Thursday, November 15, 2012

Dk. Slaa: Tutamjibu JK


 ASEMA CCM YA SASA HAIWATISHI
SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kuwataka makada wa chama hicho kujibu mapigo ya wapinzani, akidai wanafanya kazi ya kueneza uongo na kupotosha wananchi, CHADEMA imesema inamvutia pumzi kabla ya kumjibu.
Akihitimisha mkutano mkuu wa CCM mjini Dodoma juzi usiku, Rais Kikwete aliwataka mawaziri na makada wa chama hicho kufanya mikutano ya hadhara na kutumia vyombo vya habari kujibu hoja za wapinzani badala ya kutegemea nguvu za Jeshi la Polisi.
Huku akionekana kukasirishwa na kasi ya CHADEMA, Rais Kikwete alimtaja wazi wazi Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, kuwa aliwahi kumzulia uongo pamoja na mwanaye Ridhiwani.
“Slaa aliita mkutano akasema mimi, mwanangu Ridhiwani na Rostam Aziz tulikutana kwenye hoteli moja jijini Mwanza, huku akijua siku aliyoitaja mi nilikuwa kusini nikiendelea na shughuli zangu,” alisema.
Rais Kikwete alisisitiza kuwa hiyo ndiyo kazi ya upinzani, watu wazima hovyo, wanasema uongo mbele wananchi na hata wakati mwingine kwenye vyombo vya habari wakinukuu takwimu za uzushi.
Alipoulizwa jana na gazeti hili kuhusu madai hayo ya kueneza uongo kwa wananchi, Dk. Slaa alicheka kisha akasema: “Tunawatafakari na tutawajibu, ila siyo leo, wala hatuna haraka.
“Mimi kwa kweli sikusikiliza hotuba yake, na hata mkutano wa CCM sijaufuatilia, ila kama Kikwete kasema hayo unayoniuliza, basi tutamjibu kwa utaratibu rasmi wa chama, leo sisemi kitu.
“Sisi ni watu makini, tunaamini katika kile tunachokisema wala wasipaniki, tutawajibu. Maana wanadhani tunapoteza muda kufuatilia mkutano wao, nilimsikia hata Nape Nnauye akisema juzi kuwa anajua tumeacha kazi tunawakodolea macho,” alisema.
Dk. Slaa alisema kauli ya Nape ambaye pia ni Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi wa CCM, inachekesha, kwani CCM ya wao kuacha kazi zao na kuikodolea macho ilikuwa ya zamani si hii ya leo.
Katika kile kinachoonekana kama CHADEMA kuinyima usingizi serikali na CCM, Kikwete aliagiza mawaziri wote kujiwekea utaratibu wa kila mmoja kutoa taarifa za utekelezaji wa majukumu ya serikali katika vyombo vyote vya habari.
Alisema kwa vile viongozi wa chama na serikali hawajibu taarifa za upotoshaji zinazotolewa na wapinzani, wananchi wanapozisikia zikirudiwa rudiwa bila kukanushwa wanaziamini.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment