MBUNGE wa Karatu (CHADEMA), Mchungaji Israel Natse, ametoa miezi miwili kwa Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Teresa Huvisa, kufika katika chanzo cha maji cha Qanded kutatua mgogoro uliopo kabla watu hawajatumia nguvu ya umma.
Mchungaji Natse, alitoa kauli hiyo jana mjini Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema chanzo cha maji cha Qanded, ni chanzo pekee kinachofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, lakini baadhi ya watu katika bonde hilo, kwa nia ya kutaka utajiri wa haraka haraka, wamevamia na kuweka mashine za kuvuta maji.
Mchungaji Natse, alisema hatua kadhaa zimechukuliwa ili kukinusuru chanzo hiki bila mafanikio, ambapo viongozi wa Serikali ya wilaya walifika katika eneo hilo na kuagiza wavamizi hao wakamatwe.
“Lakini cha kushangaza wavamizi hawa, walipelekwa kituo cha polisi Karatu na katika hali ya kushangaza, wavamizi hao, waliachiwa bila kuchukuliwa hatua zozote,” alisema Mchungaji Natse.
Aliwataja wavamizi hao, kuwa na vigogo kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao majina yao anayo mpaka sasa.
“Ndugu wanahabari, naomba Serikali ifanye yafuatayo ili kuleta haki, kwanza iwalazimishe viongozi wake waondoe mara moja mashine zao katika chanzo cha Qanded kwa maslahi ya wananchi wote wa bonde la Eyasi na kwa kizazi kijacho na waache ubinafsi.
“Pili, naomba pia mawaziri wa Maji na Mazingira, wafike katika eneo hili mapema iwezekanavyo kujionea wenyewe jinsi tatizo lilivyo kubwa na hatua zichukuliwe. Hatutaki wananchi wafikie hatua ya kukosa uvumilivu,” alisema Mchungaji Natse.
Alisema kama Serikali haitachukua hatua stahiki kwa wavamizi hao, basi wasije wakalaumiwa kwa wananchi kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya kulinda chanzo hicho.
Mtanzania
No comments:
Post a Comment