Friday, January 25, 2013

Mrema aiponda CCM


Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustino Mrema, amesema serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imekuwa ikila rasilimali za wananchi kwa mikono miwili bila kunawa tangu uhuru hadi sasa, ndio sababu wananchi wamefikia hatua ya kutoiamini tena.
Mrema ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo, alisema hayo nyumbani kwake Sinza jijini Dar es Salaam jana katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima yaliyolenga masuala mbalimbali ya kitaifa likiwemo sakata la gesi linalotikisa nchi sasa.
Alisema kuwa kinachotokea Mtwara sasa ni wananchi kuwa na wasiwasi juu ya rasilimali pekee waliyojaliwa na Mungu wakitaka haki ya kunufaika nayo.
Mrema alifafanua kuwa siku zote ilipopatikana rasilimali, serikali imekuwa ikikwapua zote na kuwaacha wananchi wanaozunguka eneo hilo bila kitu chochote.
“Wananchi wa Mtwara wameona jinsi watu wa Geita, Nyamongo hata Mererani wanavyoachwa na mashimo bila wao kunufaika na rasilimali zinazopatikana kwao,” alisema.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, alitolea mfano wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) akisema kuwa serikali imekuwa ikisisitiza kwamba wananchi ni marafiki wa eneo hilo ili walitunze.
“Lakini tumeona wanaonufaika na rasilimali zile si wananchi wanaozunguka pale, wao huombwa kama majirani kuzima moto iwapo ukiwaka ila kunapokuwa hali shwari, wanaonekana ni maadui, wanabakwa na wanapigwa,” alisema.
Alionya kuwa serikali isipokuwa makini na suala hilo itarutubisha ugaidi, maana haitaweza kulinda bomba la gesi kuanzia Mtwara hadi Dar es Salaam na kwamba ikae na wananchi waelewane badala ya kuwatukana na kuwabeza.
“Serikali ikae nao iwasilikilize maoni yao ili iwaweke wazi watanufaika vipi na upatikanaji wa gesi katika mkoa wao. Wanamtwara sio waasi, ni watu wazuri wanawapenda Watanzania wengine, hawajakataa gesi ije Dar es Salaam ila wanataka kuhakikishiwa wao watanufaika vipi na gesi iliyopatikana kwao.
“Hiyo ni neema pekee walioyojaliwa na Mungu. Tuache kuwapaka matope wananchi wa Mtwara, tunawazushia mambo ambayo sio ya kweli kwa kuwa tunataka kuwaibia gesi yao,” alisisitiza.
Alishauri serikali iwekeze zaidi katika mkoa wa Mtwara hadi mji huo uonekane tofauti na miji mingine katika nchi kwa kigezo pekee cha upatikanaji wa gesi katika mkoa huo.
Mwanasiasa huyo mkongwe aliongeza kuwa Mtwara lazima iendelezwe ionekane tofauti na eneo ambalo halina gesi, iwe na zahanati, shule, barabara na huduma zingine nzuri za kijamii.
“Tabia ya serikali ya CCM tangu uhuru ni kuongoza kwa usanii na sasa kuleta uasi wa wananchi, wananchi wana wasiwasi hawaamini kama wanayoambiwa na serikali ni ya kweli,” alisema.
Kuendelea kuvutana na wananchi wa Mtwara badala ya kukaa nao chini kuwasikiliza, kutaibua makundi mawili ambapo Wanamtwara watasema gesi ni yao huku serikali ikisema gesi ni ya wote kwa kigezo cha Utanzania, jambo alilodai linaweza kuibua hata vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Mrema alibainisha kuwa wananchi wa sasa hawaogopi na kwamba katika suala hilo la gesi, wananchi wa Mtwara ndio wenyeji, hivyo akahoji inakuwaje wenyeji wadharauliwe katika mkoa wao ilikogundulika rasilimali itakayonufaisha taifa.
Akizungumzia hatua ya wanasiasa wa upinzani wanaounga mkono serikali isafirishe gesi kuja Dar es Salaam, Mrema bila kutaja majina alisema kuwa wanatakiwa wachukue muda kuelewa mahitaji ya wananchi na sio kukurupuka.
“Viongozi waende Mtwara kueneza sera za maendeleo si kukemea wananchi na kuwabeza kwa kujipendekeza kwa chama tawala,” alisema.
Hivi karibuni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia pamoja na baadhi ya wabunge wa chama hicho, walinusurika kupigwa na wananchi wa Mtwara wakiwa kwenye mkutano wa hadhara baada ya kuwashawishi wakubaliane na uamuzi wa serikali kusafirisha gesi hiyo kuja Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment