DK. SLAA ADAI JK ANAMLINDA IGP MWEMA
HOJA nzito zinazoendelea kuibuliwa na viongozi waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuhusu utendaji wa Rais Jakaya Kikwete, zinaonekana kuwa mwiba na kuikoroga serikali yake.
Wakati hoja ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, ya uteuzi wa baadhi ya majaji wasio na sifa ikiwa bado haijapatiwa majibu ya kuridhisha, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, naye amepigilia msumari mwingine akisema Rais Kikwete anamlinda Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Mwema.
Dk. Slaa aliibua hoja hiyo wakati akizungumzia mauaji mbalimbali yanayodaiwa kufanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya raia wema, akisema hali hiyo ni matokeo ya IGP Mwema, kulindwa na mkuu wake, na hivyo kushindwa kuwachukulia hatua wahusika.
Wakati hoja hizo zikiibuliwa, wasaidizi waandamizi wa Rais Kikwete wakiwemo mawaziri na watendaji wengine, wameonekana kupwaya, wakishindwa kuhimili mikiki ya kutoa majibu yenye kufafanua kile kinachohojiwa.
Akizungumza jana jijiji Dar es Salaam, wakati akifungua mkutano mkuu wa chama hicho Jimbo la Kinondoni, Dk. Slaa alisema kama IGP Mwema anashindwa kuchukua hatua juu ya matatizo yanayojitokeza, ikiwamo mauaji na kujeruhi wanayofanyiwa wananchi na polisi, rais anapaswa kuchukua hatua kwa lengo la kuiokoa nchi.
Huku akirejea matukio kadhaa ya mauaji na mateso mbalimbali yaliyofanyika katika mikoa ya Tabora, Morogoro, Iringa, Arusha, Mara, Mwanza, Mbeya, Dar es Salaam na maeneo mengine, Dk. Slaa alisema sheria zipo wazi juu ya suala hilo katika kuunda tume ya kimahakama katika kupata ukweli wa madhila hayo.
“Nyote mnajua kuwa haki katika nchi yetu imekuwa bidhaa adimu, matukio ya kutisha yanajitokeza kila siku, viongozi wenye dhamana na maisha yetu wanakaa kimya, katika hili kama rais hajui sheria si ana watu wanaomsaidia, hivi haoni hata haja ya kuunda tume huru ya kimahakama?” alihoji.
Alisema kuwa kutokana na ukimya wa rais, ikiwa ni pamoja na kushindwa kuwachukulia hatua Waziri wa Mambo ya Ndani, IGP Mwema, makamanda wa polisi wa mikoa ya Iringa na Morogoro, CHADEMA watakutana kabla ya Krismasi na kutoa msimamo wa nini kifanyike kutetea haki ya wananchi.
Dk. Slaa alisema madhumuni ya CHADEMA ni kukuza, kulinda na kutetea haki za binadamu, hivyo wanapaswa kuhakikisha wanafuatilia ukandamizaji wa watu katika misingi ya rangi jinsia, ukanda, rika na itikadi, jambo alilodai limewashinda CCM.
“CCM leo kila wanaposimama wanaomba waendelee kuungwa mkono ili watawale…wameacha yale yaliyo katika katiba ya nchi na kusahau maandiko yaliyo nyuma ya ilani ya chama,” alisema.
Chikawe amgwaya Lissu
Wakati Dk. Slaa akiibua tuhuma nzito kwa Serikali ya Rais Kikwete, zenye kuhitaji majibu stahili, Waziri wake wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, ameshindwa kutolea ufafanuzi hoja zilizoibuliwa na Lissu kuhusu baadhi ya majaji, aliodai waliteuliwa bila kufuata utaratibu.
Chikawe ambaye kimsingi ni miongoni mwa wasaidizi wa Rais Kikwete, anayepaswa kuitetea serikali yake, alipoulizwa juu ya hoja hiyo aliishia kusema, “hoja za Waziri Kivuli wa Sheria na Katiba, Tundu Lissu nimezisikia, nimezisoma na sina maoni yoyote juu ya hilo.”
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Waziri Chikawe alisema: “Ungekuja ofisini, nipo safari kwa sasa, hata hivyo hoja za Lissu nimeziona, nimezisoma na sina ‘comment’ kwa sasa.”
Ni waziri huyo huyo, ambaye aliliambia Bunge kuwa Tume ya Mahakama inamshauri rais wakati wote na kwamba hakuna ukiukwaji wowote uliofanyika katika uteuzi wa majaji.
Alisema haijatokea hata siku moja rais akamteua jaji wa Mahakama Kuu bila kuzingatia mapendekezo ya Tume ya Uajiri ya Mahakama.
Awali akijibu hoja za Lissu bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, ambaye jana simu yake iliita bila majibu, alimuonya Lissu kuwa ataburuzwa kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge kwa ‘taarifa potofu anazoziwasilisha bungeni’.
Lakini mapema wiki hii, Lissu alirejea hoja yake na kusisitiza kuwa alishatoa maelezo hayo hata katika Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Brigedia mstaafu Hassan Ngwilizi.
“Nilieleza jinsi rais alivyofanya uteuzi wa baadhi ya majaji pasipokupata ushauri wa Tume ya Utumishi wa Mahakama. Wamekuwa wakijibu kiujumla, mimi niliwataja kwa majina yao na hata hili nilieleza katika Kamati ya Ngwilizi ambayo taarifa yake haikuwekwa hadharani pasipo sababu za kueleweka,” alisema.
Alipotafutwa jana, Lissu ambaye pia ni mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni, alisema kuwa kwa sasa serikali haiwezi kusema chochote zaidi ya kukubali, kwani tayari ameshawapa ushahidi kwenye Kamati ya Bunge.
Alisema hoja yake kuwa kuna ukiukwaji wa katiba inaungwa mkono na nyaraka za ndani ya serikali na hasa Ofisi ya Rais, Ikulu yenyewe, ambayo Desemba 6, 2007, mkutano kuhusu ajira ya majaji waliostaafu ulifanyika Ikulu chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu Kiongozi wakati huo, Philemon Luhanjo.
Lissu aliongeza kuwa, wajumbe wengine walikuwa pamoja na Mwanasheria Mkuu, Johnson Mwanyika na Naibu wake, Sazi Salula, Katibu Mkuu Utumishi George Yambesi, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Sophia Wambura na Susan Mlawi wa Sekretarieti ya Baraza la Mawazi.
“Serikali iseme suala hili ni la kweli au si la kweli, na wale niliowataja kuwa hawana sifa kwa mfano ya elimu serikali iseme wamesoma wapi, na kwanini kulikuwa na kikosi kazi kwa ajili ya majaji wanaoajiriwa kwa mkataba ikiwa mimi sijasema kweli,” alisema.
Alisema kuwa anazidi kuuliza inawezekanaje jaji asome shahada ya kwanza ya Sheria Chuo Kikuu Huria sasa, kwamba aliteuliwaje kuwa jaji, maana hiyo ndio sifa ya msingi?
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment