Saturday, October 6, 2012

CHADEMA waitaka CCM isitumie mabavu


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ) kimeitaka serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya utawala bora kuliko kutumia mabavu kama wanavyofanya hivi sasa.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Mbeya Vijijini, Elia Kayolile wakati akitoa salamu za chama hicho kwa wananchi wa Kijiji cha Izumbwe Usafwa, Kata ya Maendeleo, Wilaya ya Mbeya.
Salamu za Mwenyekiti huyo zilitolewa mara baada ya Mwenyekiti wa Tawi la Izubwe, Ramadhani Laiton (CHADEMA) kuachiwa huru kufuatia kukamatwa baada ya kuhoji mapato na matumizi ya kijiji katika mkutano uliofanyika hapo awali.
Kayolile alisema maendeleo yanapatikana kwa kushirikisha wananchi wote na si kwa kutumia mabavu, hivyo ni budi viongozi hasa wa kuchaguliwa na wananchi wakatambua kuwa wapo kwa ajili ya kutetea maslahi ya wananchi na si vinginevyo.
“Nyie viongozi wa CCM msitafute sababu za kufilisi ama kuiba mapato ya wananchi kiujanja ujanja, sisi kama CHADEMA hatutakubali, tutasimama mpaka kieleweke kwani nguvu ya dola kamwe haiwezi kushindana na nguvu ya umma,” alisema.
Alisema anasikitishwa kuona kijiji hicho kilimpeleka mahakamani Laiton kwa sababu tu alihoji uhalali wa ukusanyaji wa fedha za wananchi pasipo risiti, na kuandaa taarifa ya fedha zilizotumika katika kesi hiyo jambo ambalo ni utumiaji hovyo wa fedha za wananchi.
Nae Diwani wa Kata ya Nsalaga, Timoth Mandondo (CHADEMA), alisema kuwa uwepo wa vyama vya siasa sio kutafutiana majungu ama ugomvi bali vipo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wote pasipo kujali itikadi, kwani hata CHADEMA ikichukua madaraka bado itawatumikia hata wale wa CCM.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Herman Mwandimaga, alisema kuwa kukamatwa kwa Laitoni kulitokana na kutotaka kuchangia michango mbalimbali ya maendeleo ya kijiji kama vile ujenzi wa shule, zahanati na madaraja.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment