CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeitaka serikali kuchukua hatua za haraka za kuwatafutia makazi wakazi zaidi ya 2,500 wa Kata ya Hananasif, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam waliobomolewa nyumba zao.
Wakazi hao walibomolewa nyumba zao mwanzoni mwa mwezi Oktoba na askari wa Manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa maelezo kwamba hawatakiwi kuishi maeneo hayo.
Akizungumza jijini jana Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Kinondoni na Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Henry Kilewo, alisema mwezi sasa umepita bila ya serikali kuchukua hatua, hivyo ni vyema ikawahudumia wahathirika hao haraka ili waache kuteseka.
Kilewo alisema kutokana na jambo hilo kuwa zito, aliviomba vyombo vingine vya utetezi kwa wananchi kuungana na CHADEMA ili kupigania haki ya wahathirika hao ambao alidai wameonewa.
“Napenda kuikumbusha Serikali ya CCM wajibu wa maisha bora kwa Mtanzania siyo manyanyaso ya kuwaonea wanyonge bali iwatafutie ufumbuzi wa haraka wahathirika hawa,” alisema.
Katibu huyo aliitaka serikali iache tabia ya kutumia ubabe kwa kuwaharibia makazi yao pasipo kuwatafutia mengine huku ikijua kuwa wao ndio wenye serikali hii.
Alisema wakazi hao hawakustahili adhabu hiyo ya kifedheha yenye kudhalilisha utu wao pamoja na uraia walionao, na kwamba wanaendelea kulilaani zoezi hilo ambalo liliendeshwa kidhalilishaji.
“Tunarudia kuwapa pole wahathirika wote waliokumbwa na bomoa bomoa hiyo…tunailaani Serikali ya CCM kwa kuwa imesababisha Watanzania sasa wanaishi kama wakimbizi na kama watumwa ilihali wapo kwenye taifa lao,” alisema Kilewo.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment