MWANASIASA mkongwe nchini, Ibrahim Kaduma, amependekeza Katiba mpya ijayo imzuie Rais wa nchi kuwa mwenyekiti wa chama cha siasa kinachotawala.
Hatua hiyo itamfanya Rais kuwa kiongozi wa watu wote na itamsaidia anapokutana na viongozi wa vyama vya siasa kuzungumza nao wote kwa usawa na vyombo vya kitaifa kama jeshi, polisi, televisheni na radio za taifa vyote vitawatendea haki viongozi hao kwa usawa.
Kaduma alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam baada ya kuwasilisha maoni yake kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, akisema kuwa Rais asiwe na madaraka ya kuteua watu moja kwa moja huku akitaka wakuu wa wilaya na mikoa wawe watumishi wa serikali waliobobea katika sayansi ya utawala.
Pia alipendekeza kura zipigwe kwa ajili ya mvuto wa program au ilani za vyama na viti vigawiwe kwa uwiano wa kura ambazo kila chama kinapata. Mgombea ubunge au mwakilishi akifariki au kuvuliwa uongozi, chama kilichomteua kiteue mtu mwingine bila kufanya uchaguzi mdogo.
Kaduma pia alitaka suala la madini, mafuta, gesi na rasilimali nyingine ziwe mali ya taifa na Katiba itamke kuwa uvunaji wa mali hizo uhakikishe asilimia 51 inamilikiwa na wananchi.
Pia alitaka kuwepo kwa tume huru ya maadili itakayoundwa na kusimamiwa na Bunge ili kuhakikisha inachunguza mienendo ya viongozi na wakuu wa mihimili.
“Tume hiyo itasimamia uongozi wa taifa yaani Rais, Makamu wake, Spika, mawaziri, majaji, mahakimu na mawakili lakini pia wabunge, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama ili kutoa maonyo panapofaa hata kupendekeza kwa Bunge kiongozi kuvuliwa madaraka yake atakapokiuka maadili,” alisema.
Mwanasiasa huyo, aliongeza kuwa muundo wa muungano uliopo sasa uendelee kuwa kama ulivyo, huku akipendekeza kuwepo na wagombea binafsi wa urais, ubunge, uwakilishi na udiwani ili kuzuia utitiri wa wagombea.
Naye mwanasiasa mkongwe mwingine Balozi Job Lusinde, amependekeza Katiba mpya iwekwe kifungu cha kupinga rushwa nchini kwa njia yoyote hata ikiwa kwa kuingilia uhuru wa mtu.
Lusinde aliyewahi kuwa waziri wa kwanza mzalendo katika Baraza la Mawaziri wa Serikali ya Tanganyika, alisema kuwa kitendo cha kuendelea kuwalea wala rushwa hakiwezi kuiletea nchi tija yoyote hasa kimaendeleo.
Aliongeza kuwa alipendekeza kwenye Katiba kuwe na kifungu kitakachowataka wabunge wa viti maalum kuongoza kwa miaka miwili ili kuwapa nafasi wanawake wengine ambao hawajashika nyadhifa hizo.
Lusinde alipendekeza muungano ubaki kama ulivyo lakini akataka Katiba itamke mkoa wa Dodoma kuwa Makao Makuu ya Serikali kwa sababu kwa sasa haionekani kama makao makuu kutokana na kutokuwepo kwa kipengele hicho katika Katiba.
Mnyika amwandikia Jaji Warioba
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, amemwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, Jaji Joseph Warioba, akimtaka apanue wigo wa kukusanya maoni ya wananchi binafsi kwa simu za mkononi na makundi ya wananchi katika mabaraza ya Katiba.
Katika barua hiyo ambayo gazeti hili linayo nakala yake, Mnyika ameandiki akirejea maelezo ya Jaji Warioba kwenye mkutano wake na waandishi wa habari wa Januari 5 mwaka huu, kuhusu mchakato wa ukusanyaji maoni ya mabadiliko ya Katiba.
“Maelezo uliyotoa yanadhihirisha upungufu katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi binafsi unaoelezwa kukamilika kwa kuwa na idadi ndogo ya watu waliotoa maoni mpaka sasa ambapo hadi awamu nne zinakamilika jumla ya watu 318,223 tu ndio waliotoa maoni,” alisema.
Alibainisha kuwa ili kuchangia katika kurekebisha hali hiyo, tume ishirikiane na makampuni ya simu kuwezesha ujumbe wa simu ya mkononi kutumwa kwa kila Mtanzania mwenye simu kumpa dondoo za msingi za elimu ya Katiba na kumpa namba anazoweza kutuma maoni kwa njia ya simu na pia maelekezo ya namna ya kutuma ujumbe wa bure wa maoni yake.
Mnyika alisema kuwa hiyo itafanya wananchi wengi kushiriki kutoa maoni. Lakini akataka pawepo na uwazi katika mfumo mzima wa maoni yanayokusanywa kwa njia ya simu na mitandao mingine ya intaneti ili ufuatiliaji uweze kufanyika kwa ufanisi.
“Kwa upande mwingine ili kurekebisha upungufu uliojitokeza kwenye awamu nne za ukusanyaji maoni ya wananchi binafsi, marekebisho na maboresho ya haraka ya ratiba na utaratibu yanapaswa kufanyika kwenye awamu ya ukusanyaji wa maoni ya makundi mbalimbali na hatua inayofuata ya kuunda mabaraza ya Katiba,” alisema.
Alibainisha kuwa kabla ya kutangaza na kusambaza utaratibu iliouita ni namna bora ya kidemokrasia ya kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba kwa kuchaguliwa na wananchi wa maeneo husika, tume iweke wazi kwa umma mapendekezo na kutumia mikutano yake ya makundi mbalimbali inayoendelea.
Mnyika aliongeza kuwa kwa kuzingatia upungufu uliojitokeza wa tume, mikutano 1776 tu na wananchi wachache kutoa maoni kutokana na sababu mbalimbali, mabaraza ya katiba yanapaswa kuundwa kuanzia katika ngazi ya kata badala ya utaratibu unaondaliwa na tume wa kuunda mabaraza hayo katika ngazi ya wilaya.
No comments:
Post a Comment