Sunday, November 4, 2012

Zitto `alilia` umri wa kugombea urais


Nia ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, kuwania urais mwaka 2015, imezidi kujionesha, baada ya kupendekeza umri wa mgombea nafasi hiyo kuwa miaka 35.
Zitto ametoa rai hiyo wakati akichangia maoni kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipokutana na wabunge mjini hapa jana.
Mbunge huyo ambaye hadi kufikia mwaka 2015 atakuwa na miaka 38, ameshatangaza nia ya kuwania urais ingawa suala la umri linaonekana kuwa kikwazo kwake, kwa mujibu wa Katiba.
Akichangia maoni yake jana, alisema umri wa mtu kuruhusiwa kugombea urais uanzie miaka 35 kama ilivyo katika nchi nyingine.
Alitoa mfano wa nchi za Rwanda, Burundi, Afrika Kusini, Kenya, Uganda, Marekani ambapo umri uliowekwa katika katiba zao ni kuanzia miaka hiyo.
Aidha, alipendekeza muda wa rais kukaa madarakani uwe kipindi kimoja cha miaka saba na akimaliza asiruhusiwe kugombea tena.
Wengine waliopendekeza umri wa miaka 35 ni pamoja na Mbunge wa Tarime Chacha Nyangwine, Hamis Kigwangala na Ali Kessi.
Walisema umri huo ndio unaotumika na nchi nyingi duniani na hata kuwekwa kwenye katiba za nchi zao.
MAONI TOFAUTI
Suala kuwepo kwa kipindi maalumu cha Rais kuwepo madarakani, umri wa kugombea urais, vyombo vya habari kuwa mhimili wa nne na serikali tatu, miongoni mwa masuala yaliyoibuka katika michango ya wabunge.
Aidha, haki ya mgombea binafsi na mawaziri wasitokane na wabunge na uraia wa nchi mbili ni mambo yaliyotawala katika michango hiyo.
Tume hiyo inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, ilianza kazi hiyo tangu Julai mwaka huu kwa kukusanya maoni ya mtu mmoja mmoja, baadaye itaingia kwenye awamu ya pili ya kukusanya maoni ya vikundi.
Kuhusu kipindi cha mtu kukaa bungeni, Kessi alipendekeza awe na awamu mbili na viongozi wastaafu wasiruhusiwe kuchukua fomu za ubunge . “Haiwezekani wastaafu waje bungeni kusinzia,” alisema.
Alitaka ukubwa wa baraza la mawaziri upunguzwe na ubaki na mawaziri 14 na manaibu 14.
Aidha, alisema majimbo yapunguzwe kwa kuwa yamekuwa mzigo kwa taifa na kutoa mfano wa Pemba na Unguja ambako kuna wabunge zaidi ya 60 na kutaka majimbo yapimwe kwa ukubwa.
Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), alipendekeza suala la Viti Maalum lifutwe na mtu aingie kwenye ushindani na kuchaguliwa kwa uwezo wake.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Diana Chilolo (Viti Maalum) aliyesema kuwa wabunge wa Viti Maalumu wanadharauliwa hata wageni wanapokwenda kwenye wilaya zao wanasahauliwa kutambulishwa.
Suala la Muungano na kuwepo kwa serikali tatu lilionyesha kuchukua maoni ya wabunge wengi ambapo walipendekeza kuwe na Serikali ya Muungano, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar.
Hoja hiyo ilichangiwa pia na Musa Haji Komba, Mariam Msabaha, Ester Bulaya, Mohamed Mnyaa, Zitto Kabwe, ambapo baadhi walipendekeza kuwepo kwa muungano wa mkataba ili kuangalia masuala waliyokubaliana kwenye muungano kama yanatakelezeka.
Kombo alisema muungano wa sasa ni muungano wa sehemu moja kutawala upande mwingine wa muungano na kutaka katika iangalie katika suala hilo. Aidha, Zitto alipendekeza kuwe na nchi moja, dola moja na serikali tatu.
Suala la mbunge wa baraza la wawakilishi kuingia kwenye Bunge la Muungano na wa Bunge la Muungano kutoingia kwenye Baraza la Wawakilishi lilitakiwa liangaliwe ili kutoa haki kwa pande zote mbili za muungano.
Hamad Rashid, alipendekeza katiba mpya ieleze mawaziri wanaoteuliwa nje ya Bunge wathibitishwe bungeni badala ya ilivyo sasa kwa kuteuliwa na Rais.
Aidha, alisema katiba ya sasa iweke wazi kuwepo kwa mahakama ya katiba ili kuepuka uvunjwaji unaoweza kutokea.
Cesilia Pareso (Viti Maalum-Chadema), alisema katiba ya sasa iweke mhimili wa nne wa vyombo vya habari ambao utakuwa na jukumu la kukosoa mihimili mingine ambayo ni Serikali, Mahakama na Bunge.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliwasifu wabunge kwa kujitokeza kwa wingi kuchangia maoni hayo na kueleza umuhimu wa Katiba kuwa ni uhai wananchi. “Mmeonyesha hali ya uwajibikaji mbele ya umma,” alisema.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment