Saturday, December 15, 2012

Kiongozi CCM ahamia CHADEMA

WIMBI la viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kukihama chama hicho limezidi kushika kasi baada ya kada maarufu kutoka Wilaya ya Rufiji, Seleman Ndumbogani kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Ndubogani ambaye amewahi kushika nafasi mbalimbali ikiwemo ya kuwa mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, alisema kuwa ameamua kuihama CCM kutokana na sera zake zisizotekelezeka pamoja na uongozi wa wilaya kuwa wa kifamilia.
Kada huyo amedai kuwa wilaya hiyo imejaa siasa chafu ambazo zimetengeneza makundi mawili katika baraza la madiwani hali inayosababisha kuwapo kwa ugomvi wa mara kwa mara katika halmashauri.
Ndubogani alidai kuwa mbunge wa Rufiji, Abdul Malobwa, ni mkwe wa mwenyekiti wa sasa wa Halmashauri ya Rufiji, Ramadhan Ngayonga, huku Katibu Mwenezi wa CCM wa wilaya hiyo, Musa Mng’eresa akiwa ni mpwa wake.
Pia alidai kuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya, Bakari Msati, ni mjomba wa mwenyekiti wa halmashauri kwamba kwa pamoja wanatokea eneo moja ya Delta.
Mbali na madai hayo, Ndubogani pia alidai kutotekelezeka ipasavyo kwa sera za CCM nako kumechangia achoke na kuhamia CHADEMA.
“Sera za CCM ni kutoa ajira nyingi serikalini na ndani ya chama kila mwaka, lakini mimi, wenzangu na watoto wetu tumeomba kazi zaidi ya miaka 20 bila mafanikio … sasa tunaing’ang’ania CCM ya nini?” alidai.
Ndumbogani aliongeza kuwa amehamia CHADEMA ili kuimarisha chama hicho kuanzia ngazi ya msingi hadi wilaya huku akiwataka wanaomfahamu wasihuzunishwe na kuhama kwake kwa kuwa CCM imepoteza dira na waje CHADEMA.
Ndumbogani alirejesha kadi ya CCM na kukabidhiwa ya CHADEMA na mbunge wa Ubungo, John Mnyika, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Maili Moja, Kibaha mkoani Pwani juzi.

No comments:

Post a Comment