Monday, November 12, 2012

Chadema kusambaza pikipiki nchi nzima


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza mkakati wa Uchaguzi Mkuu 2015 kikiahidi kumwaga pikipiki katika tarafa zote nchini kwa ajili ya kuwafikia wananchi kuelekea uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema hayo jana katika kikao cha viongozi wa chama hicho na wadau wake kilichofanyika hapa.
Mbowe alisema pikipiki hizo zitakuwa na vipaza sauti maalumu zitawasaidia viongozi wa chama hicho kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
“Tumeanza mkakati wa kuhakikisha tunawafikia wananchi kila mahali. Tunataka kusikiliza matatizo yao, na hata pale ambako kuna shida ya usafiri, kwa pikipiki tutafika,” alisema.
Tayari chama hicho kimezindua kampeni yake ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), ambayo lengo lake ni kuwaandaa wananchi kwa uchaguzi ujao.
Mbowe alisema upatikanaji wa pikipiki hizo unatokana na fedha za ruzuku ambazo zinatolewa na Serikali kwa chama hicho  pia marafiki na wanachama wake walioko nje ya nchi.
Aliwataka viongozi wa chama hicho katika ngazi zote kufanya kazi kwa kujituma ili kuhakikisha kinashika dola mwaka 2015.
“Tanzania inahitaji mabadiliko na sisi tukiwa viongozi tunapaswa kujipanga kwanza, kuhakikisha tunaongeza wanachama pia kuzitatua kero za wananchi,” alisema Mbowe.
Katika mkutano huo, Mbowe aliwapongeza viongozi wa Chadema, Wilaya ya Hanang’ kwa kazi kubwa waliyoifanya kiasi cha kupata na madiwani 17 katika halmashauri hiyo.
Awali, Mbunge wa Viti Maalumu, Mkoa wa Manyara, Rose Kamili alisema chama hicho kimejipanga kutwaa Jimbo la Hanang’ katika uchaguzi ujao na Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’.
“Katika miaka hii mitano Chadema, Hanang’ tumekuwa na mafanikio makubwa na hili linatokana na mshikamano mkubwa wa viongozi katika ngazi mbalimbali,” alisema.
Mwananchi

No comments:

Post a Comment