Friday, September 7, 2012

Kada CCM Songea atimkia CHADEMA


ALIYEKUWA Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mjimwema katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Magdalena Gama, amejivua uanachama wa chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kuona kimekosa mwelekeo.
Gama alitoa kauli hiyo jana kwenye Ofisi ya CHADEMA, Kata ya Mjimwema alipokuwa akikabidhiwa kadi mpya na Mwenyekiti wa chama hicho, Tawi la Pachanne, Swedi Milanzi.
Alisema ameamua kuihama CCM baada ya kuona baadhi ya viongozi wake, wamekuwa na tabia ya ubinafsi na kuonekana ni mali yao binafsi.
Alisema amejiunga na CHADEMA kwa kuwa ndicho chama pekee chenye sera nzuri zenye tija kwa Watanzania wote bila kuwepo matabaka.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho, Samweli Chale, alisema kitendo alichokifanya Gama ni cha kiungwana, kwani CCM imejaa fitina hasa kwa wale viongozi wanaoonekana kwa jamii kuwa makini.
Chale ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Kata ya Bombambili, alisema msimamo wa chama hicho ni kuboresha zaidi maendeleo mbalimbali ya wananchi na kina malengo ya kuhakikisha kinashika dola kuanzia ngazi ya uongozi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji na kwamba hakuna chama kingine chenye kipaumbele zaidi ya CHADEMA.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment