Monday, January 21, 2013

Moto wa gesi wazidi kushika kasi Mtwara


SAKATA la kupinga ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam limechukua sura mpya baada ya wananchi zaidi ya 30,000 kusaini katika fomu maalumu kupinga gesi hiyo kusafirishwa.
Wakati wananchi hao wakikamilisha shughuli hiyo na kukabidhi fomu hizo kwa wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF), umoja wa vyama tisa vya siasa mkoani umemwomba Rais Jakaya Kikwete kusitisha mradi huo ili kuepusha uvunjifu wa amani unaoweza kujitokeza.
Pia, umoja huo umewataka wabunge wote wa Mkoa wa Mtwara kutangaza msimamo wa kila mmoja juu ya gesi kwenda Dar es Salaam au kukubaliana na uamuzi wa Serikali ili wajue nani msaliti kwao.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika Uwanja wa Sabasaba mjini hapa, viongozi hao kwa nyakati tofauti wamemtaka Rais Kikwete kutokutumia ‘jazba na mabavu’ katika kulipatia suluhu jambo hilo, badala yake busara zitawale kwa kusitisha mradi huo.
“Sisi Watanzania hatujazoea vita, bali tumezoea kupata hasara… katika hili naomba Kikwete akubali kupata hasara kama tunavyokubali hasara nyingine…Sisi wananchi tupo radhi tuingie kwenye deni kubwa kama hilo, lakini gesi haiwezi kwenda Dar es Salaam,” alisema Uledi Abdallah Makamu, Mwenyekiti wa umoja huo na kuongeza:
“Hizo trilioni tatu kama anaona hawezi kuzilipa iwapo gesi itabakia Mtwara...Basi atafute njia nyingine za kulipa… Atambue kuwa hakuna fedha yenye thamani ya amani na utulivu wetu…akumbuke kuwa mafahali wawili hawakai zizi moja.”Naye Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mtwara Mjini, Mustafa Nchia aliwataka wabunge kutoa misimamo yao ili wananchi wajue ni mbunge yupi anawaunga mkono na yupi msaliti kwao.
“Hadi sasa ni Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini), George Mkuchika, (Newala), Asnain Murji (Mtwara Mjini) na Clara Mwatuka (Viti Maalum CUF), wametoa misimamo yao, vipi ninyi wengine…Tunataka kusikia msimamo wa kila mmoja,” alisema Nchia huku akishangiliwa na mamia ya watu waliohudhuria mkutano huo.
Zitto ampinga Kikwete
Wakati Rais Kikwete akisisitiza kuwa mgogoro kuhusu gesi unachochewa na wanasiasa kwa lengo la kukwamisha juhudi za Serikali za kumaliza tatizo la mgawo wa umeme,  Mbunge wa Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe amesema huo ni uzushi. Katika taarifa yake jana, Kabwe alisema Serikali haitashinda vita hii kwa kuzusha kwamba wanasiasa wanaopinga wanatumika na kampuni nyingine au kwa mataifa ya magharibi kutaka kuvuruga nchi.
“Serikali ijitazame yenyewe. Bila kufanya hayo tunayo pendekeza, wananchi wataendelea kupigania haki yao...Hii ni vita ya uwajibikaji. Wananchi wanataka kufaidika na rasilimali za nchi yao.
Kwa mujibu wa Zitto, Serikali imekuwa ikitoa majibu ya porojo na kuwatusi watu wa Mtwara, na kama ilivyozoeleka Rais Kikwete na mawaziri wake wamekuwa wakisema suala la Mtwara linatumika na wanasiasa kujitafutia umaarufu.
“Inasikitisha sana kuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwaambia mabalozi wa nchi za kigeni waliopo hapa nchini kuwa yanayoendelea mkoani Mtwara yanachochewa na wanasiasa tuliosimama na wananchi wanaodai kufaidi utajiri wa nchi yetu. Rais Kikwete na mawaziri wake wameshindwa kabisa kuonyesha uongozi katika suala hili na hatimaye kuhatarisha umoja wa kitaifa.”
Aliongeza kuwa anafahamu kwamba Ubalozi wa China umeandika barua serikalini kuwaondoa raia wa China waliopo Mtwara kwa hofu ya maisha yao. Serikali inaficha ukweli huu kama ilivyoficha ukweli kwamba Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alifukuzwa na wananchi alipokwenda huko hivi majuzi. Serikali itaficha ukweli mpaka lini?” alihoji.
Waziri na wanasiasa
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene amesisitiza kuwa mgogoro na vurugu zinazoendelea mkoani Mtwara kuhusu gesi unachangiwa na wanasiasa.
Alisema kuwa watu hao aliodai wanakosa uzalendo na utaifa, wanalenga kuhakikisha tatizo la umeme linaendelea kuwepo nchini hadi uchaguzi mkuu ujao ili wapate ajenda ya kisiasa jukwaani.
Simbachawene aliyekuwa Arusha kuhudhuria Mkutano wa mawaziri wa Nishati wa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (EAPP), alisema asilimia 15 ya gesi inayokusudiwa kusafirishwa kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam itamaliza kabisa tatizo la umeme nchi ndani ya kipindi cha miezi minane baada ya mitambo hiyo kuanza kuzalisha umeme.
Kwa upande wa Mkoa wa Mtwara, Simbachawene alisema wakazi wake watanufaika na mgawo wa asilimia 0.3 ya fedha zote zitakazopatikana kutoka na mauzo ya gesi ndani na nje ya nchi ambazo zitatumika kuboresha maisha ya wananchi kwa kujenga miradi ya miundombinu, elimu, afya na kilimo.
“Baada ya gesi kuanza kuzalishwa na kuuzwa, kazi ya wananchi wa Mtwara kupitia halmashauri zao za wilaya  itakuwa ni kusoma mita kuangalia kiasi gani kimekwenda Dar es Salaam na kimeingiza fedha kiasi gani na kukokotoa asilimia zao ambazo lazima zirejeshwe kwa ajili ya maendeleo yao,” alisema Simbachawene
Mwananchi

No comments:

Post a Comment