CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, akamatwe kwa sababu anawalazimisha kuvunja sheria.
Akisisitiza kukamatwa kwa msajili huyo, Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi wa CHADEMA, Anthony Komu, alisema kauli ya Tendwa kuwataka wasusie ruzuku ni ukiukwaji wa sheria utakaowanyima haki wafuasi wa chama hicho kufanya shughuli za kuijenga CHADEMA.
Akizungumza kwa njia ya simu na Tanzania Daima Jumapili, Komu alisema Tendwa hana busara, hali iliyomfanya kushindwa kutimiza wajibu wake wa kuwa mlezi wa vyama vya siasa.
Kwa mujibu wa Komu, msajili huyo hana uwezo wa kukifuta chama hicho licha ya vitisho alivyopata kuvitoa kupitia vyombo vya habari huku akisisitiza kwamba CHADEMA imesusa kufanya kazi na Tendwa si kupokea ruzuku.
“Sisi tumesema Tendwa ameshindwa kutimiza wajibu wake ndiyo maana tumesusa kufanyakazi naye lakini hili la ruzuku ni haki yetu, tena ni matakwa ya sheria, kwa nini anatuambia tususie?
“Huyu anatakiwa kukamatwa kwa sababu anatuambia tuvunje sheria… lakini pia hana mamlaka ya kutufuta wala kuzuia ruzuku yetu tunayoipata kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
“Tulishamweleza kwamba tunapokea pesa kutoka Uholanzi ambako na CCM nao wanapewa tena nyingi kuliko zetu, hivyo kumweleza namna Nape alivyotuchafua kwamba tunapokea pesa chafu lakini hakuchukua hatua zozote,” alisema Komu.
Jana vyombo mbalimbali vya habari vilimkariri Tendwa akiwataka viongozi wa CHADEMA waliosuasia kufanya kazi pamoja naye kuikataa ruzuku wanayopata ambayo hupitia ofisini kwake.
“Kama hawamtaki yule mtoa ruzuku, je, watakuja kuidai? Sina tatizo na kususiwa lakini nisusiwe kwa haki…kususia maana yake hutimizi wajibu, sheria, haki na Katiba ya nchi.
“Lazima tutambue mamlaka zilizopo…hivi wao wakichukua serikali na wengine wawasusie?” alikaririwa Tendwa alipozungumza na waandishi wa habari juzi wakati wa kongamano la kujadili umuhimu wa amani, usalama na wajibu wa Jeshi la Polisi kwa vyama vya siasa.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment