Friday, September 28, 2012

Chadema, CCM kusuka au kunyoa leo

Ni vita ya uchaguzi wa Meya Mwanza
Dk. Slaa atua, ateta na madiwani wake

KIVUMBI cha kumpata Meya wa Jiji la Mwanza na naibu wake, kinatarajiwa kutimka leo. Uchaguzi huo, ambao unaonekana kuvutia hisia za wananchi wa Jiji hilo, unatarajiwa kuwa na mvutano mkubwa kati ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Uchaguzi huo, unafanyika baada ya kugawanywa Jiji la Mwanza, ambako kuanzia sasa kutakuwa na Manispaa ya Ilemela na Nyamagana.

Akizungumza na MTANZANIA mjini hapa jana, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe, alisema hadi jana majina ya madiwani waliokuwa wameteuliwa yalikuwa yamewasilishwa ofisini kwake.

Alisema maandalizi yote ya uchaguzi huo, yamekamilika na kuvitaka vyama vyote vilivyoteua wagombea kutimiza wajibu wa kanuni za halmashauri.

“Ni matumaini yangu, kuwa uchaguzi huu utafanyika katika mazingira ya amani na utulivu mkubwa,” alisema Kabwe.

Katika uchaguzi huo, CCM imemsimamisha Diwani wa Kata ya Mkolani, Stanslaus Mabula, kuwania nafasi ya Meya wa Jiji la Mwanza, huku Diwani wa Kata ya Igogo, John Minya, akiteuliwa kuwania nafasi ya Naibu Meya.

Katika Manispaa ya Ilemela, chama hicho kimemsimamisha Diwani wa Kata ya Sangabuye, John Maluga, kuwania nafasi ya Meya, na Sarah Ng’hwani kuwania unaibu.

Kwa upande wake, CHADEMA kimemsimamisha Charles Chinchibella, aliyekuwa Naibu Meya kipindi kilichopita kuwania umeya wa Jiji.

Lakini, chama hicho kimeacha wazi nafasi ya naibu meya ili kutafuta nafasi ya kuungwa mkono na Chama cha Wananchi (CUF), ambacho kimemsimamisha Diwani wa Kata ya Mirongo, Daud Mkama, kuwania nafasi hiyo.

Kwa upande wa Manispaa ya Ilemela, CHADEMA kimemsimamisha Abubakar Kapera kuwania nafasi ya Meya na Dan Kahungu anajitosa kwenye umeya.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa, juzi aliwasili Mwanza kimya kimya kwa ajili ya kumaliza mgogoro unaoendelea kufukuta.

Kabla ya kuwasili kwa Dk. Slaa, chama hicho kilimtuma Mkurugenzi wa Oganaizesheni na mafunzo, Benson Kigaila, kwenda kutatua mgogoro huo, lakini mambo yalionekana kuwa magumu.

Baada ya kuwasili, alifikia katika Hoteli ya Midland, iliyopo katikati ya Jiji la Mwanza na kutwa nzima ya jana alikuwa na vikao mfululizo na madiwani na Wajumbe wa Kamati Tendaji za Wilaya za Ilemela na Nyamagana katika Hoteli ya G & G.

Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho, zilieleza kuwa Dk. Slaa aliamua kufika mwenyewe, baada ya kuelezwa hali ya mambo ni mbaya kutokana na maamuzi ya Kamati Kuu kuwafuta wagombea waliokuwa wameshinda katika nafasi za umeya na naibu meya katika Manispaa ya Ilemela.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Kamati Tendaji ya chama hicho, Wilaya ya Ilemela, iliwateua Marietha Chenyenge kugombea umeya na Rosemary Brown nafasi ya naibu meya katika Manispaa ya Ilemela.

Licha ya matokeo kutangazwa, Mbunge wa Ilemela, Highnes Kiwia (CHADEMA), alitishia kujiuzulu nafasi ya ubunge endapo majina ya madiwani hao yangelithibitishwa na makao makuu, ambapo kutokana na shinikizo hilo, waliamua kutengua matokeo hayo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho, Dk. Slaa aliwaambia madiwani walioenguliwa kuwa chama kiko tayari kuwapatia kiapo cha utii chini ya wanasheria wao.

"Dk. Slaa, alikuwa mkali kwa madiwani hao, aliwaambia maamuzi ya Kamati Kuu yanapaswa kuheshimiwa," kilisema chanzo chetu.


Mtanzania

No comments:

Post a Comment