WAFANYA KIKAO CHA DHARURA NA KUWEKEANA MASHARTI MAGUMU
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, kuunda tume huru ya kushughulikia vifo vinavyotokea katika hali za utata, hasa vinavyohusisha jeshi hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kumaliza kikao chake na IGP Mwema, Dk. Slaa alisema wamemwambia ikiwa Jeshi la Polisi litaendelea kung’ang’ania kujichunguza katika matukio ya kihalifu huku wakiwa ndio watuhumiwa, CHADEMA hakitakuwa tayari kutoa ushirikiano.
“Tulimwambia ni lazima sheria zifuatwe, na haziwezi kufuatwa kama polisi watajichunguza wenyewe; kwa maana katika hatua hii ya awali tayari wamekwisha kuonesha hali ya kutoaminika kwa kusema milipuko ile ilibebwa na waandishi wa habari,” alisema Dk. Slaa.
Aliongeza kuwa katika hatua hiyo ya awali, walikubaliana na IGP Mwema kuunda kamati ya kufuatilia na kupokea malalamiko.
Kwa upande wa CHADEMA, ameteuliwa Tumaini Makene, na kwa upande wa Polisi atakuwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, Kamishna Robert Manumba. Kamati hiyo imeanza kazi jana.
Alisema makubaliano mengine ni IGP kuruhusu mikutano ya ndani ya CHADEMA kuendelea, na kutoa amri kwa askari wa Mkoa wa Iringa kuruhusu watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo kupelekewa chakula.
Aliongeza kuwa katika makubaliano hayo walimueleza IGP kuhakikisha kila maelezo yake yanayofanyika kati yao na CHADEMA yanakuwa katika maandishi, kwa kile alichoeleza kuwa mara nyingi walipokubaliana, polisi wamekuwa wanageuka.
Kutokana na hilo, CHADEMA imeamua kusitisha ratiba zake kwa siku mbili kupisha shughuli za mazishi. Baada ya hapo, wataendelea na ratiba ya awali ya kujenga chama chao.
Vilio vyatawala Iringa
Nyumbani kwa marehemu Daudi Mwangosi kulitawaliwa na vilio na majonzi. Watu walikaa katika makundi kujadili tukio la kuuawa kwa mwandishi huyo aliyekuwa akifanya kazi katika Kituo cha Televisheni cha Channel Ten.
Wakati watu wakiwa katika hali hiyo, klabu ya waandishi wa habari mkoani hapa imetangaza kususia shughuli zote za Jeshi la Polisi mpaka watakapotoa maelezo ya kueleweka juu ya kuuawa kwa mwandishi huyo ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoani Iringa (IPC).
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Msaidizi wa klabu hiyo, Francis Godwin, alisema wamesikitishwa na matamshi yaliyotolewa na jeshi hilo kuwa bomu lililomuua mwandishi huyo lilitoka kwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
“Tunashindwa kuielewa kauli hii ya Jeshi la Polisi. Iweje bomu wanalodai limerushwa na wafuasi wa CHADEMA liende kumdhuru mwandishi huyo peke yake wakati alikuwa ameshikiliwa na mmoja wa askari wa jeshi hilo baada ya kupigwa virungu, kwa vile tu alitaka kujua sababu za mwandishi mwenzake kukamatwa?” alihoji Godwin.
Ili taarifa hiyo potofu isiendelee kusambaa, aliomba vyombo huru kuingilia kati ili kupata ukweli wa tukio hilo.
Aliongeza katika maazimio yao ya kutoshirikiana na Jeshi la Polisi kuanzia jana, waandishi wa habari wamekubaliana kutokwenda katika ofisi ya kamanda wa polisi mkoani humo kupata habari ya matukio ya kila siku. Aliwaomba waandishi wa mikoa mingine kuwaunga mkono, kwa kuwa msiba huo unawakilisha manyanyaso wanayofanyiwa waandishi nchini kote.
Alisema kwa kuanza waliwataka waandishi wote walio katika Kamati ya Wiki ya Nenda kwa Usalama mkoani hapa kujitoa katika kazi hiyo na kuacha kuripoti matukio yatakayofahamisha shughuli za Jeshi la Polisi, huku akiomba tukio zima la msiba lisiingiliwe na wanasiasa.
Aliongeza kuwa taratibu za kujua mwili wa marehemu utazikwa lini na wapi ni mpaka wawasiliane na ndugu wa marehemu, ingawa taarifa za awali zilisema kuna mpango wa mwili huo kusafirishwa kupelekwa wilayani Tukuyu, Mbeya kwa mazishi.
Wakati huohuo, nyumbani kwa marehemu Daudi Mwangosi umati wa watu uliokusanyika ulilaani tukio hilo na kueleza hali hiyo inasababisha wananachi wazidi kuichukia serikali. Mmoja wa waombolezaji hao, Mwasonga Lusekelo, alisema serikali inapaswa kuacha shughuli za kisiasa kuendelea na kwamba wananchi ndio wenye uamuzi wa kuchuja pumba na mchele.
Alisema kitendo cha kuendelea kuzuia shughuli za kisiasa ni kuzidi kuipa sifa na kuzidisha imani kwa wananchi kuwa serikali ina mambo mazuri ambayo haitaki wananchi wayajue.
Kwa upande wake mke wa marehemu, Itika Mwangosi, hakuweza kuelezea chochote zaidi ya kulia huku akilalamika kuwa mumewe ameshindwa kurudi nyumbani.
“Mwangosiii, Mwangosi uliondoka ukiahidi kurudi mbona sasa hujarudi, limerudi jina lako tu eeeeh Mungu, kwanini wameniondolea mume wangu?” alisikika akilia mke wa marehemu Mwangosi.
Marehemu Mwangosi ameacha mjane na watoto wanne na kati ya hao wavulana ni watatu.
LHRC kuishitaki Polisi ICC
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema kinajiandaa kulishitaki Jeshi la Polisi katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) iliyopo The Hague, nchini Uholanzi.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mkurugenzi wa kituo hicho, Hellen Kijo-Bisimba, alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kuchoshwa na matukio ya mauaji yanayofanywa na polisi.
“Umefika mwisho wa kutoa matamko juu ya matukio ya aina hii. Tunaona ni vema kuyashughulikia kimataifa zaidi,” alisema.
Alisema katika kikao walichoketi jana walikuwa wakitafakari kuliburuza Jeshi la Polisi nchini mahakamani, lakini wameona hiyo haitasaidia kwa kuwa hadi sasa wana takriban kesi 17 walizofungua zenye kufanana matukio na zimekuwa zikipigwa kalenda kila uchwao.
“Tanzania ni mojawapo ya nchi mwanachama katika Fungamano la Haki za Binadamu Afrika, tutaangalia namna gani ya kuzungumza na Umoja wa Mataifa, ili tuone hatua zaidi zikichukuliwe,” alisema.
Kwa mujibu wa Kijo-Bisimba hali ya kukataza watu kufanya mijumuiko si haki ilimradi tu hawavunji sheria na kuhoji iweje hao wakamatwe wakati wengine wamezindua kampeni Bububu?
Alieleza walitegemea polisi wapo kwa ajili ya usalama wa raia, lakini kwa sasa hali imebadilika na hata raia nao wameanza kutokuwa na imani nao.
MCT, wahariri kutoa tamko
Katibu Mkuu wa MCT, Kajubi Mkajanga, alisema: “Kwa maana hii inatutaka wananchi na waandishi tuamini kuwa vitendo vya mauaji vinavyoendelea mikononi mwa vyombo vya dola hasa kwenye mikutano ya vyama vya sisa ni hatari na tusishiriki kutimiza wajibu wetu kikatiba.”
Mukajanga aliwataka waandishi wa habari kuchimbua na kuandika habari za kina hususan za kuuawa kwa Mwangosi, kwani kuna tofauti ya maelezo ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa na Waziri wa Mambo ya Ndani, John Nchimbi.
“Jana nilipoongea na Waziri Nchimbi ambaye yupo safarini kuelekea Durban alisema taarifa alizopewa 'marehemu alilipukiwa na bomu la machozi ambalo halikulipuka kitaalamu’. Kamanda Kamuhanda asubuhi jana alisema kuna kitu kizito kilirushwa ama kuwadhuru polisi ama Mwangosi, hii ni ajabu isiyotakiwa kufumbiwa macho,” alisema Mukajanga na kuongeza kuwa kinachohitajika ni uchunguzi wa kina ili kupata ukweli.
Jukwaa la Wahariri lilisema dalili zote zinaonesha kuwa polisi wanahusika kwa namna moja, kwani kitendo cha kumzingira mtu na kumshambulia kinathibitisha kwamba hawakuwa na nia njema hata kidogo dhidi ya mwandishi huyu.
Katibu Mkuu wa TEF, Neville Meena, alisisitiza: “Kila mauaji yakitokea kumekuwa na visingizio vya watu kuuawa na vitu vizito, siku nyingine watauawa watu 100 tutaambiwa kulikuwa na vitu vizito...Tanzania ya leo si ya mwaka 1961 ambapo taarifa ilihitaji zaidi ya siku kuipata, leo tukio linatokea na muda huohuo watu wanapata taarifa,” alisema.
Akibainisha baadhi ya mambo yanayotia shaka katika tukio la mauaji ya mwandishi Mwangosi, Meena alitoa mfano wa picha zilizotolewa kwenye baadhi ya magazeti na majibizano baina ya Kamanda Kamuhanda na waandishi hususan Mwangosi kwenye mkutano na waandishi kuwa ni dhahiri kulikuwa na agenda ya siri nyuma ya pazia katika mauaji hayo.
“Kwa upande wetu tunasubiri taarifa ya muungano wa vyama vya waandishi wa habari nchini UTPC tutakapokutana tutaungana na makubaliano na uamuzi wa vyama vya waandishi nchini na duniani dhidi ya serikali na vyombo vya habari...tusubiri nadhani kesho au kesho kutwa tutawaambia,” alisema.
Wanahabari walaani
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake nchini (Tamwa), Ananilea Nkya, amesema kitendo cha kutoa roho ya mtu si tu kinalitia aibu Jeshi la Polisi, bali kinataribu taswira ya nchi kimataifa.
Alisema hata kama ni adhabu ya kifo mtu anasikilizwa kwanza, lakini si walivyomfanyia mwandishi huyo.
“Kitendo hiki kinalitia aibu kubwa Jeshi la Polisi, na hasa IGP, Said Mwema, aliyesema kuwa ataliweka jeshi hilo katika sura ya kisasa, sasa kutoa roho ya mtu ndio ukisasa?” alihoji mkurugenzi huyo.
Alishauri iundwe tume huru ya kulishughulikia suala hilo, kwa kuwa kazi ya polisi ni kulinda raia si kuua.
Chama cha Waandishi wa Habari mkoani Mara (MRPC) kimeeleza kupokea kwa masikitiko makubwa mauaji ya mwandishi huyo.
Mwenyekiti wa chama hicho, Emmanuel Bwimbo, alisema kitendo cha kuuawa kwa mwandishi huyo hakifai kufumbiwa macho, kwani hakuwa na kosa lolote tofauti na kutimiza wajibu wake.
Bwimbo alisema Jeshi la Polisi hivi sasa limepoteza heshima, kwani limekuwa na kazi ya kuua watu, tofauti na kuwalinda watu.
“Kwa kweli sasa tunakoelekea ni kubaya maana hawa polisi sasa kazi yao ni kuua si kulinda, juzi wameua mgodini Nyamongo na hazijapita siku wameua tena mwandishi kwa kweli wakati umefika sasa hata sisi kutowapa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kutoandika habari zao,” alisema.
Nao wanaandishi wa habari mkoani Dodoma wamelaani mauaji hayo na kusema kamwe hawakubaliani na nguvu kubwa iliyotumiwa na Jeshi la Polisi katika tukio hilo.
Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoani Dodoma (CPC), Habel Chidawali, alisema kamwe jeshi hilo haliwezi kujitetea kwa kudai kifo cha mwandishi huyo ni bahati mbaya.
Alisema Jeshi la Polisi limekuwa likionesha wazi wazi kuwa linatumia nguvu, ubabe na matumizi mabovu ya silaha za moto ambayo hayajaweza kusaidia siku zote na badala yake kinachoachwa ni maumivu na vilio kwa wananchi.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari nchini (TUJ), Samson Kamalamo, alisema ni simanzi kumpoteza mwanahabari huyo na angependa kitendo hicho kichukuliwe kama funzo kwa vyombo vya habari kuwapatia bima wafanyakazi wake pamoja na kuhakikisha wanawapatia mafunzo jinsi ya kuripoti matukio kama hayo.
“Kabla ya kifo hiki TUJ tulishatoa mafunzo ya jinsi ya kuripoti habari kama hizi za migogoro, lakini kwa upande mwingine polisi wanapaswa kuwa makini katika kutekeleza majukumu yao. Maji ya kuwasha ni bora zaidi kuliko utumiaji wa silaha,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DPCT), Joseph Kayinga, alisema kadiri siku zinavyosonga mbele, mazingira ya wanahabari yanakuwa katika hali hatarishi.
Polisi yajitetea
Mkurugenzi wa Operesheni wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, amesema jeshi hilo halina bomu lililotumika kumuua mwandishi huyo.
Akizungumza katika kituo cha radio cha Magic FM jijini Dar es Salaam, Chagonja, aliwataka wananchi kuwa watulivu wakati jeshi hilo likifanya uchunguzi wa kifo hicho.
Alisema timu itakayofanya uchunguzi itaongozwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema pamoja na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba na maofisa wengine wa jeshi hilo.
“Tunawaomba wananchi wa Iringa wawe watulivu wakati Jeshi la Polisi likifanya uchunguzi wa tukio hili,” alisema Chagonja.
Pamoja na hayo, alivitaka vyama vya siasa kutii sheria zilizowekwa katika kufanya maandamano, ili kudumisha amani nchini.
Kwa upande wake, Mchungaji na Mwalimu wa neno la Mungu katika Kanisa la Evangelist Asembless of God (EAGT) Jimbo la Dodoma Magharaibi, Emanuel Msengi, amekemea tabia ya Jeshi la Polisi kutumia nguvu na silaha za moto na kusababisha vifo vya watu wasiokuwa na hatia.
“Sasa taifa linaanza kupoteza mwelekeo, kwani inaonesha wazi kuwa nguvu ya Mungu imetoweka katika taifa na roho ya mauaji kwa watu wasiokuwa na hatia inatawala,” alisema.
Kuhusu kuunda tume ya kuchunguza mauaji hayo, alisema ni matumizi mabaya ya fedha za walipakodi, kwani inaonesha wazi kuwa waliohusika ni askari wa Jeshi la Polisi na hakuna sababu yoyote ya kuunda tume.
Maoni ya wadau mbalimbali
Watu wa kada mbalimbali wamelaani tukio la mauaji ya mwandishi wa habari wa Televisheni ya Channel Ten, Daudi Mwangosi.
Akizungumza katika ofisi za Tanzania Daima, Sifa Majura, alieleza kushangazwa na kitendo cha kikatili kinachodaiwa kufanywa na jeshi hilo.
Alisema ni uonevu uliopitiliza, askari polisi kwa makusudi kukatisha uhai wa mwandishi huyo aliyekuwa akitimiza majukumu yake.
“Uko wapi utawala bora tunaouhubiri kila mara…hakuna bali kinachofanyika ni kuudanganya ulimwengu, ili tuendelee kupata fedha za wahisani hao,” alisema.
Alihoji kuwa ni kitu gani cha dhambi alichotenda mwanahabari huyo hadi jeshi hilo lifikie hatua ya kutenda unyama wa aina hiyo.
Aliutaka umma wa Watanzania kuamka na kuacha kukaa kimya, ili kupinga unyama huo ambao hauvumiliki.
Huku akiifananisha nchi ya Marekani alisema pamoja na kuwa na maadui wengi lakini katika mikusanyiko na maandamano ya raia polisi wake hawaendi na risasi za moto.
“Nashangaa hapa nchini Jeshi la Polisi ni wapi wanataka kutupeleka…wenzetu kule pamoja na vurugu lakini hawabebi risasi za moto zaidi ya virungu na mabomu ya machozi,” alisema.
Naye, Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Mbeya, William Mwamalanga, alisema Jeshi la Polisi linapoteza dira kwa kuwa linashindwa kulinda raia na sasa limegeuka kuwa la kiuaji.
Alisema hatua hiyo inajenga chuki miongoni mwa jamii, kwani jeshi hilo linaonesha wazi kuwa linatumiwa na vyama vya siasa.
Alisema hali iliyoanza kujionesha sasa hivi kuna hatari kubwa kuja kuibuka wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Mwamalanga, aliwataka viongozi wa jeshi hilo kukubali kuwajibika na kujiuzulu kutokana na kushindwa kazi.
“Katika muda mfupi tu mauaji yanaibuka kila mahali, nadhani wakati umefika wa viongozi wakuu wa jeshi hilo kukubali kujiuzulu bila shuruti,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa asasi inayojihusisha na masuala ya afya ya Sikika, Irenei Kiria, amelaani kitendo hicho na kusema ana matumaini waliohusika katika mauaji hayo watachukuliwa hatua kwa kufikishwa katika vyombo vya dola, ili sheria ichukue mkondo wake.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia nchini (TGNP), Ussu Mallya, alisema, kitendo kilichofanywa ni cha kusikitisha, kuhuzunisha na kushangaza kwa kuwa, polisi sasa wameacha kufanya kazi yao ya kulinda raia na kufanya mauaji.
“Msingi wa polisi wa kulinda raia unaanza kuporomoka, ni vitendo vinavyozidi kuendelea bila kuchukuliwa hatua madhubuti ya kuvikomesha raia wengi watapoteza maisha,” alisema.
Alisema anapouawa mwanahabari ambaye amejitolea kuhabarisha wananchi hicho ni kitendo cha kutisha waandishi wengine na kuwanyamazisha washindwe kufanya kazi zao kwa uhuru.
Alisema wanaohusika wafanyiwe uchunguzi kwa kuwa vitendo hivi visipodhibitiwa vitazidisha vurugu.
Msingi wa polisi kulinda raia umeporomoka kwani sasa wamegeuka walinzi wa chama cha mapinduzi na wanapokea na kutekeleza amri za CCM. Hili halina utata kama alivyosikika Wasira katika kipindi TBC1 ambapo alionekana wazi kuunga mkono mauaji hayo kwa kujariku kuelekeza lawama kwa CHADEMA.Badala ya kulinda rai na mali zao wamegeuka wauaji wa wananchi hasa wale wanaoonekana kuwa ni wana mageuzi. Hali hii inatisha na sijui watatuua mpaka lini
ReplyDelete