Habari zilizotufikia hivi punde zinasema kuwa, Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi (pichani) wa kituo cha Televisheni cha Channel Ten amefariki dunia katika ghasia zilizozuka kati ya wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na polisi katika mkutano wa chama hicho mkoani Iringa jioni hii.
Pia askari polisi mmoja wa Wilaya ya Igowole anasemekana yuko mahututi kutokana na kipigo. Taarifa kamili kuhusiana na tukio hili zitawajia baadaye.
Inaripotiwa kuwa, kabla ya kuanza kwa vurugu hizo, viongozi wa CHADEMA na wafuasi wake walikuwa katika mkutano wa kufungua tawi la chama hicho katika kijiji hicho. Wakiwa katika eneo la tukio, Polisi walifika katika tawi hilo na kuwataka wafuasi wa chama hicho kutawanyika kwa kuwa mikutano ya vyama vya siasa imepigwa marufuku kupisha kazi ya Sensa ya Watu na Makazi ambayo imeongezewa siku saba baada ya muda wake wa awali kukamilika.
Kutokana na amri hiyo, wafuasi hao walikataa kutawanyika na kuwalazimu polisi kutumia mabomu ya machozi kwa nia ya kuwatawanya. Wakati wakipiga mabomu hayo, inadaiwa mwandishi mmoja wa habari, aliwafuata polisi na kuhoji sababu za kutumia nguvu hiyo kutawanya wananchi. Ndipo mwandishi huyo alikamatwa na kusababisha Mwangosi kwenda kujaribu kumnasua mwandishi mwenzake kutoka mikononi mwa polisi. Polisi walimsihi Mwangosi aondoke katika eneo hilo ili waendelee na kazi yao na alipokaidi, walimkamata na yeye. Wakati Mwangosi akiwa amezungukwa na askari polisi wanaokaribia watano, kulisikika mlio wa mlipuko na baadae Mwangosi na mmoja wa askari aliyekuwa amemshika walianguka chini. -- Kutoka kwenye blogu ya Ziro na Tina
No comments:
Post a Comment