Thursday, September 6, 2012

CHADEMA waikataa tume ya Nchimbi


TENDWA AIBUKA, ATISHIA KUWAFUTIA USAJILI
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeipinga tume ya kuchunguza mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa Channel Ten, Daudi Mwangosi, iliyoundwa na Waziri wa Mambo wa Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, kwa maelezo kuwa inaongozwa na jaji asiye na sifa.
Kimesema kuwa Jaji huyo mstaafu, Stephen Ihema, anafahamika ni mtu asiyejua kazi, kwani ameshindwa kutoa hukumu katika kesi zaidi ya 300.
Akizungumza na waandishi jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa chama hicho, Tundu Lissu, alisema kutokana na Jaji Ihema kutoweza kazi, hata Jaji Bernard Luanda alipata kumkosoa kwa kutoa waraka kwa majaji wote mwaka 2005.
“Kama mnafuatilia taarifa za hivi karibuni, Ihema ni mmoja wa majaji waliopo kinyume cha sheria na Katiba. Aliteuliwa kuwa jaji enzi za Benjamin Mkapa, ilipofika mwaka 2003 kwa sababu hakuwa anajua sheria,” alisema.
Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki, aliongeza kuwa Ihema hajui kazi ya ujaji na kwamba alisharundika zaidi ya kesi 300 ambazo anashindwa kuziandikia hukumu. Na kuwa mtu ambaye anajulikana kutokuwa na uwezo wowote wa kufanya kazi ya kisheria.
“Ndugu zangu na hili naomba nirudie maana wasiseme tumeanza maneno yetu, mwaka 2003 kabla mimi sijawa mbunge kuna mtu anaitwa Joram Alute, ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Singida kwa sababu ya ubovu wa Jaji Ihema, Joram alimwandikia Rais Mkapa barua ya kumuomba kumuondoa Jaji Ihema Mahakama Kuu, kwa sababu hakuwa na uwezo wowote wa kufanya kazi ya ujaji.
Miaka karibu 10 wana CCM, Joram Alute, si CHADEMA, alisema hawezi kazi, aidha ni mvivu au hajui namna ya kuandika hukumu, hafai kuwa jaji,” alisema Lissu.
Aliongeza kuwa mwaka 2005 Jaji Ihema alikuwa amemaliza mkataba wa kwanza na kupewa mwingine wa kazi ya ujaji, hali ambayo ilimfanya Jaji Bernard Luanda (sasa Jaji wa Mahakama ya Rufaa), baada ya kuandikiwa na Jaji Manento kuwa Ihema amepewa mkataba wa ujaji, aliandika waraka uliosambazwa kwa majaji wote kuwa Ihema si jaji kwa mujibu wa Katiba.
Alisema kwa mujibu wa sheria za nchi, majaji wanateuliwa, hivyo Jaji Ihema kupewa mkataba ni kinyume cha sheria na katiba.
Lissu alieleza kuwa hata alipopelekwa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, tume hiyo ilikuwa ni ya kuficha uchafu na madhambi ya viongozi, kwani ilikuwa kimya kwa miaka yote huku viongozi wakishiriki kufilisi taifa.
Alisema kutokana na maelezo hayo ni dhahiri kuwa Ihema hana uwezo na pia maadili yake ni ya mashaka, kwani hilo linafahamika ndani ya mahakama.
Pamoja na hilo, alisema tume hiyo imeundwa kwa lengo la kurekebisha mambo baada ya Jeshi la Polisi kukamatwa mchana kweupe wakifanya mauaji.
“Ni tume ambayo lengo lake si kuchunguza mauaji, ni kuondoa hii picha ya mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi hadhaharani…hii ndivyo tunavyoiangalia.
Kwa kuwa si tume ya kuchunguza mauaji sisi kama chama hatutaiunga mkono na tutawashauri wananchi wa Tanzania, wawe wanachama wetu, wasiwe wanachama wetu, wasiiunge mkono,” alisema.
Nchimbi akosolewa
Lissu alisema kwa mujibu wa sheria ya kuunda tume za uchunguzi mwaka 1962 sura ya 29, anayepaswa kuunda tume ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutoa hadidu rejea na kwamba kulingana na utaratibu huo si jukumu la waziri kuunda tume.
Alisema tume za aina hiyo zinatoa ripoti kwa rais au zinaweza kutoa taarifa hadharani endapo rais ataelekeza hivyo katika hadidu rejea.
“Hivyo kwa matukio makubwa ya kitaifa yanayotokea, kisheria ni jukumu la rais, si jukumu la waziri ambaye anawasimamia watuhumiwa wa hicho kinachotakiwa kuchunguzwa.
Kwa hiyo katika upeo huo wa kisheria, Waziri Nchimbi hana mamlaka ya kuunda tume ya kuchunguza mauaji hayo,” alisema.
Lissu alifafanua kuwa walioua ni polisi ambao inawezekana waliamriwa waue na wakubwa zao kisiasa (waziri) au kiutendaji (IGP na maofisa wengine wa jeshi), hivyo kama unachunguza mauaji yaliyofanyika waziwazi, inawezekana yamefanywa kwa amri za kisiasa au kiutendaji.
Hivyo alihoji kama tume hiyo ina uwezo wa kumhoji waziri au IGP na kusema kuwa: “Tume hii ni danganya toto, ya kitchen party, pengine na ya marafiki, ili kuondoa picha mbaya kwa Jeshi la Polisi,” alisema.
Wajumbe wake waguswa
Lissu alisema Naibu Kamishna wa Polisi, Isaya Mungulu, kutoka makao makuu hana uwezo kwa kumuita waziri au IGP kwa ajili ya kumhoji kuhusiana na mauaji hayo.
Kuhusu mtaalamu wa mabomu, Wema Wapo, kutoka Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) alihoji kuwa anakwenda kuchunguza kitu gani kisichojulikana, kwani katika picha muuaji anajulikana.
“Inaonekana ni bomu la machozi ambalo alipigwa nalo, ambalo limemchanachana. Sasa ni kitu gani kisichojulikana. Sasa unaita mtaalamu achunguze mlipuko upi ambao haujulikani?” alihoji.
Kwa upande wa Theopili Makunga kutoka Jukwaa la Wahariri (TEF) na Pili Mtambalike kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT), alisema hao ni waandishi wa habari na kuhoji iwapo wana utaalamu wa kuchunguza vifo.
“Hii ni tume ya marafiki, yenye lengo la kukosha mauaji yaliyofanywa na marafiki, kwa vyovyote vile hii si tume halali ya kuchunguza mauaji ya Mwangosi,” alisema Lissu.
Hadidu rejea zapingwa
Lissu alihoji ni mtu gani asiyefahamu chanzo cha mauaji hayo, kwani vyombo vya habari vimemuonyesha kupitia picha, hivyo kuhoji tume hiyo inakwenda kuchunguza kitu gani.
Kuhusu swali kama kweli kuna uhasama kati ya polisi mkoani Iringa na waandishi, alihoji iwapo tume hiyo inakwenda kuchunguza mauaji ama uhasama.
Kwa upande wa swali kama nguvu iliyotumika na polisi ilikuwa sahihi, alisema kuwa hilo ni suala la kisheria na pia kunahitajika ushahidi.
“Kuhusu swali linalohoji mahusiano kati ya polisi na vyama vya siasa. Hili liko wazi kabisa kwa sababu sijawahi kusikia Jeshi la Polisi limevunja mikutano ya CCM, kwa hiyo hapa wanakwenda kuichunguza CHADEMA,” alisema.
Aliongeza kuwa iwapo wanataka kuchunguza suala hilo kwa nini Mungulu yupo kwenye tume hiyo na hakuna mtu wa CHADEMA wala Msajili wa Vyama vya Siasa au mwakilishi wake.
“Hii si tume ya kuchunguza mauaji, ni ya kufunika mauaji haya…hatuwezi kukubaliana na tume hii,” alisema.
Mbali na hilo, alisema kuna haja ya kuchunguza matukio mbalimbali ya mauaji yaliyotokea hivi karibuni likiwemo la Morogoro, Arusha, Igunga na Arumeru Mashariki.
“Matukio yote haya hayajachunguzwa inavyostahili. Hatutaki mambo yaishe hivi hivi,” alisema.
Mapendekezo yao
Kutokana na hali hiyo, alisema chama hicho kinamtaka Rais Jakaya Kikwete kuunda tume ya uchunguzi wa mauaji ambayo itaongozwa na majaji waadilifu na kwamba itakuwa bora iwapo watatoka Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu, ambao watafanya uchunguzi wa wazi.
“Katika tume hiyo mashahidi watakuwa wakiitwa hadharani. Tume za aina hii hazipo, lakini kwa mujibu wa sheria Rais anaweza kuunda tume hiyo. Hatutaki uchunguzi wa kificho ambao unaonesha polisi hawakukosea,” alisema.
Alieleza kuwa tume hiyo itakuwa na mamlaka ya kumuita mtu yeyote isipokuwa rais. Na kwamba kwa kuwa muuaji anajulikana, chama hicho kinataka askari wote waliohusika wakamatwe na kufunguliwa kesi ya mauaji.
“Tunajua si wote walioua, ila katika sheria kuna kitu kinaitwa common intension, mmoja ameua, lakini alioshirikiana nao wanahusika. Hili linawezekana kwa kuwa kuna ushahidi,” alisema.
Alisema iwapo rais hataunda tume hiyo, kuna njia nyingi za kuendelea na suala hilo, na kusema hilo chama kinapaswa kutoa kauli.
Wataka Nchimbi ajiuzulu
Katika hatua nyingine, Lissu alisema kutokana na tukio hilo, Waziri Nchimbi anapaswa kuwajibika kisiasa kwa kujiuzulu, kwani hawezi kuendelea kuwa waziri na kuheshimika kutokana na tukio hilo.
“Kama ana chembe ya uadilifu afuate nyayo za Mwinyi (Ali Hassan Mwinyi) miaka 36 iliyopita ambaye alijiuzulu uwaziri. Nchimbi hawezi kuwa waziri na kuendelea kuheshimika kama anaongoza jeshi la wauaji. Akishindwa kujiuzulu rais amfukuze kazi,” alisema.
Alieleza kuwa mauaji ya aina hiyo ni ya kisiasa na kuongeza kuwa jeshi hilo limekuwa likifanya kazi kwa niaba ya CCM.
Tendwa aibuka
Mauaji ya Daudi Mwangosi, anayedaiwa kuuawa kwa bomu na askari polisi mkoani Iringa, yamemuibua Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, ambaye ametishia kuvifuta vyama vinavyojihusisha na siasa za vurugu.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Tendwa ambaye alitumia muda mwingi kuwatisha CHADEMA pia amelionya Jeshi la Polisi na kulitaka lifanye kazi zake kwa wajibu wa sheria za nchi.
Tendwa ambaye ofisi yake imekuwa ikilalamikiwa na vyama vya upinzani kuwa inashindwa kutekeleza wajibu wake kutokana na kuegemea upande wa Chama tawala cha CCM, alisema kuwa demokrasia ya sasa imekua na kusababisha vifo vya raia wasio na hatia.
Alisema hawezi kuvumilia siasa za vurugu zinazohatarisha amani ya taifa lililopata uhuru wake miaka 50 iliyopita kwa kisingizio cha operesheni za ukombozi.
Tendwa alisema haoni haja ya CHADEMA kuendelea na operesheni yao ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) wakati huu ambao si kipindi cha uchaguzi, hivyo kutishia kukifuta chama hicho alichodai mikutano yake imekuwa ikizusha vurugu.
Aliainisha kuwa kuanzia mwaka jana hadi sasa mauaji kadhaa ya raia yametokea katika mikutano ya kisiasa katika mikoa ya Arusha, Singida, Morogoro na Iringa na kwamba hali hiyo haiwezekani kusema taifa ni huru.
Alisema kuwa Agosti 10 mwaka huu, mkutano wa vyama vya siasa na Jeshi la Polisi ulifanyika na kuzungumzia masuala mbalimbali likiwamo la amani nchini, kufanyika kwa mikutano ya vyama, wajibu wa vyama vya siasa kwa kufuata sheria za nchi na wajibu wa Jeshi la Polisi nchini.
Tendwa aliongeza kuwa kutokana na kuwapo kwa sheria ya mikutano ya vyama vya siasa nchini, ikitokea chama chochote cha siasa kitaleta chuki na uvunjifu wa amani kitapaswa kufutwa.
“Kutokana na hali tuliyoifikia kwa sasa inatisha, hivyo vyama vya siasa viondoe uchochezi,” aliongeza.
Pia amelitaka Jeshi la Polisi kutimiza wajibu wake wa kulinda raia pamoja na mali zao na kuwataka wavitumie vyombo vyao kwa ustaarabu.
DCI asuswa Iringa
Jeshi la Polisi nchini limeanza kuonja shuluba ya matukio yao kususiwa na waandishi wa habari, ambapo jana Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, DCI Robert Manumba, alikuwa wa kwanza kukumbwa na adha hiyo mkoani Iringa.
Waandishi wa habari wameazimia kutoripoti taarifa zozote za jeshi hilo hadi hapo wale waliohusika katika kusababisha kifo cha mwanahabari, Daudi Mwangosi, watakapokuwa wamekamatwa na kuchukuliwa hatua.
Manumba ambaye jana alikuwa akitaka kutoa taarifa za awali juu ya uchunguzi wa kifo cha Mwangosi, alijikuta katika wakati mgumu baada ya wanahabari hao kugoma kabisa kwenda kumsikiliza.
Pia waandishi hao wamekosoa tume iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, wakisema haijakidhi haja wala kuzingatia uwiano, kwa kile walichoeleza kuwa hakuna hata klabu moja ya waandishi wa habari iliyoshirikishwa.
Awali waandishi hao walitoa masharti kwa DCI wakitaka awepo peke yake katika chumba cha mikutano lakini Manumba alijitetea kuwa tamko alilotaka kutoa ni lazima na maofisa hao walisikie.
“Jamani punguzeni jazba juu ya hili, ninajua mna mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa hili na suala hili limemgusa kila mmoja, hasa ninyi waandishi wa habari, hivyo naomba mnisikilize na mjue tunataka kuwaambia nini,” alisema DCI Manumba bila mafanikio.
Wakati huo huo, waandishi wa habari mkoani hapa, walisema wakati tume iliyoundwa na Dk. Nchimbi haijaanza kazi yake rasmi ni vema Kamanda wa Polisi mkoani humo akaachia madaraka yake kwa muda ili kupisha uchunguzi huru.
Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa, Frank Leonard, alisema mbali na kumtaka Kamuhanda kujiuzulu pia ni wakati muafaka kwa tume iliyoundwa ikawahusisha na viongozi wa klabu ya waandishi.
TUCTA yamlilia Mwangosi
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (Tucta), limemlia aliyekuwa mwandishi wa kituo cha runinga cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi, likisema alikuwa ni mchapa kazi.
Katibu Mkuu wa Tucta, Hezron Kaaya, alisema kuwa ni jambo la kusikitisha na kushangaza kwa mwandishi kuuawa wakati akitekeleza majukumu yake.
“Kwa kweli Tucta kati ya mambo ambayo yametuuma na kutusikitisha ni kifo cha Mwangosi kinachoripotiwa kufanywa na Jeshi la Polisi, hasa kitendo cha kusambaratishwa mwili wake, kwani hata mnyama anapouawa katika mawindo huwa hauawi kwa namna ile,” alisema.
Kaaya aliongeza kuwa ni jambo la kusikitisha kwa kuwa kifo kile kitachukua muda mrefu kwa Watanzania kukisahau kwani hakuwa na kosa lolote alilolifanya mpaka kuuawa namna ile.
Aliongeza kuwa kwa hali ilivyo sasa taifa linaelekea pabaya, kwa sababu haki ya mnyonge haizingatiwi tena na wenye nguvu, akitoa mfano kuwa wanyonge wanapodai haki yao jibu rahisi ni kusambaratishwa kwa mabomu na virungu vya polisi.
Alisema endapo hali hiyo itaachwa iendelee hivyo, kunaweza kutokea maafa makubwa kwa wananchi waliochoka kuonewa na kudhulumiwa haki zao.
Kaaya alibainisha kuwa Watanzania wengi wameuawa katika matukio ya kisiasa na hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa kukomesha hali hiyo isiendelee kutokea, badala yake zinaundwa tume ambazo hata hivyo hazijulikani zinakoishia zaidi ya kutumia fedha za walala hoi.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment