Wednesday, January 23, 2013

Chadema: Ufisadi utaiua CCM


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemshukia Katibu wa Itikadi na Uenezi  wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, kwamba Chadema haitakufa badala yake CCM ndiyo itakufa kutokana na saratani ya ufisadi inayowaandama viongozi wengi na wanachama wa chama hicho.

Mkurugenzi wa Oganizesheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaila, alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam kujibu madai yaliyoyatoa Nnauye na kunukuliwa na vyombo vya habari kwamba Chadema kitakufa kutokana na laana ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Kigaila alisema suala la Chadema kufa kama baadhi ya viongozi wa CCM wanavyobashiri halipo kwasababu chama kinaweza kufa pale tu kinapoacha kusimamia maslahi ya  umma jambo ambalo limekuwa likifanywa na Chadema  kuliko hata chama tawala.

“CCM ndiyo itakufa sababu inakabiliwa na kansa ya ufisadi, kila mmoja anajua mafisadi wametajwa ndani ya CCM kwa miaka kadhaa lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi yao na badala yake wanaendelea kupewa nafasi za uongozi ndani ya chama,” alisema Kigaila.

Alisema CCM imebaki kuwa kikundi cha mafisadi wachache ambao wanatumia rasilimali za nchi kujinufaisha huku idadi kubwa ya Watazania wakiendelea kuteseka kwa kukabiliwa na hali ngumu ya maisha.

Kigaila alisema pamoja na kwamba mafisadi ndani ya CCM wanafahamika, Chadema haiwezi kuchukua hatua za kuwashitaki mahakamani kwasababu kazi ya chama cha upinzani ni kukosoa, kushauri na kuelekeza kwa lengo la kushinikiza hatua ziweze kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa lakini bahati mbaya hakuna hatua zinazochukuliwa.

“Chadema haiwezi kuwashitaki mafisadi mahakamani, huwezi kupeleka mashtaka polisi ambao wapo chini ya CCM, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) anayomamlaka ya kufuta kesi yeyote, sheria inamruhusu hivyo, Chadema tunasema mahakama yetu ni Watanzania ambao wataweza kutoa hukumu kulingana na mambo wanayofanywa ndani ya serikali ya CCM,” alisema Kigaila.

Alisema miaka ya 80 CCM ilithubutu kuwachukulia hatua viongozi waliokwenda kinyume na matakwa ya chama lakini hivi sasa hakiwezi hata kuchukua hatua hiyo hata kwa Katibu wa CCM wa Tawi.

“CCM siyo chama cha siasa sasa, siyo tena cha wafanyakazi na wakulima, hakitetei tena maslahi ya wanyoge, kimebeba wenye fedha na mabwanyenye,” alisema Kigaila.

Alisema uwezo wa kuthubutu na kuchukua hatua ndiyo umekuwa moja ya sababu ya Watanzania kuiunga mkono Chadema katika harakati zake za kuleta mabadiliko ya kweli ndani ya nchi.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment