IMEBAINIKA kuwa mwenendo wa mauaji yanayofanywa na Jeshi la Polisi katika mikutano na maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ni mkakati wa makusudi uliosukwa na watawala ili kukivuruga chama hicho, na kuwatisha wananchi kwamba ni chama cha fujo.
Hii si mara ya kwanza kwa watawala kufanya njama hizi dhidi ya wapinzani. Mara ya mwisho, waliofanyiwa hivyo ni Chama cha Wananchi (CUF), kilipokuwa chama kikuu cha upinzani.
Njama hizo zilikiangusha chama hicho, hadi kikajisalimisha kwa kufunga ndoa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, huku kikipoteza mvuto Tanzania Bara.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wameliambia gazeti hili kuwa, CHADEMA inapaswa kuwa macho na njama hizi, kwani CCM imegundua kwamba inazidi kudhoofika na CHADEMA kinazidi kuimarika katika jamii; hivyo walio madarakani wanafanya kila njama kuua wapinzani ili wabaki madarakani.
Siku chache zilizopita, polisi walimuua kijana Ally Zona wakati wakitawanya waandamanaji wa CHADEMA mjini Morogoro. Jumapili iliyopita wameua mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Daud Mwangosi, mkoani Iringa na kuleta sokomoko la kitaifa, ambalo limelichafua mno Jeshi la Polisi na Tanzania mbele ya jumuiya ya kimataifa.
Utetezi wa polisi na jitihada zake kuwasingizia CHADEMA, waandishi na wananchi wengine kuwa ndio walifanya mauaji hayo, umegonga mwamba kwa sababu katika matukio yote haya, wapo mashahidi waliokuwapo pale pale.
Matukio haya yanatokea wakati ambapo vita ya kisiasa baina ya chama kilichoko madarakani na CHADEMA ikizidi kuongezeka kutokana na uungwaji mkono mkubwa unaopata chama hicho cha upinzani kwa sasa kuliko historia ya wakati mwingine wowote.
Kasi ya kukua kwa CHADEMA katika miaka ya karibuni inatishia madaraka ya watawala ambao wamekuwa madarakani kwa miaka ipatayo 50, na ambao chama chao, CCM, kimepoteza mvuto kwa umma, na hakiaminiki kutokana na kuzongwa na tuhuma nyingi za ufisadi, na kukumbatia makundi hasimu yanayotafuta madaraka na masilahi mengine, huku yakiendelea kudhoofisha uongozi wa CCM uliokwisha nyong’onyea.
Wakati CHADEMA kikipambana kukumbatia mapenzi ya umma unaokiunga mkono, huku kikifungua misingi na matawi vijijini, CCM inahaha kukidhibiti kwa propaganda na nguvu za polisi.
Kwa muda mrefu, CCM imejaribu kukipaka CHADEMA matope ya ukanda, ukabila na udini, kama ilivyofanya kwa CUF miaka ya nyuma; lakini baada ya kuona mbinu hizo zimeshindikana, sasa imeamua kutumia jeshi kutisha viongozi wake na wananchi kwa visingizo mbalimbali.
Hata hivyo, CHADEMA kinasema kimejiandaa vema kukabililiana na propaganda zote na vitisho vya watawala; na kwamba kimejifunza kwa makosa waliyofanya wengine katika NCCR-Mageuzi na CUF.
Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu, anazo tafsiri tatu za matukio ya mauaji yanayofanywa na polisi katika mikutano ya CHADEMA.
Anasema: “Hawana majibu na matatizo ya wananchi, hawana majibu na tatizo la maji, elimu, matibabu ya uhakika na kero kadha wa kadha zinazowakabili wananchi. Kwa sababu hawana jibu, wanatumia nguvu. Sasa hawatumii vitisho tu, wanatumia nguvu.
“Hii ni taswira ya ‘system’ (mfumo) inayojua inaondoka. System imara haitumii nguvu, inatumia vitisho, kama kupeleka watu mahakamani. Sasa huko tumekwishapita, tumeingia katika hatua ya kuuawa.”
Tafsiri ya pili ya Lissu, ambayo ina uhusiano na ile ya kwanza, ni kwamba kwa vile watawala wanaona wako hatarini kuondoka, wanatafuta namna ya kuwachafua CHADEMA kwa wananchi ili wawaogope.
“Ikishindikana kutuchafua kwa propaganda wanaua. Wanaua watu kwenye mikutano na hadharani. Maana yake ni nini? Ni kwamba wanatuma ujumbe kwa jamii kwamba ukienda kwenye maandamano ya CHADEMA utakufa. Tafsiri yake ni kwamba watu waogope,” anasema Lissu.
Tafsiri yake ya tatu ni kwamba, watawala wanatengeneza mazingira ya kisiasa ili CHADEMA kionekane chama cha vurugu, ili utafutwe msingi wa kukifutia usajili.
“Ukishafanya mauaji kwenye mkutano unajenga mazingira ya kusema hiki chama hakina sifa, unamtengenezea mazingira msajili wa vyama vya siasa akiondoe…ukikiondoa CHADEMA maana yake umeondoa mgogoro na bungeni…utawaondoa akina Lissu, akina nani kule… Hivyo, nasema wanatafuta sababu ya kuendelea kutawala kupitia kuua raia,” anasema Lissu.
Anasisitiza kwamba kwa mantiki hiyo, Jeshi la Polisi limeacha kazi yao ya msingi ya kulinda raia na mali zao, na sasa limegeuka jeshi la kulinda walio madarakani ili waendelee kutawala.
“Jeshi limegeuzwa chombo cha ulinzi wa watawala. Hilo la kusema kwamba kazi ya Jeshi la Polisi ni kulinda raia na mali zao ni siasa, lakini the primary function (kazi yao ya msingi) ambayo hawaisemi ni hii ya kulinda watawala ili waendee kuwepo,” anasema Lissu.
Aidha, wachambuzi wanasema kinachotokea sasa ni kwamba watawala wanaanza kuhamanika, na wanaweza kutumia polisi kutenda mambo ambayo hatima yake itakuwa mbaya kwao, kama ilivyokuwa kwa watawala wa mataifa mengine waliofikishwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu dhidi ya binadamu, The Hague, Uholanzi.
Taratibu, kwa sababu ya matumizi mabaya ya Jeshi la Polisi, hata sifa ya Tanzania katika jamii ya kimataifa inaanza kuchafuka.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment