri mkuu inachunguza jambo hilo hilo.
Naye kigogo mmoja wa CCM aliliambia gazeti hili kwamba, spika amechemsha kutaka kuunda tume sasa.
Alisema kuwa alichotakiwa kufanya ni kuitaka serikali ije na maelezo kuhusu mgogoro huo, lakini sio Bunge kuunda tume.
“Waziri Mkuu yupo Mtwara ana timu kubwa ya watendaji na vyombo vya dola kuchunguza suala hiliBunge haliwezi kwenda kuchunguza kabla serikali haijaja na taarifa yake," alisema kiongozi huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Mbunge wa Nkasi, Ally Kessy (CCM), alisema tume ya Makinda haina sababu kwani Bunge linapaswa kusubiri taarifa ya serikali.
“Tatizo la spika anafanya vitu kwa kukurupukaWaziri mkuu na timu yake wanachunguza, Bunge nalo linataka kuchunguzaTusubiri serikali inasema nini, tusiporidhika ndiyo tunaweza kuunda tume,” alisema.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msingwa (CHADEMA), alisema tume ya spika itaundwa kwa ajili ya kuwatafutia watu ulaji kwa sababu haina ulazima wa kwenda kuchunguza jambo hilo sasa.
Msigwa alisema tume hiyo inaweza kuundwa na taarifa yake isije bungeni kama ilivyotokea wakati wa mgogoro wa madaktari.
“Wakati wa mgogoro wa madaktari, spika aliiagiza Kamati ya Huduma za Jamii chini ya Margareth Sitta, iende kuchunguza suala hilo, iliporudi tukaambiwa ripoti haitajadiliwa, imepelekwa kwenye kamati, hivyo sioni umuhimu wa tume ya Bunge kwa sasa,” alisema.Akizungumzia mkorogano huo jana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema kuwa inawezekana spika alipotoa tamko hilo, hakujua hatua ambayo serikali imefikia.
“Nadhani baada ya kutoa taarifa ya serikali, tutaona kama bado kuna umuhimu wa kuunda tume ya Bunge kuchunguza,” alisema.
Pinda alimtetea Spika Makinda kwamba alikuwa na nia njema, na hakuna ubaya kama Bunge litaamua nalo kuchunguza.
Wakati akiahirisha mkutano wa Bunge juzi mjini hapa, Spika Makinda aliwafunga mdomo wabunge kujadili suala la gesi, na kwamba Bunge litaunda tume kuchunguza mzozo huo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Pinda ametangaza kumaliza mzozo huo baada ya kutembelea na kufanya mikutano na vikundi mbalimbali mkoani Mtwara.
Alisema tatizo la wananchi Mtwara lilikuwa elimu na baada ya kuwaelimisha, wameelewa.
“Tatizo lao halikuwa kupinga gesi kwenda Dar es Salaam, tatizo ni kutaka kujua wananufaika vipi na gesi yao, nimewaeleza, wamenielewa,” alisema Pinda.
Kwa mujibu wa Pinda, moja ya madai ya watu wa Mtwara ni kutaka kiwanda cha kusafisha gesi kijengwe mkoani kwao ili kutoa fursa ya ajira, na pia masalia ya gesi hiyo yabaki Mtwara ili kuwezesha kufungua viwanda vipya.
Waziri Mkuu Pinda alisema jana alilazimika kuwaita mawaziri sita ambao wameelezea mipango ya serikali kuhakikisha mikoa ya Lindi na Mtwara inapiga hatua kimaendeleo.
“Mtwara wanasema tumewaacha nyuma kwa muda mrefuHivyo nilimwita Waziri Harrison Mwakyembe, John Magufuli na wengine kila mmoja kueleza katika eneo lake atafanya nini kuleta maendeleo Mtwara na Lindi,” alisema.
Aligusia kuwa chama chake cha CCM mkoani Mtwara kina mpasuko mkubwa kutokana na sakata hilo, hali aliyosema ameifikisha makao makuu ili kutafuta muafaka.


Nchimbi: Uharibifu unatisha
Wakati huo huo, serikali imetangaza uharibifu wa mali na hasara iliyopatikana kutokana na vurugu za Mtwara ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani, DkEmmanuel Nchimbi alisema hasara iliyopatikana inatisha.
Alisema kuwa tathmini iliyofanywa katika Wilaya ya Masasi, imebaini kuwa ili ofisi ya serikali iweze kuendelea na kazi zake, inahitaji sh milioni 700 papo hapo, vinginevyo haiwezi kufanya kazi kwani kila kitu kimeteketezwa na vingine kuibwa.
Alisema tathmini ya ofisi na mali za serikali tu bila kuangalia watu binafsi, kuna hasara ya bilioni 1.3.
“Uchunguzi umebaini kuwa kundi hili la waasi lilikuwa linahama hama na pale Masasi waliteka kituo kimoja cha mafuta na kuruhusiwa kuchota petroli ya kiasi walichotaka na kwenda kuitumia kuteketeza nyumba na mali za watu wengine,” alisema.
Alizitaja nyumba na mali zilizoteketezwa Mtwara Mjini kuwa ni pamoja na nyumba ya Diwani wa Kata ya Chikongola, Mohamed Chikopa, nyumba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikao na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia ambayo ilikuwa ikiendelea kujengwa.
Alisema nyumba hiyo iliharibika kwa kupigwa mawe vioo vya madirisha, milango na kuunguzwa baadhi ya sehemu.
Nyumba nyingine iliyoshambuliwa ni ya A/INSP Jumanne Malangahe iliyopo eneo la SabasabaNyumba hiyo ilipigwa na kuchomwa godoro moja kwa kulimwagia petroli pamoja na kuharibu mita ya umeme.
Alisema jengo la Kata ya Ufukoni nalo lilichomwa moto pamoja na kuunguza nyaraka mbalimbaliMali nyingine ni gari la polisi lenye namba za usajili PT.1420 ambalo lilishambuliwa kwa mawe na kuvunjwa kioo cha mbele na pembeni.
Jengo la Mahakama ya Mwanzo ya Mtwara Mjini lilichomwa moto na kuteketea pamoja na kuteketeza nyaraka mbalimbali za mahakama hiyo.
Alisema katika maeneo ya Magomeni, duka la Mohamed All Mchanyambe ambaye ni Diwani wa Kata ya Ufukoni lilivunjwa na kuibiwa mali mbalimbali zenye thamani ya sh milioni 30.
Waziri aliongeza kuwa, katika eneo hilo la Magomeni, grocery ya askari E 8935 CPL Philimon ilishambuliwa na kuibiwa vitu mbalimbali vyenye thamani ya sh milioni 1.8 pamoja na fedha taslimu sh 250,000.
Pia alisema askari mwenye namba G.5456, PC Shabani alijeruhiwa kwa kupigwa jiwe sehemu za kichwa karibu na jicho upande wa kulia na hali yake inaendelea vizuri.
DkNchimbi alisema kuwa uharibifu uliofanywa wilayani Masasi ulikuwa mkubwa kuliko ule wa MtwaraKwamba watu wanne waliuawa kwa kupigwa risasi wakati wakiwa wanamshambulia askari kwa kumkata mapanga.
Alitaja majina ya waliouawa kuwa ni Bakari Hamisi (30), Jofrey Simonje (16) na wengine wawili ambao majina yao hadi sasa hayajafahamika.
Kwa mujibu wa DkNchimbi, magari matano ya serikali yalichomwa moto yakiwemo mawili mapya ya kubebea wagonjwa.
Magari hayo ya kubebea wagonjwa ni pamoja na SM 3840, aina ya Cruiser na gari lenye namba za usajili SM 9060 Land CruiserMengine ni namba SM 9721 aina ya Issuzu tiper, STK 8417 aina ya Toyota Prado, Land Rover na Toyota Maruti, mali ya Ofisa Takwimu.
Alisema kuwa yapo pia magari matano ya watu binafsi yaliyochomwa moto, matano ya serikali yaliyovunjwa vioo na saba ya watu binafsi yaliyovunjwa vioo.
Katika mali hizo, pia DkNchimbi alitaja pikipiki zilizoharibiwa kuwa ni nne ambazo ni TZ 98938, mali ya Fredrick Linga, T 773 BLA mali ya Hasani Said, T 688 AXH mali ya Said Nanjona na T 178 AVK mali ya Mwalimu Swani.
Alizitaja nyumba zilizochomwa moto kuwa ni ya Ofisa Elimu, nyumba na gari la Mbunge Viti Maalumu, Mariam Kasembe (CCM) na Anna Abdallah.
Aidha, alieleza kuwa Mahakama ya Mwanzo Lisekese ilichomwa moto, Ofisi ya CCM Wilaya ya Masasi Ilichomwa moto, nyumba binafsi ya askari F.3S /STG Lusekelo ilivunjwa vioo, nyumba ya askari E.4696 CPL Hasani ilichomwa moto na askari polisi D/SSGT Osiah Kibona alijeruhiwa sehemu za kichwani kwa kukatwa mapanga na hali yake ni mbaya.
Alisema askari WP5576 PC Eneck William, chumba chake kilivamiwa na kundi la watu na kuchukuliwa vitu vyote vya ndani wakati askari G238, PC Lais Saigirani nyumba yake ilibomolewa yote, askari E4696, CPL Hasani Saidi Lipemba, nyumba yake ilichomwa moto na E234 CPL Jonas Mweri, nyumba yake ilibomolewa yote.
Pia Nchimbi alisema kuwa geti kuu la kuingilia ofisi kuu ya halmashari lilivunjwa, kuondolewa kwa mabati ya uzio wa jengo jipya linalojengwa, kuungua kwa kompyuta tano za mezani, laptop nne, printa tano, scana na machine ya kurambaza.

No comments:

Post a Comment