AAMBIWA SULUHU YA MTWARA SI KUPIGA WANANCHI RISASI
MOTO wa gesi asilia unazidi kumwakia Rais Jakaya Kikwete, ambapo vyama mbalimbali vya siasa na viongozi wakuu wa dini nchini wameendelea kumtaka kiongozi huyo avunje ukimya na kuingilia kati.
Wakati hali ikiwa tete huku Waziri Mkuu Mizengo Pinda akijaribu kusaka suluhu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF) na Askofu Mkuu wa Anglikana nchini, wametoka msimamo mzito kuhusu sakata hilo.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, jana alitoa msimamo wa chama chake kwenye kikao cha dharura cha Baraza Kuu, akisema wako pamoja na wananchi wa Mtwara na kwamba serikali inapaswa kusikiliza sauti yao.
Wao CUF kupitia kwa Waziri wao wa Afya wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Mapinduzi ya Zanzibar, Juma Haji Duni, alisema mauaji ya raia wema wanaodai haki yao ya gesi asilia yanayofanywa na polisi hayakubaliki.
Yeye Askofu Valentino Mokiwa alimtaka Rais Jakaya Kikwete kuacha ukimya na badala yake asitishe ziara zake nje ya nchi aende Mtwara kusikiliza kilio chao na kupata ufumbuzi wa haraka.
Akifungua kikao cha Baraza Kuu, Mbowe alisema ni wakati wa serikali kusitisha mara moja mpango huo wa kusafirisha gesi hiyo kwenda Dar es Salaam na ikae na wananchi kwa ajili ya kupatia ufumbuzi.
“Haya yanayotokea leo mkoani Mtwara ni matokeo ya wananchi kuchoka na ufisadi unaofanywa na serikali ya CCM, wanachofanya Mtwara sio jambo la kusifu ila ni ujasiri wa kupongezwa,” alisema.
Alisema serikali ya CCM kwa sasa inapaswa kujiandaa kutoa maelezo ya mrejesho wa madini katika maeneo mbalimbali ya nchi, usafirishwaji wa meno ya tembo pamoja kuweka wazi mikataba zaidi ya 26 katika sekta ya uchimbaji wa gesi nchini.
Mbowe alisisitiza kuwa serikali haiwezi kuwa na nia ya dhati ya kuwasikiliza wananchi kwa kuwa miongoni mwa wamiliki wa makampuni yanayochimba gesi ni ya viongozi wa CCM ikiwemo Katibu Mkuu wake Abdulrahman Kinana kupitia makampuni hayo (Artimax).
Mbali na Kinana Mbowe pia alimtaja kiongozi mwingine wa CCM mwenye maslahi binafsi katika gesi kuwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, ambaye pia ni Mbunge wa Newala.
“Wakati wa kubembelezana katika kutekeleza wajibu kwa wananchi umepitwa na wakati na suala la wananchi kudai rasilimali ziwanufaishe halitaishia Mtwara pekee bali litaenda kila eneo nchi nzima,” alisema.
Duni asema yahusuyo CUF
Akihutubia mkutano wa hadhara juzi jijini Mwanza kwa ajili ya kumbukumbu ya wafuasi wa CUF waliouawa na polisi katika maandamano ya Januari 26 na 27 mwaka 2001 mjini Zanzibar, Duni alisema utawala unaoua raia wake umekosa hoja za kuwaongoza Watanzania.
Alisema kuwa mauaji ya raia wanaodai haki yao kamwe hayakubaliki huku akitolea mfano wa utawala wa serikali za Libya, Misri na Tunisia ulivyoangushwa na wananchi akisema hiyo ni fundisho kwa watawala wanaotumia mabavu na kushindwa kutatua kero zinazolikabili taifa.
Duni ambaye alikuwa akitumia jina la ‘wauaji hawa’, alisema Tanzania haijafikia hatua ya kuuana wala kuhasimiana kama ilivyowahi kutokea huko Zanzibar.
Alifafanua kuwa kilio cha wananchi wa Mtwara ambao alidai wametelekezwa na serikali, hakiwezi kutatuliwa kwa mtutu, mabomu na risasi bali ni kwa mazungumzo na maelewano.
“Mtawala yeyote anapoanza kutumia risasi kuua wananchi wake wanaodai haki, huyo amekosa hoja za kuongoza nchi. Kule Libya na Misri tuliona jinsi watawala wake walivyoamua kutumia mtutu kuua raia wanaodai haki yao ya msingi. Lakini utawala huo uko wapi sasa?” alihoji.
Waziri Duni ambaye pia ni mjumbe wa Baraza Kuu la CUF Taifa, alisema wananchi wa Mtwara wameonekana kutelekezwa na serikali yao kwani licha ya kuwa umbali wa kilometa 60 hakuna barabara nzuri inayounganisha kati ya mkoa huo na Dar es Salaam.
Alimshukia pia Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kuwa ni Rais wa kwanza Tanzania aliyesababisha umwagaji damu ya wananchi wake Januari 27 mwaka 2001, kisha kuzalisha wakimbizi wa kisiasa.
Kuhusu vyama vya siasa, aliwaomba viongozi wa CHADEMA, NCCR-Mageuzi, CUF na vyama vingine vya upinzani kuungana na kuweka mgombea mmoja wa urais mwaka 2015 ili kuiondoa kirahisi madarakani CCM.
Askofu Mokiwa anena
Naye Askofu Mkiwa aliiambia Tanzania Daima kwa simu jana kuwa ni muhimu uongozi ulio madarakani ukajiepusha kupuuza madai ya wananchi wa Mtwara.
Dk. Mokiwa alisema kwa kuwa Rais Kikwete ametokana na wananchi hivyo kuna ulazima wa kuwapa nafasi ya kuwasikiliza ili kujua mahitaji yao kuliko anavyokaa kimya hatua inayoweza kutafsiriwa vibaya.
“Serikali ni lazima isiwakilize wananchi wake hata kama wengine wanaonekana kuwa hawafai…uongozi bora siku zote unashirikisha wananchi wake,” alisema.
Aliongeza kuwa suala la gesi linahitaji ushirikishwaji wa pamoja na kwamba serikali ni muhimu ikawekeza katika mikoa ya kusini ambayo inaonekana kusahaulika kwa kipindi kirefu.
Askofu Mokiwa alifafanua kuwa kama kuna uwezekano wa kujenga viwanda katika mkoa huo hakuna ulazima wa gesi hiyo kusafirishwa na kuletwa jijini Dar es Salaam kwani itazidisha msongamano wa watu.
“Ni lazima tuige mifano ya nchi za wenzetu ambapo hawaweki vipaumbele kwa eneo moja pekee, mara zote wanatawanya viwanda vyao hivyo nasi hakuna ulazima wa kujenga viwanda hapa; tutawanye na kuvipeleka eneo lingine,” alisema.
Alisema kuwa hatua ya kutokea kwa vurugu za mara kwa mara kuhusiana na raslimali ya gesi inatokana na ushahidi wa huko nyuma kwani rasilimali nyingi zilizopo hazikuwahi kuwafaidisha Watanzania.
Dk. Mokiwa aliongeza kuwa Watanzania wanajua kuwa serikali imeshindwa kutimiza ahadi nyingi pamoja na kupatikana kwa gesi hiyo bado tatizo la umeme litaendelea kuwatesa.
No comments:
Post a Comment