Saturday, November 10, 2012

Jaji Werema `agonga mwamba` kwa Zitto


 Mkakati wa kuifuta hoja ya Zitto wakwama
 Serikali yaagizwa kuwasilisha uchunguzi Bunge la 11

Mkakati wa kuifuta hoja binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto, kuitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania walioficha fedha nje ya nchi, umeshindwa.
Hatua ya kuikwamisha hoja hiyo, ilionekana kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema na ‘kupigiwa chapuo’ na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Jaji Werema, akijibu hoja ya Zitto, alipendekeza mambo kadhaa ambayo kimsingi, baadhi ya wabunge waliyashtukia na kusema kama yakipitishwa, hoja hiyo itakuwa imefutwa.
Kabla ya wabunge waliokuwa wakiunga mkono hoja hiyo kumshtukia, Jaji Werema alipendekeza kuifanyia marekesho ya kuitaka serikali iwasiliane na Benki ya Dunia ili kupitia kitengo cha assets recovery, mabilioni ya fedha yarejeshwe.
Fedha hizo ni zinazomilikiwa na Watanzania katika benki za nchini Switzerland na maeneo mengine ambapo zinafichwa, ili kukwepa kodi.
Jaji Werema alitaka pendekezo hilo liondolewa kwa maelezo kuwa mamlaka za uchunguzi zinalifanyia kazi.
Kuhusu azimio la kuwapiga marufuku viongozi wa serikali, watoto wao na Watanzania wengine kufungua akaunti nje, Werema alisema suala hilo linashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Kigeni.
Aliongeza kuwa suala hilo linashughulikiwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na kitengo cha fedha cha inteligensia, hivyo akataka azimio hilo liondolewe.
Pia alisema azimio la kutaja akaunti za watu wenye fedha benki za nje ni gumu na linakwenda kinyume na sheria za benki zinazotaka kutunza siri za wateja wao.
Alisema pendekezo la kuitaka serikali katika bajeti ya mwaka 2013/14 kuanzisha kodi maalum, ‘financial transaction tax’ ya angalau asilimia 0.5 yake, thamani ya ‘transaction’ ili kuweza kuwa na rekodi za uhakika fedha ndani na zinazotoka nje linahitaji utafiti ufanywe na serikali.
Jaji Werema alisema ofisi yake imechukua hatua za kutosha ikiwemo kwenda Uswisi na kwingineko na itashirikiana na vyombo binafsi vya uchunguzi kufanya uchunguzi huo.
Baada ya Jaji Werema kutoa mapendekezo katika hoja ya Zitto, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alisema kimsingi mapendekezo hayo yana lengo la kuua hoja ya Zitto.
“Hoja ya mabadiliko ya Jaji Werema kuondoa mapendekezo hayo, kwa maoni yangu yanakinzana na kifungu 53 (3) (4) cha kanuni za Bunge, kinachopendekeza kuwepo kwa mabadiliko na sio kufuta hoja.
“AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) hana mamlaka ya kufuta hoja na hapa tumeona hataki kufanya mabadiliko kwenye hoja isipokuwa anasema futa hii, futa hii…kibaya zaidi ni pale anapotaka hii hoja iondolewe na hana mamlaka isipokuwa mtoa hoja.
“Naomba Spika utumie busara ya meza yako umwelekeze AG kwamba hana uwezo huo,” alisema.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, aliunga mkono mapendekezo ya Jaji Werema huku akijaribu kuzipiga chini hoja za Lissu.
Hata hivyo, aliunga mkono pendekezo la serikali kuwasilisha bungeni hapo ripoti ya uchunguzi katika Bunge la 11 na kwamba ili kasi hiyo iende vizuri washirikishwe pia kampuni binafsi za uchunguzi.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), alisema mapendekezo ya Jaji Werema yakibaki kama yalivyo hoja ya Zitto itakosa sifa.
“Tusifanye dhambi ya kuiondoa hoja hii, ni hoja ya msingi sana na ninapenda ili watu wapete ujasiri wataje majina…ukiwataja hawa hoja yako itakuwa na mashiko, tusaidiane na wala sio fedheha kuwataja,” alisema.
Zitto kwa upande wake alisema, “ukitazama vizuri mapendekezo ya Jaji Werema anataka kuiondoa hoja hii na hii sio sahihi kwake hata kidogo.”
Mbunge wa Kisesa, Luaga Mpina (CCM), alisema hakubaliani na pendekezo la kuiondoa hoja hiyo na akaunga mkono azimio.
Azimio hilo liiagize serikali kufanya uchunguzi huo na kwamba ripoti yake iwasilishwe bungeni hapo katika Bunge la 11 na kama itashindwa basi Bunge liunde kamati ndogo ya kufanya uchunguzi huo.
Suala hilo liliungwa mkono na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (TAMISEMI), Hawa Ghasia, alisema lichukuliwe na serikali na katika Bunge la 11, serikali itoe ripoti na kama itashindwa basi Bunge linaweza kuchukua hatua zingine muafaka.
Akihitimisha mjadala huo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema hoja ya Zitto sio kwamba imetupwa isipokuwa inaingia kwenye utaratibu wa serikali wa kuyatekeleza maazimio hayo.
Alisema serikali itapaswa kutoa taarifa ya utekelezaji wa hoja ya Zitto katika Bunge la 11, (Aprili) mwakani na kama ikishindwa na wabunge kutoridhika basi wataunda kamati ndogo kwa ajili ya kufanyia uchunguzi maazimio hayo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment