RUFAA ya kupinga kuvuliwa ubunge wa aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), inatarajiwa kusikilizwa leo na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa chini ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande na wenzake, Natalia Kimaro na Salum Massati.
Hata hivyo, habari za uhakika kutoka mahakamani hapo zinaeleza kuwa tayari mawakili wa pande zote mbili wameandika barua ya kuomba kusogezwa mbele kwa shauri hilo hadi Oktoba 2, mwaka huu, kufuatia mawakili, Tundu Lissu, anayemtetea Lema na kaka yake, Alute Mughwai, anayewatetea walalamikaji, kufiwa na baba yao mzazi.
Shauri hilo lililokuwa likisubiriwa kwa hamu na wakazi wengi wa Jiji la Arusha na Watanzania wengi linatarajiwa kusikilizwa kwa siku moja kisha kupangiwa tarehe kwa ajili ya kutoa uamuzi.
Wakili Mughwai anashirikiana na wakili Modest Akida kuwawakilisha wadaiwa kwenye shauri hilo ambao ni wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Mkanga, Agness Mollel na Happy Kivuyo, waliofungua shauri lililotengua ubunge wa Lema wakidai kuwa wakati wa kampeni alimdhalilisha mgombea wa CCM, Dk. Batilda Burian kwa kutumia lugha za matusi.
Awali, Lema kupitia wakili wake, Method Kimomogoro, anayesaidiana na Lissu, aliwasilisha kwenye mahakama hiyo hoja 18 za madai akipinga kutenguliwa kwa ubunge wake na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Aprili 5, mwaka huu.
Kwenye baadhi ya madai hayo, Lema aliiomba Mahakama ya Rufaa kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu, uliotengua ubunge wake, huku akiitaka imtangaze kuwa mbunge halali wa Jimbo la Arusha Mjini.
Aidha, aliitaka mahakama hiyo ya juu, iwaamuru walalamikiwa katika shauri hilo walipe gharama za rufaa hiyo pamoja na zile za kesi iliyomalizika kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Katika madai mengine, Lema anamlalamikia Jaji Gabriel Rwakibarila, aliyesikiliza kesi hiyo kuwa alitoa uamuzi wake kwa kuzingatia maneno ya uvumi, huku akipuuza ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.
Lema anadai kuwa jaji alikosea wakati alipoamua kuwa mpiga kura yeyote anaruhusiwa kupinga matokeo ya uchaguzi hata kama haki zake za msingi hazijaguswa.
Tanzania Daima
Update
Rufaa ya Lema Arusha, kesi yaahirishwa hadi Oktoba 2, 2012
Wakili mwenza wa wakili wa walalamikaji anomba kesi ihairishwe maana wakili mwenza amefiwa na baba yake ambaye ni mzee Lissu na kikao cha familia kitakaa tarehe 27 siku ya alhamisi baada ya kumaliza maazishi hivyo anaweza kuja siku ya ijumaa tar 28 hivyo anomba siku ya hukumu badala ya tar 1 oct bac iwe siku ya tar 2 oct.
No comments:
Post a Comment