Saturday, September 29, 2012

Chadema chakanusha kuwafanyia fujo CUF


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekanusha kuwatuma wafuasi wake kuwafanyia vurugu wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) na kutoa pole kwa wahanga wa tukio hilo.

Aidha kimelaani kauli iliyotolewa na Naibu  Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na haki za binadamu, Abdul Kambaya, kwa kudai kuwa ni ya vitisho na haiwezi kutolewa na kichwa cha mtu anayefikiri vizuri.

Katibu wa Chadema, Amani Golugwa, alisema hayo wakati akitoa tamko la kukanusha shutuma za chama cha CUF, kufanyiwa vurugu na Chadema.

Alisema kuwa kimsingi  mfuasi wao alijichanganya kwenye vurugu zilitokea eneo la Kilombero, wakati wafanyabiashara ndogo ndogo wakigawana maeneo ya kufanyia biashara zao, baada ya eneo la awali la NMC kutowatosha.

“Chadema tunakanusha kuhusika na jambo hili na hii si tabia ya Chadema na kamwe haiwezi kuwa tabia yetu kufanya siasa chafu za namna hii, sisi tunajali amani, upendo na hivi ndiyo makuzi yetu,”alisema.

Aidha, Golugwa alisema chama kinawakaribisha watu wote na vyama vyote kuendesha shughuli za siasa safi na kikubwa wazingatie demokrasia vizuri, ili kuleta matumaini kwa watanzania.

Alisema chama hakiwezi kuzuia chama chochote kwa sababu za kisiasa, ila wanaamini wananchi watachagua wenyewe chema na kibaya.

Pia aliwataka wananchi kupuuza maneno yaliyotolewa na chama cha CUF ambayo aliyanukuu “Uwezo wa kuwafanya tutakavyo tunao na kwa sababu wameanza tunaweza kumaliza,”  na kudai kuwa wao hawataki kufikishana
huko na hawana historia ya vurugu.

Golugwa pia alionya wanaopandikizwa ndani ya chama hicho kwa lengo la kuleta vurugu na kudai wakiwabaini watachukulia hatua stahiki.

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema Taifa, Godbless Lema, alisema chama kimegundua mikakati ya siri inayofanywa na viongozi wa serikali ya kutaka kuzuia chama hicho, kuendelea na mikutano ya vuguvugu la mabadiliko (M4C) na kutaka kumtumia msajili wa vyama vya siasa kuzuia mikutano ya siasa.

Aliwasihi wafuasi wasio na uvumilivu wa kuona viongozi wa Chadema wakitukanwa kwenye mikutano yao, kuacha kuhudhuria mikutano ya vyama vya siasa vingine, ili kuepusha vurugu.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment