Friday, September 7, 2012

Tendwa ajipalia makaa


SIKU moja tangu Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, ajitokeze na kulaani mauaji ya raia yaliyofanywa na polisi kwenye mikutano ya kisiasa na kutishia kuvifutia usajili vyama vinavyojihusisha na vurugu, wanasiasa wamemshukia vikali.
Wakati Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahimu Lipumba, akidai Tendwa ni bomu na mvurugaji wa vyama vya siasa, CHADEMA wamemtaka msajili huyo aanze kwa kukifuta CCM ambacho kimekuwa na matukio ya kufanya fujo.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Profesa Lipumba, alisema ameshangazwa na kauli ya Tendwa ambayo inaonyesha wazi kashindwa kusimamia haki ya vyama vya siasa na matokeo yake ameamua kuvuruga mambo.
Alisema kuwa Tendwa hapaswi kutoa vitisho kwa vile vyama vimekuwepo kwa utaratibu wa sheria, na hivyo kazi yake si kushauri polisi kama ambayo ameonyesha katika kauli yake.
“Najua Tendwa anataka kutuonyesha kuwa labda yeye ni kada wa chama fulani cha siasa, lakini sitaki kuamini hilo bali anachotakiwa kufanya ni kuacha kujichanganya na kauli anazozitoa,” alisema.
Prof. Lipumba alisema kuwa hatua ya kutoa vitisho hivyo sio tu inazidisha chuki kwa wananchi, bali pia inaongeza vurugu zisizokuwa na msingi.
Wao CHADEMA kupitia kwa mkuu wa Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), Benson Kigaila, walisema Tendwa angeanza na CCM ambayo inaingiza silaha nchini, kuweka vijana makambini na kuwafunza mbinu za kufanya fujo.
Alisema kuwa wamekuwa wakitoa taarifa za kuilalamikia CCM kuhusiana na fujo hizo, lakini Tendwa amekaa kimya na badala yake anawazushia wao kuwa ndiyo wanafanya vurugu.
Naye Mchungaji wa Pentekoste, William Mwamalanga kutoka mkoani Dodoma, alisema kuwa Tendwa anatakiwa kuwa na hekima na busara wakati huu ambao taifa lipo katika majonzi ya kumpoteza mwanahabari.

“CHADEMA ina watu wengi na pia ni kati ya vyama vinavyolalamikia kuhujumiwa na Jeshi la Polisi, hivyo kauli kama hiyo anayoitoa inaweza kuzidisha uhasama miongoni mwa jamii,” alisema.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Life Way Ministries, lenye makao yake makuu mjini Dodoma, Elia Mauza, naye alisema kuwa kauli ya Tendwa ni ya kukurupuka na haina ufumbuzi wa kutatua tatizo la mauaji yanayosababishwa na polisi.
Alisema kamwe Jeshi la Polisi halina nafasi ya kujikwamua katika tukio hilo la mauaji ya mwandishi kwani alikuwa kazini.
“Hapa Tendwa asitafute njia ya kulisafisha Jeshi la Polisi na kuonyesha kuwa waliosababisha kifo ni wanasiasa, polisi hawana nafasi ya kutoka juu ya jambo hili,” alisema.
Naye Kamishna wa NCCR-Mageuzi Mkoa wa Dodoma, Kayubo Kaptari, alisema kuwa kwa sasa siasa za nchi zinaelekea kubaya na kinachosababisha ni Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kuingiwa na hofu ya kuondoka madarakani.
“Tendwa anatakiwa kueleza ni chama gani cha siasa cha upinzani ambacho kinamiliki silaha kama si Jeshi la Polisi ambalo lipo chini ya Serikali ya CCM,” alisema.
TCD wamtaka Pinda
Katika hatua nyingine, Kituo cha Demokrasia nchini (TCD), kimeomba kukutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa dhumuni la kuzungumzia hali halisi ya mauaji ya utata yanayoendelea kutokea nchini na kufanywa na vyombo vya usalama.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa kituo hicho, James Mbatia, alisema kuwa vyama vyote sita vyenye wabunge pamoja na kimoja kinachowakilisha vyama visivyo na wabunge vimekubaliana kukutana na Pinda haraka iwezekanavyo.
“Kukutana na waziri mkuu ni muhimu kwa vyama vyote vya siasa tukimuhusisha IGP na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa sababu viko chini yake, hivyo ni vema kukutana naye kujadili hali hii tete inayolikabili taifa,” alisema Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi.
Aliongeza kuwa hali hiyo ya mauaji inapaswa kudhibitiwa haraka ili isiendelee nchini kwa sababu inaweza kuota mizizi na kusababisha maafa kwa wananchi.
“Tunataka kukutana na waziri mkuu haraka, wakati wowote uwe usiku au mchana ili kujadili jambo hili la dharura, juzi tulifika ofisini kwake tukaambiwa yupo katika mkutano na mmoja wa viongozi kutoka nchini China,” alisema.
Aidha, kituo hicho kimelaani mauaji hayo na kuyafananisha na ukiukaji wa katiba kwa sababu yanafanyika kinyume na katiba ya nchi ibara ya 14, inayosema kila raia wa nchi hii ana haki ya kuishi.
“Tunasikitika kutokana na vifo hivyo ambavyo vimetokea Arusha, Singida, Songea, Morogoro hivi vya karibuni na juzi Iringa,” alisema Mbatia ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa.
Vyama hivyo vyenye wabunge bungeni ni CCM, CHADEMA, CUF, UDP, NCCR- Mageuzi na TLP.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment