Monday, September 10, 2012

Prof. Mwandosya alionya Jeshi la Polisi Asema Kifo Cha Mwangosi kiwe Cha Mwisho

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais asiyekuwa na wizara maalumu na Mbunge wa Jimbo la Rungwe Mashariki, Prof. Mark Mwandosya, amesema kuwa kifo cha mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi, aliyeuawa na polisi kiwe cha mwisho.

Kauli ya Waziri Mwandosya inafuatia mahojiano ya moja kwa moja yaliyofanywa na Tanzania Daima Jumapili katika Kijiji cha Busoka, Kata ya Itete mkoani Mbeya ambapo alikuwa miongoni mwa waombolezaji waliojitokeza kumzika mwandishi huyo.


Prof. Mwandosya akiwa anatokea nyumbani kwake katika Kijiji cha Lufilyo ambapo yupo katika mapumziko ya kiafya, aliweza kujikongoja hadi msibani hapo huku afya yake ikiendelea kuimarika zaidi na hakuacha kusema yale ambayo yamemgusa juu ya kifo hicho.


“Hii inaniuma sana, watoto wadogo tuliowazaa tunashuhudia wakifa hivi hivi, mazingira ya kifo hiki yamenisikitisha sana, naomba kifo cha Mwangosi kiwe cha mwisho, sipendi kusikia tena mambo kama haya yakitokea tena, iwe mwisho, iwe mwisho kabisa,” alisema Prof. Mwandosya.


Licha ya waziri huyo kuonyesha huzuni na majonzi makubwa juu ya kifo hicho, alidai kuwa msiba huo ni changamoto kwa serikali, wananchi na viongozi wa vyama vya siasa kuwa ipo haja ya kujitathimini zaidi juu ya hali ya nchi ilivyo na ulinzi na usalama wa raia unavyozidi kulegalega.


“Tangu tupate uhuru miaka 50 iliyopita enzi za Mwalimu Nyerere haya mambo hayakuwepo, nchi ilikuwa na heshima kubwa na Mtanzania alisifika na kuheshimika popote duniani anakokwenda. Leo hii tunakwenda wapi? Tukienda nje tutaambiwa hawa wanatoka kwenye nchi ya vurugu,” alisema Mwandosya.


Uhusiano wake na Mwangosi

Prof. Mwandosya alieleza wazi uhusiano mkubwa aliokuwa nao kati yake na marehemu Mwangosi kuwa alikuwa sehemu ya familia yake, kama mtoto wake, kndugu yake, kijana wake na aliweza kufanya nae kazi kwa karibu.

Kuwa mara kadhaa alikuwa akipokea ushauri mzuri kutoka kwake. Licha ya kumzidi umri aliweza kupokea kwa umakini mkubwa maneno ya busara na ushauri aliokuwa akipewa na marehemu, kuwa hakuwa mwepesi kuburuzwa kwa kile alichokuwa akiamini kuwa hakifanywi sawa na waziri huyo.


“Nilikuwa mahali pengine natofautiana na kabisa na marehemu kutokana na msimamo wake, tuliweza hata kukosana, lakini hakusita kuniuliza maswali mengi na mengi yalikuwa ya msingi, hakuwa mtu wa kuridhika na jambo aliloona si sawa, hakika huyu mtoto wangu ameniuma sana, Mwangosi kaniuma, kifo chake kiwe cha mwisho kutokea katika mazingira kama haya,” alisema.


Prof. Mwandosya alisifu ukuaji wa demokrasia hapa nchini, akizitofautisha siasa zake na nchi jirani ya Kenya kuwa ni vigumu viongozi wa serikali iliyopo madarakani kuweza kukaa meza moja na upinzani hasa kwenye matukio mabaya kama haya ya mauaji.


Aliviasa vyama vya siasa kikiwepo chama chake CCM kuwa visiwe chanzo cha vurugu na machafuko yanayotokea katika kampeni, mikutano ya hadhara na maandamano.


Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment