VIONGOZI wa dini, wamekuja juu na kuonyesha kutoridhishwa na mwenendo wa Jeshi la Polisi nchini, baada ya kudaiwa kumuua Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel TEN Mkoani Iringa, Daudi Mwangosi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, maaskofu hao wamesema tabia ya askari polisi kuhusishwa na matukio ya kumwaga damu, haiwezi kukubalika kwa sababu askari hao wanatakiwa kudhibiti vurugu badala ya kumwaga damu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, maaskofu hao wamesema tabia ya askari polisi kuhusishwa na matukio ya kumwaga damu, haiwezi kukubalika kwa sababu askari hao wanatakiwa kudhibiti vurugu badala ya kumwaga damu.
Katika mahojiano na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, Askofu Msaidizi, Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini, alisema kuna haja Jeshi la Polisi kuacha tabia ya kuzuia maandamano ya vyama vya siasa kwa kuua raia wasio na hatia.
Kwa mujibu wa Askofu Kilaini, Serikali kupitia Jeshi la Polisi, inatakiwa kujiangalia upya katika kuzuia maandamano ya wafuasi wa vyama vya siasa bila kumwaga damu, “Inasikitisha sana, hali ni mbaya, hivi kweli haiwezekani kuzuia maandamano bila kuua, tujiulize hivi hao wanaozuia maandamano wako ‘trained’ vya kutosha katika kuzuia maandamano? Hivi hawawezi kutumia virungu kuzuia maandamano bila kutumia risasi na mabomu ya hatari, hili liangaliwe kwani kuua siyo vizuri,” alisema Askofu Kilaini.
Pamoja na kutoridhishwa na mwenendo wa jeshi hilo, Askofu Kilaini amewaonya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kujitazama upya ili wasiwaingize wananchi katika hali ya kuuawa ovyo wakati wa kutekeleza siasa zao. Alisema si jambo jema kwa chama hicho, kufanya siasa, huku wananchi wakiendelea kuuawa bila hatia.
Naye Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekoste Tanzania, Kanda ya Mbeya, William Mwamalanga, alipozungumza na MTANZANIA jana kwa simu alisema, kuna haja Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmnuel Nchimbi pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, wajiuzulu kufuatia mauaji ya Watanzania wasio na hatia yanayoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi.
Alisema kuwa, viongozi hao wawili, wamepoteza sifa za kuwa walinzi wa raia na kwamba matukio ya mauaji ya kila mara yanayofanywa na askari wa Jeshi la Polisi, yatasababisha nchi kuingia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa tena.
Mchungaji Mwamalanga, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na Haki za Jamii wa Kanisa hilo, alisema Tanzania haiwezi kuendelea kuomboleza damu za watu wasio na hatia, huku viongozi waliopewa dhamana wakiwa kimya maofisini.
Alisema Dk. Nchimbi na IGP Mwema, hawana sababu nyingine ya kutowajibika kwa sababu wameshindwa kulinda uhai wa Watanzania.
“Matukio haya yanaendelea siku hadi siku, hii maana yake ni kwamba, polisi wanataka nchi yetu kuingia katika machafuko na vita ya wenyewe kwa wenyewe, hili halikubaliki, ni vema Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na IGP Mwema, wawajibike kwa kujiuzulu kwa sababu wamesababisha vifo hivyo. Hatuwezi kuendelea kuomboleza vifo vinavyofanywa kwa makusudi na Jeshi la Polisi, huku viongozi hao wakiwa ofisini bila hata kutoa kauli ya kukemea unyama huo unaofanywa na polisi. Tumeshuhudia vifo huko Iringa, Morogoro, Mbeya, Tarime, Arusha na kwingineko kwa sababu tu watu wachache wanaamua kutoa roho za wenzao kwa sababu wanazozijua wao. Sisi kama watumishi wa Mungu, hatuwezi kuendelea kuombea taifa ambalo watu wake wanaendelea kuuawa kila siku, kwa sababu maombi hayo hata Mwenyezi Mungu hawezi kuyasikiliza,” alisema Mchungaji Mwamalanga.
Mchungaji huyo aliendelea kusema kuwa, kamwe maandamano ya CHADEMA, hayawezi kuwa kisingizio na chanzo cha mauaji ya raia, kwa sababu Dkt. Nchimbi na Kamanda Mwema wamekosa busara za namna ya uendeshaji wa taasisi hiyo nyeti.
“Hata katika nchi zilizoendelea kama Marekani watu wanaandamana, maandamano si uhaini, ni kazi ya polisi kulinda na kusindikiza maandamano hayo na si kuua raia wasiokuwa na hatia, kulikuwa na sababu gani kutumia nguvu kiasi hicho. Hili Jeshi la Polisi ni la Watanzania wenyewe, hatujalikodi kutoka nje, polisi wamepoteza sifa, raia wa Tanzania tungekuwa tumelikodi kutoka nje, tungesema hawana uchungu na nchi yao, lakini hawa ni Watanzania wenzetu, kwa nini wameamua kuwa wanyama?” alihoji.
Mchungaji huyo alikwenda mbali zaidi na kusema kuna haja ya kufuatilia kwa kina aina ya askari wanaopelekwa katika operesheni mbalimbali, kwani kuna uwezekano wa kuwepo kwa hujuma za makusudi zinaendelea bila uongozi wa juu wa serikali kujua.
Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam
Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, yeye amewataka wananchi kuwa na subira kutokana na kifo cha mwandishi huyo wa habari.
Akizungumza na MTANZANIA, Sheikh Alhad, alisema kifo cha Mwangosi, kimekuwa na utata kutokana na aina ya silaha iliyotumika.
“Ninachojua ni kwamba, Mwandishi wa Habari anapaswa kufanya kazi yake katika mazingira yoyote sambamba na kulindwa kwa usalama wake. Kwa kifo cha Mwangosi hivi sasa ninaiomba jamii ivute subira ili kuweza kubaini ukweli juu ya chanzo cha kifo chake. Hakika kifo cha ndugu yetu huyo kinapaswa kuwa ni somo tosha, bado ninasisitiza kuwa, tunahitaji kujua nini kilichopelekea kupigwa na hadi kupoteza maisha yake,” alisema Sheikh Alhad.
Mtanzania
No comments:
Post a Comment