Monday, December 3, 2012

Lema kumchakaza Waziri Wassira


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeanza Operesheni Chakaza Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Bunda, kwa lengo la kumthibitishia mbunge wa jimbo hilo, Stephen Wassira kuwa hana ubavu wa kudhibiti kasi ya kuenea kwa chama hicho kama anavyojigamba.
Operesheni hiyo inakuja zikiwa ni siku chache tangu Wassira ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), kuwaomba wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM wamchague kuwa mjumbe wa NEC ili aweze kudhibiti kasi ya kuenea kwa CHADEMA.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Godbless Lema, ndiye ataongoza operesheni hiyo itakayoanza Desemba 12 kwa kutumia usafiri wa helikopti na magari ili kuhakikisha wanafika maeneo yote ya wilaya hiyo ndani ya siku sita.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Lema ambaye anasubiria uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kuona kama atarejeshewa ubunge wake wa Arusha Mjini, alisema kuwa amekuwa akishangazwa na kauli za majigambo zinazotolewa na Wassira, ikiwemo ile ya Dodoma ya kudai yeye ana mwarobaini wa CHADEMA jambo alilosema hana ubavu huo.
Alisema kuwa ili kumdhihirishia kwa vitendo Wassira na CCM kuwa hawana ubavu wa kuzuia mabadiliko yanayoendeshwa na CHADEMA kwenye maeneo mbalimbali nchini, wameamua kuweka kambi kwenye jimbo lake na kuhakikisha wanawavua magamba na kuwavika magwanda wapiga kura wake.
Lema aliongeza kuwa, mbali ya kuendesha mikutano ya hadhara watakuwa na jukumu la kukagua uhai wa chama kuanzia kwenye msingi na matawi, kwa kuhakikisha wanasimika uongozi pale itakapoonekana kuna ulazima wa kufanya hivyo.
Katika oparesheni hiyo, Lema ataongozana na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, mjumbe wa mkutano mkuu wa CHADEMA, Lucas Webiro na aliyekuwa diwani wa Sombetini kupitia CCM, Alphonce Mawazo.

No comments:

Post a Comment