Thursday, September 13, 2012

CHADEMA yafungua kesi mahakamani dhidi ya Nape; Yazungumzia inakopata ufadhili

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimekiri kufadhiliwa kutoka nje ya nchi katika shughuli zake za kujijengea uwezo.

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa alisema hayo jana katika semina iliyoshirikisha baadhi ya viongozi wa chama hicho na wageni kutoka shirika la Chama cha Kikristo cha Ujerumani (CDU) la Konrad Adenauer Stiftung (KAS).

Kwa mujibu wa Dkt. Slaa, CHADEMA na KAS, wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa miaka sita sasa na ushirikiano huo umelenga zaidi kukuza demokrasia nchini.

Dkt. Slaa alidai kuwa CHADEMA ni chama chenye uwazi kwa kila mtu na katika uhusiano wao na KAS, hakiletewi fedha moja kwa moja kwa ajili ya operesheni au maandamano, ila kujijenga kiuwezo.

“Kwa sasa kumekuwa na propaganda zinazoenezwa kwamba CHADEMA wanapata mabilioni ya fedha kutoka kwa wafadhili, hii si kweli, ila wanatujengea uwezo na si kutufadhili kampeni. Napenda kusema propaganda za aina hii zimepitwa na wakati na wote watakaozifanya tutawafungulia kesi,” alisema Dkt. Slaa.

“Wanaosema kwamba CHADEMA wanapokea mabilioni nao wanashirikiana na mashirika ya aina hiyo yenye mrengo mmoja na ni utamaduni duniani kote, vyama vyenye mrengo mmoja kushirikiana, hivyo hii dhana isipotoshwe,” alidai.

Pamoja na kusema kuwa KAS haitoi fedha moja kwa moja kwa CHADEMA kwa ajili ya maandamano na kampeni, lakini Dkt. Slaa alidai kuwa shirika hilo huwasaidia wastani wa Sh milioni 60 kwa mwaka kwa ajili ya machapisho na kutoa elimu.

Pia alisema kipo chama cha Uholanzi ambacho hakukitaja jina, lakini akakiri kuwa huwafadhili Sh milioni 20 kulingana na idadi ya wabunge walio bungeni.

Pamoja na kusema kuwa ni kawaida kwa vyama vya mrengo mmoja kusaidiana duniani, Dkt. Slaa alisema chama hicho cha Uholanzi kinachowasaidia, pia hufadhili CCM fedha zaidi ya zinazopelekwa CHADEMA kutokana na chama hicho tawala kuwa na idadi kubwa ya wabunge.

Nape ashitakiwa 

Dkt. Slaa alidai kwamba kwa kuanzia wameamua kumshitaki Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye. 

Kwa mujibu wa madai ya Dkt. Slaa, tayari CHADEMA imefungua kesi namba 186 ya mwaka 2012, katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam dhidi Nape, ambaye anadaiwa alitamka CHADEMA kufadhiliwa kutoka nje.

Dkt. Slaa alisema kuwa, kesi hiyo yenye tuhuma zaidi ya tano, pia itawaunganisha watu wengine waliowahi kutamka kauli za namna hiyo vikiwamo vyombo vya habari vilivyoandika taarifa hiyo.

“CHADEMA tumeamua kumfikisha Nape mahakamani, ili atuthibitishie hayo mamilioni tunayopokea kwa wafadhili wa Ujerumani na kesi hii, itawaunganisha na wale waliowahi kusema kauli kama hiyo. Hapa mnaona kuna wageni, hawa ni viongozi kutoka Ujerumani na baadhi yao ni watumishi wa Serikali ya nchi hiyo, sasa tumekutana hapa kwa makusudi, ili kuwaeleza wazi jinsi wenzetu wanavyosema kutokana na ushirikiano wetu na wao. Tunashangaa sana, yaani CHADEMA ikishirikiana na watu kutoka nje ya nchi wanasema na kuzusha mambo ambayo yanaweza kuleta utengano kati ya nchi na taifa jingine. Kwa mfano, sisi CHADEMA tunashirikiana na Taasisi ya Korrad Adenauer Stiftung ya Ujerumani, CCM inashirikiana na FES, CUF inashirikiana na FNF zote za Ujerumani, sasa tunataka Nape atueleze mbele ya Mahakama juu ya jambo hili,” alisema Dkt. Slaa. 

Dkt. Slaa alidai kuwa kesi hiyo itakapokuwa ikiendelea, wataongeza watu wengine walioeneza kauli hiyo.

Semina ya KAS 

Akizungumzia semina ya kujenga uwezo iliyotolewa jana kwa makada wa CHADEMA, Dkt. Slaa alisema imelenga kuangalia wanavyoweza kuleta uchumi wa soko utakaoshirikisha watu walio katika ngazi za juu na chini.

Lengo la kushirikisha watu hao wa tabaka mbalimbali kwa mujibu wa Dkt. Slaa, ni ili raslimali za nchi zitumike kwa faida ya Watanzania wote ambapo pia mgeni kutoka KAS ambaye alipata kuwa Naibu Waziri wa Uchumi na Maendeleo wa Ujerumani, Klaus-Jurgen Hedrich atatoa mada.

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alisema ili uchumi uwe endelevu, lazima wananchi wapewe haki na kuruhusu sekta binafsi kusimamia uchumi na si rahisi kusimamia uchumi kwa sera za kijamaa.

Mbowe pia alisema lengo la kukutana na mawaziri na wabunge wa Ujerumani jana ni kujadili masuala ya uchumi duniani na mahitaji yake katika nchi mbalimbali. Akasema chama cha siasa kinapaswa kutimiza majukumu yake, lakini pia kinapaswa kutambua kina wajibu wa kujadili uchumi wa taifa lake pamoja na utamaduni wa asili.

“Leo tumekutana na viongozi kutoka Ujerumani kubadilishana uwezo wa kisiasa, kujifunza kutengeneza vitabu, Katiba na mafunzo kwa viongozi. Lakini, nimetumia nafasi hii kuwaeleza hili la CCM na Serikali yake kutoa tuhuma kutufadhili jambo ambalo watalifanyia kazi kadiri watakavyoona. Pia tumewaeleza kwamba, Serikali hii inapokwenda kuomba msaada katika mataifa makubwa inasema inatekeleza sera na uchumi wa soko, lakini wanaporudi nyumbani wanawaeleza wananchi kuwa wanatekeleza ujamaa na kujitegemea jambo ambalo ni uongo. Sisi CHADEMA tupo pande zote, tunachagua yaliyo mazuri katika pande hizo na kuyafanyia kazi ili kuendana na soko huru, kuna misingi ambayo wakipewa watu binafsi wanaweza kusimamia uchumi, lakini hiyo isiondoe wajibu wa Serikali kutekeleza wajibu wake kwa wananchi,” alisema. 

Naye aliyekuwa Mbunge na Waziri wa Uchumi na Maendeleo katika Serikali ya Ujerumani, Klaus-Jurgen Hedrich, alisema maendeleo ya nchi yoyote hayaji kama hakuna uhuru wa kutoa maoni na uhuru wakujitawala.

Alisema kwamba, ili wananchi wapate maendeleo ni lazima Serikali itoe fursa sawa ya kuwasikiliza wanachodai na kwamba, Tanzania inasifika kwa amani na utulivu lakini anashangaa kuwapo na malalamiko,” alisema.

Katika mazungumzo yake, alionyesha kutoridhishwa na kifo cha Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Channel ten, Marehemu Daudi Mwangosi, aliyeuawa Iringa wakati akitekeleza wajibu wake. 


Wavuti

No comments:

Post a Comment