Sunday, September 23, 2012

M4C yaitesa CCM


MIKUTANO ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) inayofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wilayani Geita, ikiongozwa na aliyekuwa diwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata ya Sombetini mkoani Arusha kabla ya kujiuzulu na kutimkia CHADEMA, Alphonce Mawazo, imezoa makada 308 wa CCM na CUF.
Makada hao ni wa vijiji vya Bukondo, Kaduda na Katoro wilayani humo ambapo kati ya hao 100 ni wanachama wapya.
Ukiacha wanachama wengine, baadhi ya makada maarufu waliotimkia CHADEMA kutoka CCM ni Isaac Tanzania, Sami Luhemeja, Linda Maduka, Mussa James, Luhamba Butama, Emmanuel Joseph, kada wa CUF, Emmanuel Mhongo pamoja na Lugwisha Elias, ambaye kwa hasira aliamua ‘kusilimisha’ familia yake yote wakiwamo wake zake wawili.
Kwa mjibu wa makada hao na wananchi wengine, sababu za kutimkia CHADEMA, walisema ni kutokana na serikali ya CCM kukithiri kwa ufisadi, hali ambayo imesababisha washindwe kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa kipato cha chini.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Kaduda muda mfupi baada ya viongozi wa CHADEMA kumtoa kizuizini katika ofisi ya mtendaji wa kijiji alikokuwa akishikiliwa kwa kosa la kualika watu kwa kupiga mbiu wahudhurie kwenye mkutano wa CHADEMA, Lugwisha alisema ameamua kujiunga na chama hicho yeye na wake zake baada ya kuchoshwa na manyanyaso ya mtendaji wa kijiji hicho, Fundi Makanza, aliyedai ni ‘Mungu mtu’ na ameigeuza ofisi yake kuwa mahakama.
“Nimeona nihamie huku maana pamoja na kuwa kada mzuri wa CCM sioni mabadiliko yoyote zaidi ya manyanyaso ya kila siku tunayofanyiwa na mtendaji Makanza, ambaye tunaona hana nia nzuri na wananchi wake…ukifikishwa ofisini kwake ni kama umefikishwa mahakamani… yeye huyohuyo ni mtendaji, polisi na mahakama, kwa hali hiyo unawezaje kuipenda CCM na kuendelea kubaki huko?” alilalama Elias huku akishangiliwa.
Kwa upande wake kiongozi wa M4C kutoka makao makuu Dar es Salaam, Mawazo, aliwataka wananchi kuachana na CCM, kwani kwa miaka yote imeshindwa kuwaletea maendeleo na badala yake wachukue hatua ili kuiondoa madarakani leo na si kesho, vinginevyo vizazi vijavyo vitakuta mashimo kutokana na spidi waliyonayo ya kuiuza nchi.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment