Tuesday, January 15, 2013

Makinda ataka mabunge mawili


ASEMA SPIKA, MAWAZIRI WASIWE WABUNGE
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, amependekeza kuwa katika Katiba Mpya ijayo iruhusu kuwapo kwa mabunge mawili; yaani hili la sasa na jingine la seneti kama ilivyo kwa nchi za Marekani na Uingereza.
Makinda alisema kuwa sababu kubwa ya kuwapo kwa mabunge hayo ni kutokana na viwango vya elimu vya wabunge wengi wa sasa kuwa vya kawaida, hivyo kuhitaji Bunge la seneti litakalokuwa na wabunge wenye upeo zaidi.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, baada ya kuwasilisha maoni yake kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Makinda alisema wabunge wa sasa wamekuwa na tabia ya kujadili hoja za kitaifa lakini mwishowe wanazigeuza kuwa za vyama vyao.
“Kuna umuhimu wa kuwa na Bunge la seneti ambalo wabunge wake watakuwa na uzoefu wa kutambua na kupambanua mambo kwa masilahi ya taifa bila kuingiza vyama,” alisema.
Makinda pia alisema kuwa katiba mpya itamke kuwa Spika wa Bunge asitokane na vyama vya siasa na asiwe mbunge ili awe na maamuzi huru badala ya kutetea vyama.
Pia alisema kuwa, kwa sababu shughuli za Bunge zimekuwa nyingi na Bunge limepanuka, amependekeza wawepo manaibu katibu wawili watakaosaidiana kuendesha shughuli za Bunge.
Aliongeza kuwa amependekeza mawaziri wasiwe wabunge ili wafanye kazi kwa usawa, kwani kwa sasa usawa haupo kutokana na mawaziri wengi kupendelea majimbo yao.
Aidha, alisema kuwa viti maalumu vinahitajika kuwapo, kwani mfumo dume bado upo majimboni, na kueleza kuwa vikiondolewa wanawake watakuwa nyuma, lakini akaongeza kuwa kwa sasa wanawake bado wanaendelea kuelimika.
Kuhusiana na kuweka ukomo wa ubunge, alisema kuwa hakuna sababu, kwani kuna baadhi ya wabunge wanang’ara majimboni kwao kutokana na kutimiza ahadi zao kwa wananchi.
Naye Jaji Mkuu, Chande Othman Chande, alisema kuwa amependekeza katiba mpya ilinde kwa namna yoyote Mahakama, kwani si mhimili unaofungamana na upande wowote, hivyo usiingiliwe na siasa, kwani ni sehemu pekee haki inapopatikana.
Alisema kuwa wamependekeza katiba mpya itambue haki ya mwananchi kupata fursa ya kupata haki na Serikali iwajibike kumpa mwananchi fursa ya kupata haki, kwani kwa sasa Tanzania haimpi mwananchi haki.
“Nipo hapa kutoa maoni kwa niaba ya watenda kazi wote wa Mahakama, majaji, mahakimu na wafanyakazi wengine wapatao 6,000, lakini sisi tunataka katiba mpya impatie mwananchi haki ya kupata fursa ya kupata haki, kwa mfano kuna mikoa 12 haina mahakama kuu na wilaya zaidi ya 25 hazina mahakama za wilaya, sasa katiba itoe fursa ya kupata haki yake,” alisema.
Pia alisema kuwa katiba mpya itambue nchi inatawaliwa na misingi ya katiba, pia utawala wa sheria utawale lakini katiba ya sasa haisemi hivyo, ikiwemo mihimili yote kuongozwa na katiba.
Kuhusu uteuzi wa majaji, alisema kuwa wamependekeza katiba mpya ipanue Tume ya Utumishi wa Mahakama, kwa kutoka majaji sita wanaounda tume hiyo na kufikia 12.
Alisema kuwa wanapendekeza watakaoongezwa wawe ni mtumishi wa Mahakama, mtu wa kawaida, haki za binadamu, tume ya umma, mawakili na mkufunzi wa Kitivo cha Sheria ili rais ashauriane na tume hiyo katika kuteua majaji.

No comments:

Post a Comment