Thursday, September 20, 2012

CHADEMA wafanyiwa ubedui Arusha


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani hapa, jana kililazimika kuahirisha mkutano wake uliokuwa ufanyike kwenye uwanja wa wazi wa NMC baada ya kukuta umewekwa uzio wa seng’enge na Halmashauri ya Jiji la Arusha, ikiwa ni maandalizi kwa ajili ya kutumiwa na wafanyabiashara wadogo, maarufu kama wamachinga.
Uzio huo uliwekwa usiku baada ya CHADEMA kuwa wametoa msimamo wa kufanya mkutano kwenye uwanja huo licha ya Jeshi la Polisi kuwazuia kwa madai kuwa kuna mtihani wa darasa la saba ulioanza jana.
Katibu wa CHADEMA mkoani hapa, Amani Golugwa, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa wamefikia uamuzi wa kuahirisha mkutano huo baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wa wamachinga hao na kuona kile walichokuwa wakikipigania kuhakikisha wafanyabiashara hao hawaondolewi mitaani bila kuelekezwa mahali pa kwenda kimetimizwa.
Hata hivyo, alisema kuwa anaamini jambo hilo limefanyika kwa hila na kukurupuka kwa lengo la kuzuia mkutano wao kwani uwanja huo ulikuwa umetolewa kwa kampuni moja ya simu za mkononi kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za promosheni mpaka siku ya Jumamosi, lakini ghafla juzi jioni waliwafuata na kuwataka waondoke kwani uwanja huo unazungushiwa uzio.
“Hili jambo wamelifanya kwa kukurupuka na limejaa hila ndani yake, lengo kuu ni kuzuia mkutano wetu, sisi tunaahirisha si kwasababu ya zuio la polisi, bali tunataka tupishe Wamachinga kugaiwa eneo hilo, ingawa pia tunasikitika kwani wanawahamishia eneo ambalo halina huduma muhimu kama choo,” alisema Golugwa.
Naye Mwenyekiti wa madiwani wa CHADEMA kwenye halmashauri hiyo, Doita Isaya, alisema kuwa kwenye vikao vya madiwani iliamuliwa machinga wahamishiwe kwenye eneo la Samunge ambapo pia walimuomba Rais Jakaya Kikwete kutumia mamlaka yake kurudisha maeneo ya wazi kwa halmashauri hiyo yaliyopo Mbauda na Kilombero.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Godbless Lema, alisema kuwa wakati halmashauri ilipotaka kuwaondoa kwa nguvu wamachinga katikati ya Jiji la Arusha, wao walisimama kidedea kuwataka wasiondoke mpaka watakapooneshwa eneo wanalopelekwa.
Hata hivyo alisema kuwa serikali imeamua kwa makusudi kuwapeleka NMC ambapo nyakati za mvua hujaa maji na tope. Tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini imetangaza kuwepo kwa mvua za el-nino.
Akizungumzia shutuma hizo, Meya wa Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo, alisema kuwa uamuzi wa kuzungushia uzio uwanja huo kwa lengo la kuugawa kwa wamachinga ulifikiwa baada ya halmashauri kuunda kamati ya madiwani ambao walishirikiana na viongozi wa wamachinga.
Alisema kuwa kamati hiyo ilikuja na mapendekezo kuwa uwanja huo ndiyo unafaa hivyo mapandekezo  hayo yakapelekwa kwenye kamati ya mipango miji kisha kamati ya fedha kabla ya kupelekwa kwenye baraza la madiwani ambapo nako lilipitishwa hivyo kilichokuwa kimebaki ni utekelezaji.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment