MAHAKAMA YATUPA PINGAMIZI ZA CCM
MAHAKAMA ya Rufaa Tanzania, imekataa kuifuta rufaa iliyofunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema (CHADEMA) kwa maelezo kuwa upungufu uliyopo kwenye nakala ya hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, iliyotengua ubunge wake, hauwezi kuwa sababu.
Lema alikata rufaa mahakamani hapo, akipinga hukumu iliyotolewa Aprili 5 mwaka huu, na Jaji Gabriel Rwakibarila wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Uamuzi huo mdogo ulitolewa jana katika Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam na Naibu Msajili wa mahakama hiyo, Zahara Maruma, huku mamia ya wafuasi wa Lema wakiwa wamefurika kujua hatima yake.
Maruma alisoma uamuzi huo kwa niaba ya jopo la majaji wanaosikiliza rufaa hiyo, Natalia Kimaro, Salum Massati wakiongozwa na Jaji Mkuu Othman Chande.
Uamuzi huo unaotokana na pingamizi la awali lilowasilishwa na wajibu rufaa ambao ni wananchama wa CCM wa la Arusha Mjini wanaotetewa na Medest Akida na Alute Mughwai, dhidi ya Lema na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Arusha mjini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali anayewakilishwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali Timon Vitalis.
Lema katika rufaa hiyo anawakilishwa na Method Kimomogoro na Tundu Lissu ambao jana hawakuwepo mahakamani, ambapo wakili Edson Mbogoro aliwawakilisha.
Jaji Chande alisema hivi karibuni wajibu rufaa waliwasilisha pingamizi la awali ambapo waliwasilisha hoja tatu, akiiomba mahakama hiyo iifute rufaa hiyo wakidai kuwa kikaza hukumu kilichotumiwa na Lema kukata rufaa kilikuwa hakina mhuri wa mahakama wala haionyeshi hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha iliyotengua ubunge wake ilitolewa lini.
Kwamba walidai kuwa kikaza hukumu hakikuzingatia kanuni za Masijala za Mahakama Kuu ya mwaka 2005 na kwamba kikaza hukumu hicho kilikuwa kimekosekana maneno kama ‘hukumu hii imetolewa kwa mkono wangu’.
“Jopo langu limepitia hoja za pande mbili limefikia uamuzi wa kukubaliana na hoja ya kwanza kuwa ni kweli kikaza hukumu kilichotumiwa na Lema kukata rufaa kilikuwa na dosari hizo za kutokuwa na mhuri wa tarehe, na tatizo hilo halikusababishwa na Lema ni watendaji wa mahakama waliyoaanda kikakaza hukumu hiyo.
“Kwa sababu hiyo, mahakama hii imekataa ombi la wajibu rufaa lililotaka mahakama hii ifute rufaa iliyokatwa na Lema kwa sababu eti kikataa rufaa hicho kilikuwa na upungu huo, licha ya kwamba ni kweli mahakama hii inakiri kuwepo kwa upungufu huo lakini hauwezi kufanya mahakama hii iifute rufaa ya Lema,” alisema.
Alisema mahakama hiyo imempatia Lema muda wa siku 14 kuanzia jana awasilishe upya rufaa yake ambayo atakuwa ameifanyia marekebisho yatakayoonesha mhuri na tarehe ya kutolewa kwa hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Aidha, Jaji Chande alisema jopo lake limetupilia mbali hoja mbili za wajibu makada wa CCM, zilizodai kikaza hukumu hakikuzingatia kanuni za masijala ya Mahakama Kuu ya mwaka 2005 na kwamba kilikosa maneno; ‘hukumu imetolewa kwa mkono wangu,’ akisema hoja hizo hazina mantiki kisheria.
Uamuzi huu ni wa pingamizi la awali na hausiani na rufaa iliyokatwa na Lema mahakamani hapo kwani rufaa hiyo bado haijaanza kusikilizwa.
Oktoba 2 mwaka huu, pingamizi hilo la awali lilianza kusikilizwa mjini Arusha ambapo wakili Kimomogoro alidai kuwa Jaji Gabriel Rwakibarila wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, aliyetoa hukumu ya Lema, jalada la kesi hiyo lilihamishiwa Dar es Salaam, hivyo hakukuwa na muda wa kupitia hukumu na hati ya kukazia hukumu.
“Waheshimiwa majaji wa Mahakama ya Rufaa, wakili mwenzetu, Mughwai, ametueleza hapa aliomba mara mbili tofauti apewe tuzo hiyo ikiwa imesahihishwa, lakini hakupatiwa majibu, katika mazingira hayo alitegemea sisi tungeipata vipi?” alihoji.
Baada ya uamuzi huo kutolewa jana, Lema alizungumza na wafuasi wake nje ya mahakama hiyo, akisema anawashukuru wana-CHADEMA wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kumfariji.
Alisema kuwa alikuja akawa na wasiwasi mkubwa na uamuzi huo wa mahakama ya rufaa kwani kesi iliaribiwa, kwamba alikuwa akisita kuja kuupokea uamuzi huo kwa sababu hivi sasa mahakama imekuwa na sifa mbaya.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment