Saturday, October 6, 2012

Wauaji wa Kada wa CHADEMA watoroka

POLISI WAHAHA KUFICHA UKWELI, WATOA DAU LA MIL. 5/-
WASHTAKIWA wawili waliompora askari polisi bunduki wakiwa chini ya ulinzi katika mahakama ya mkoa wa Arusha na kutoroka kusikojulikana, katika mazingira ya kutatanisha imebainika kuwa ni wale wanaokabiliwa na tuhuma ya mauaji ya aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo.
Washtakiwa hao Samweli Mtinange maarufu kama Samu na Mohamed Shaban Limu walitoroka juzi majira ya saa 7:30 mchana wakati wakitolewa kwenye chumba cha mahabusu mahakamani wakipelekwa kwenye karandinga la polisi kwa ajili kurudishwa rumande kwenye gereza la mkoa, Kisongo.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas, alithibitisha kutoroka kwa washtakiwa hao wanaokabiliwa na kesi hiyo ya mauaji namba 184/2012, lakini akakanusha kuporwa bunduki na silaha zaidi ya 30 kwa askari polisi aliyekuwa akiwalinda.
Tukio hilo limezua hofu kubwa na kuzusha tuhuma kuwa limepangwa kiufundi na baadhi ya watu, kwa nia mahsusi za kisiasa hasa ikizingatiwa kutokea kwa tukio jingine baya la mauaji ya mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, mkoani Iringa mwanzoni mwa mwezi uliopita.
Wasiwasi huo umekuja kutokana na mazingira ya tukio hilo, ambalo wadadisi wa mambo wanatia shaka juu ya kutokuwepo kwa mikakati imara iliyosukwa kufanikisha utorokaji huo.
Kurugenzi ya Ulinzi na Usalama ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imedai kupokea kwa mshtuko na tahadhari kubwa, kitendo cha watuhumiwa wawili wa mauaji hayo, kutoroka mbele ya askari polisi wenye silaha, baada ya kumnyang’anya bunduki mmoja wa askari waliokuwa lindo kwenye eneo la mahakama ya wilaya.
Aidha kurugenzi pia imepokea kwa tahadhari kubwa taarifa kuwa Kamanda wa Polisi (RPC), mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, pamoja na kukiri kuwa waliokimbia mbele ya polisi kwa kumnyang’anya askari silaha ni watuhumiwa wa mauaji ya Mbwambo, aligoma kutaja jina la askari aliyenyang’anywa bunduki na hata majina ya wenzake waliokuwa lindo hapo mahakamani.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Rwakatale, alisema tukio hilo sasa limekifanya chama hicho kianze kuweka mkazo kwenye kuunganisha ‘nukta’ katika matukio ya namna hii na limezidi kudhihirisha pasi na shaka yoyote umuhimu wa kuundwa kwa chombo huru cha uchunguzi wa mauaji yenye utata, yanayohusishwa na siasa, mojawapo likiwa ni tukio la mauaji ya Mbwambo.
Rwakatale amelitaka Jeshi la Polisi kutoa maelezo ya kutosha yatakayoendana na uwajibikaji, unaopaswa kufuatiwa na hatua za kisheria, ili kuweza kujinasua kwenye kashfa hii ya juzi Arusha, ambapo sasa inatafsiriwa kuwa jeshi hilo limehusika kufanya ‘mchezo’ mwingine kwa nia ama ya kutaka kuficha mtandao wa mauaji hasa ya kisiasa au kuficha ushahidi muhimu wa masuala ambayo ama yamebainika kwenye mahojiano au ambayo yangebainika mahakamani, ikizingatiwa kuwa baadhi ya watuhumiwa wa kesi hiyo ni viongozi wa CCM.
“Kitendo cha RPC Sabas kukanusha askari wake kunyang’anywa bunduki, ambayo baadaye iliokotwa ikiwa imetelekezwa, ni dalili za mwendelezo wa tabia ya jeshi hilo, kupitia maofisa wake waandamizi, kujitokeza kuficha ukweli na kufanya propaganda, kwa kila tukio ambalo jeshi hilo linapaswa kuwajibika kwa makosa linayofanya”
“Itakumbukwa pia katika barua ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Mheshimiwa Freeman Mbowe kwenda kwa Rais, chama kilimtaka Rais kuunda Tume ya Kijaji/ Kimahakama ya uchunguzi wa vifo vilivyotokea katika mikusanyiko, mikutano, maandamano au mazingira ya kisiasa yaliyohusisha CHADEMA. Vifo hivi ni vile vilivyotokea Arusha (05/01/2011), Igunga (Novemba 2011), Arumeru Mashariki (Aprili 2012), Iramba (Julai 14, 2012), Morogoro (27/08/2012) na Iringa (02/09/2012),” imesema taarifa hiyo.
CHADEMA imesema kuendelea kutokea kwa masuala yenye utata katika usalama kumeonyesha kuwa serikali ya CCM inazidi kukomaza mfumo wa kulindana na kutaka kuficha masuala fulani fulani, hasa katika matendo ya mauaji yanayofanywa na Jeshi la Polisi, chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Hali ambayo inatia shaka ni hatma ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
“Hatuoni mantiki ya kigugumizi cha serikali ya CCM na viongozi wake, kushindwa kuzungumzia utendekaji wa haki na uwajibikaji kama moja ya misingi muhimu sana ya tunu ya amani.
Masuala haya yakitekelezwa inavyotakiwa, hata kazi ya ulinzi na usalama kwa raia na mali zao, itakuwa rahisi kwa sababu itakuwa ni wajibu wa jamii nzima. Kinyume na hapo, kwa kufumbia macho vitendo vya wazi vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwemo isiyoweza kuthaminishwa na kitu chochote, haki ya kuishi, inazidi kujipotezea uhalali wa kutawala.
CHADEMA imeendeleaa kusisitiza kutaka uwajibikaji wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi, IGP Saidi Mwema, Kamanda wa Operesheni Maalum wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, RPC wa Mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile na RPC wa mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, kutokana na mauaji yaliyotokea mkoani Morogoro na Iringa, kwa wao wenyewe kujiuzulu au kufukuzwa kazi na Rais ili kupisha uchunguzi huru.
“Wakati Kurugenzi ikisisitiza msimamo wa chama wa kuitaka serikali iwakamate na kuwafungulia kesi ya mauaji, Kamanda wa FFU Mkoa wa Morogoro (kwa mauaji ya Ally Zona) na RPC Kamuhanda na askari wote wanaoonekana kwenye picha wakimsulubu marehemu Daudi Mwangosi kabla hajalipuliwa kwa bomu la polisi na kufa, inapenda kusisitiza kuwa Jeshi la Polisi linawajibu wa kuhakikisha watuhumiwa wa mauaji ya Mbwambo waliotoroka, Samwel Mtinange na Mohamed Limu, wanapatikana huku hatua zinazostahili juu ya tukio hilo la utorokaji zikichukuliwa kwa wahusika wote,” wamesema.
Mbali na waliotoroka, washtakiwa wanaoendelea kushikiliwa kuhusiana na mauaji ya Mbwambo ambaye aliuawa kikatili kwa kukatwa kichwa na kitu chenye ncha kali shingoni kubaki wanne wakiwemo wenyeviti wa serikali za vitongoji wanaotokana na Chama cha Mapinduzi (CCM), Davis Mkumba (Kisambaramajengo) na Mathias Nathan (Magadini) ambapo washtakiwa wengine ni Saidi Florianna Swalihi na Yohana.
Aidha hatua ya Kamanda Sabas kukanusha taarifa kuwa watuhumiwa hao wakati wakitoroka walifanikiwa kumnyang’anya bunduki mmoja wa askari waliokuwa wakilinda, mashuhuda wa tukio hilo ambao hawakuwa tayari majina yao kutajwa magazetini walilieleza Tanzania Daima kuwa watuhumiwa hao walimnyang’anya silaha aina ya SMG mmoja wa askari polisi aliyekuwa akiwalinda jambo lililozua hofu kubwa miongoni mwa baadhi ya watumishi wa mahakamani ambao baadhi waliamua kujifungia ndani ya vyumba vya mahakama wakihofia mahabusu huyo kuwafyatulia risasi.
Mashuhuda hao waliendelea kudai kuwa mmoja wa mahabusu hao alikuwa wa kwanza kutoka kwenye chumba cha mahabusu na alipomkaribia askari huyo ambaye jina wala cheo chake hakijafahamika alimvamia na kumpora silaha hiyo inayodaiwa kuwa na risasi 30 na kuruka uzio mrefu wa mahakama hiyo.
Jeshi la Polisi limewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa washtakiwa hao ambapo limetangaza zawadi nono ya shilingi milioni tano kwa wananchi watakaofanikisha kukamatwa ikiwa ni shilingi milioni 2.5 kwa kila mtuhumiwa.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment