Friday, January 25, 2013

Lusinde ataka Katiba iwabane wala rushwa


Aliyekuwa Waziri wa kwanza katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya kwanza ya Tanganyika, Balozi Job Lusinde, amesema katiba mpya iwe na vifungu vyenye sheria kali kwa ajili ya kushughulikia masuala ya utoaji na upokeaji rushwa.

Balozi Lusinde alitoa mapendekezo hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasilisha maoni yake kuhusu kuundwa kwa Katiba Mpya mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Balozi Lusinde alisema ni lazima katiba ijayo iwe na vipengele vinavyoeleza kupiga vita rushwa hata kwa njia zisizokuwa za kawaida kwa ajili ya kutetea haki.

Alisema katiba mpya inapaswa kuwa na vipengle vinavyoruhusu hata kuingilia uhuru wa baadhi ya watu kupiga vita dhidi ya rushwa ili haki iweze kupatikana.

“Katiba Mpya, ionyeshe kupiga vita dhdi ya rushwa hata kwa njia zisizokuwa za kawaida hata ikiwezekana kuingilia kati uhuru wa mtu ili kupata haki,” alisema Balozi Lusinde.
Balozi Lusinde pia amependekeza kuwa katiba mpya iwe na kifungu kinachoruhusu kuendelea kuwapo kwa viti maalum bungeni.

Kwa upande wa Muungano, alipendekeza kuwa katiba ijayo iendelee kusisitiza kuwa Tanzania ni serikali ya nchi mbili kama ilivyo sasa.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Africa Insurance ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Makumira, Ibrahim Kaduma, ametaka katiba mpya itamke waziwazi kuhusu umuhimu wa kuwa na tume huru ya maadili ambayo itateuliwa na Bunge kutokana na mapendekezo ya wananchi.

 “Maadili ya taifa lolote ni msingi wa maisha au nguzo ya maslahi ya taifa ambayo inatawala tabia na mwenendo wa watu, taasisi na vyama vya siasa katika kuweka malengo yao ya kutawala kuongoza au kuandaa mipango ya maendeleo ya taifa. Kwa Tanzania ya leo tatizo la msingi katika mifumo ya maisha na taasisi za kijamii, kiuchumi, kisiasa na kidini ni kukosekana kwa falsafa ya taifa inayoongoza sera zao jambo hilo linatokana na kutokuwapo kwa dira ya taifa,” alifafanua Kaduma.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment