Monday, January 28, 2013

Lema kuiteka Dodoma


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Dodoma kimeandaa mapokezi makubwa ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbles Lema, kesho akiwa anarejea mjini humu kuhudhuria vikao vya Bunge kwa mara ya kwanza baada ya kushinda rufaa yake ya kupinga kuvuliwa ubunge.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu wa Chadema Mkoa wa Dodoma, Stephen Massawe, iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, Lema anatarajiwa kupokewa katika eneo la Ihumwa, nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma.

Massawe alisema baada ya mapokezi hayo, Lema atakwenda moja kwa moja hadi viwanja vya Shule ya Sekondari ya Central mjini hapa.

Massawe alisema mapokezi hayo yameandaliwa kwa lengo la kumpongeza Lema kwa kushinda rufani yake.

Pia yanalenga kumpongeza Lema kwa kazi alizofanya za kuimarisha chama katika kipindi ambacho ubunge wake ulitenguliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha.

Alisema ukomavu wa kisiasa wa Lema na ushirikiano na wenzake, vimeleta chachu kubwa kwa ujenzi wa Chadema na kukifanya chama hicho kusonga mbele zaidi.

Massawe alisema baada ya mapokezi hayo, Lema atawahutubia wakazi wa Manispaa ya Dodoma katika mkutano wa hadhara utakaofanyika katika viwanja wa Shule ya Sekondari ya Central. Alisema Lema atafuatana na wabunge kadhaa pamoja na viongozi wa kitaifa wa chama hicho, ambao nao watapata nafasi ya kutoa salamu kwa wananchi.

“Lema tumemwandalia mapokezi ya kifalme katika mkoa wetu. Tumetambua kwa muda wa miezi tisa aliyokaa nje ya Bunge, amefanya kazi kubwa ya kujenga chama. Lema ameonyesha ujasiri mkubwa katika kutenda kazi yake kipindi akiwa bungeni na pale alipokuwa nje ya Bunge,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:

“Cha kumshukuru Mungu zaidi ni kurudi kwake bungeni. Ataendelea kuibua madudu, ambayo yanafanywa na serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi.”

Lema alivuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Aprili 5, mwaka jana, baada ya mahakama hiyo kukubaliana na hoja mbili za ushahidi uliotolewa na wadai.

Kati ya madai manne yaliyowasilishwa mahakamani hapo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Gabriel Rwakibarila, aliyekuwa akisikiliza shauri hilo baada ya kujitoa kwa Jaji Aloyce Mujulizi, Februari 6, mwaka jana, alikubaliana na madai mawili hivyo kutengua ubunge wa Lema.

Jaji Rwakibarila alisema mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa kwamba, Lema katika mikutano yake ya kampeni za uchaguzi iliyofanyika kuanzia 20 Agosti hadi Oktoba 30, 2010 alitumia lugha za kashfa dhidi ya aliyekuwa mgombea wa nafasi hiyo kwa tiketi ya CCM, Dk. Batilda Buriani.

Alinukuu baadhi ya maneno aliyotamka Lema kwenye mikutano hiyo na kutolewa ushahidi na wadai ni kama, “Dk. Batilda siyo mwaminifu, amezaa na Mzee wa Monduli na alipo hapo ana mimba nyingine ya Lowassa (Edward),” kuwa ni baadhi ya matamshi ya kashfa, ambayo hayakubaliki kwenye kampeni za uchaguzi.

Pia alisema mahakama imeridhika na ushahidi kuwa Lema katika mikutano yake ya kampeni alitumia hoja ya ubaguzi wa kijinsia dhidi ya Dk. Batilda kwa lengo la kushinda.

Alisema ushahidi uliotolewa umethibitisha Lema alitamka kwenye mikutano yake kwamba, “Tangu lini mwanamke akawa kiongozi wa malaigwanan," akisisitiza kuwa hayo ni maneno ya ubaguzi wa kijinsia.

Jaji Rwakibarila alisema madai na ushahidi uliotolewa umeiridhisha mahakama hiyo kuwa Lema alikiuka kifungu 108 cha Sheria ya Uchaguzi,1985, kinachozuia kufanya kampeni kwa misingi ya ubaguzi wa kikabila, kijinsia, kidini au rangi.

Kwa msingi wa ushahidi uliotolewa hapa, mahakama imeridhika kwamba Lema alikiuka Sheria ya Uchaguzi katika kampeni zake na kwa hivyo, matokeo ya uchaguzi wa ubunge wake yanatenguliwa kama ilivyoombwa na wadai. Kesi hiyo namba 13/2010 ilifunguliwa na wapigakura watatu wa CCM; Musa Mkanga, Happy Kivuyo na Agness Mollel, kupitia kwa wakili wao, Alute Mughwai, akisaidiana na Modest Akida.

Waliiomba mahakama kutengua matokeo ya ubunge wa Lema kwa kukiuka kanuni, taratibu na sheria za uchaguzi. Walidai wakati wa kampeni Lema alimdhalilisha kijinsia Dk. Batilda kwa kutoa lugha za matusi kuwa yeye ni Mzanzibari na siyo mwaminifu katika ndoa yake.

Makada hao wa CCM walidai Lema alifanya udhalilishaji huo katika vituo 22 vilivyokuwa vinatumika kufanya kampeni za uchaguzi, ambako alitoa lugha za kashfa na ubaguzi wa kidini na kijinsia na kwamba lugha hizo ziliathiri matokeo ya uchaguzi katika jimbo hilo.

Hata hivyo, mahakama hiyo ilitupilia mbali malalamiko mawili ya wadai kwamba, Lema alitumia hoja za udini na ukazi.

Jaji Rwakibarila alisema mashahidi waliopelekwa mahakamani hapo wameshindwa kuthibitisha madai hayo.

Alisema suala la Dk. Batilda kukaa Zanzibar na kugombea ubunge Arusha Mjini hilo peke siyo haramu.

Kuhusu madai ya udini, Jaji Rwakibarila alisema mahakama haijaridhika na ushahidi uliotolewa kwa sababu mashahidi hawajathibitisha kwamba wanaovaa vilemba kichwani ni al Qaeda.

Alisema kuvaa kilemba kichwani ni heshima na hivyo, wapo wanawake wengi wanaovaa vilemba. Lema, ambaye alikuwa mlalamikiwa wa kwanza alikuwa akitetewa na Wakili Method Kimomogoro, wakati aliyekuwa mlalamikiwa wa pili, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) alikuwa akitetewa na mawakili waandamizi wa serikali; Timon Vitalis na Juma Masanja.

Hata hivyo, Desemba 21, mwaka jana, Mahakama ya Rufani ilimrejesha bungeni Lema ikiwa ni takribani miezi tisa tangu alipovuliwa wadhifa huo na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha.

 Mahakama hiyo ilimrejesha Lema bungeni, baada ya kushinda rufaa yake ya kupinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Hukumu hiyo iliyosomwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Elizabeth Mkwizu, ilimtambua Lema kuwa mbunge halali wa Arusha Mjini na kuwaamuru wajibu rufaa kumlipa gharama za rufaa hiyo.

Katika hukumu hiyo iliyoandikwa na Jaji Bernard Luanda kwa niaba ya wenzake wawili Natalia Kimaro na Salum Massati waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo, Mahakama ya Rufani ilisema wajibu rufani hawakuwa na haki ya kisheria kufungua kesi dhidi ya Lema kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi.

“Rufaa imefanikiwa na tunatengua hukumu, tuzo na amri ya Mahakama Kuu. Tunamtangaza mrufani kuwa Mbunge wa Arusha Mjini,” ilisema Mahakama ya Rufani katika hukumu yake hiyo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment