Monday, December 3, 2012

Rufaa ya Lema kunguruma leo

*Anaiomba Mahakama imrudishie ubunge
*Adai alivuliwa ubunge kwa maneno ya uvumi 
RUFAA namba 47 ya mwaka 2012 iliyokatwa na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), akipinga kuvuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, inatarajia kusikilizwa leo Mahakama ya Rufaa, jijini Dar es Salaam.

Rufaa hiyo itasikilizwa leo mbele ya jopo la majaji watatu, Salum Massati, Nathalia Kimaro na Benard Luanda wa Mahakama ya Rufaa Tanzania.

Walalamikaji katika kesi ya msingi iliyomvua ubunge Lema ni wanachama watatu wa CCM, Mussa Mkanga, Agness Mollel na Happy Kivuyo, ambao kupitia mawakili wao Alute Mughwai na Modest Akida, walifungua kesi hiyo ya uchaguzi na kushinda.

Katika hoja zao, walidai wakati wa kampeni, Lema alimdhalilisha mgombea wa CCM, Dk. Batilda Burian, kwa kutumia lugha za matusi. Dk. Burian kwa sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya.

Lema kupitia wakili wake, Method Kimomogoro, aliwasilisha hoja 18 za kupinga kutenguliwa kwa ubunge wake na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha Aprili 5, mwaka huu.

Miongoni mwa hoja hizo, Lema aliiomba Mahakama ya Rufaa kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu wa kumvua ubunge, huku akiitaka imtangaze kuwa mbunge halali wa Jimbo la Arusha Mjini.

Aliitaka mahakama hiyo ya juu, iwaamuru walalamikiwa katika rufaa hiyo, walipe gharama za rufaa pamoja na zile za kesi iliyomalizika katika Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha.

Katika madai mengine, Lema anamlalamikia Jaji Gabriel Rwakibarila aliyesikiliza kesi hiyo, kwamba alitoa uamuzi wake kwa kuzingatia maneno ya uvumi, huku akipuuza ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.

Rufaa hiyo imefikia hatua ya kusikilizwa baada ya Lema kutimiza amri iliyotolewa na Mahakama ya Rufaa   Novemba 8, mwaka huu ikimtaka afanye marekebisho ya dosari za kisheria katika muhtasari wa hukumu ndani ya siku 14, kutokana na pingamizi lililowekwa na wajibu rufaa.

Lema alifanya marekebisho hayo na kuwasilisha upya rufaa yake ambayo leo inasikilizwa.


Mtanzania

No comments:

Post a Comment