Wananchi wa kata ya Hembeti Jimbo la Mvomero mkoani Morogoro, juzi walizua kizazaa baada kuzuia gari la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kuendelea na safari wakimtaka ahutubie mkutano wa hadhara uliokuwa ukihutubiwa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Hamad Yusuph.
Mbowe, aliyekuwa akitoka mkoani Dodoma baada ya kumaliza vikao vya Bunge, kiwa anaelekea katika kata ya Mtibwa kwenye mwendelezo wa operesheni vuguvugu la mabadiliko( M4C), alipofika katika kata ya Hembeti, gafla wananchi walimsimamisha wakitaka naye awahutubie kabla ya kuondoka.
Kitendo hicho kilimfanya mmoja wa makada waliokuwapo mkutanoni hapo, Arcado Ntagazwa, kumpa kipaza sauti ili asalimie umati huo.
Akizungumza na wananchi hao baada ya kupewa kipaza sauti, Mbowe alisema dhamira ya Chadema kuwa mkoani Morogoro ni kuwaondoa katika wimbi la usingizi wa kuishabikia Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Alisema hivi sasa Serikali inayoongozwa na CCM imeshindwa kutatua matatizo ya msingi ya nchi na kusababisha wananchi kuendelea kuishi katika hali ya umaskini wakati nchi imebarikiwa na Mwenyezi Mungu kuwa na rasilimali nyingi.
“Tunakwenda kila kata ya mkoa wa Morogoro kujenga mtandao wa chama bila kujali dini, kabila wala rangi. Ujumbe wangu kwa wana-Hembeti ni kujua wajibu wa chama cha siasa ni kupata viongozi na sera mbadala zitakazowezesha nchi kusonga mbele,” alisema Mbowe.
Alieleza kuwa Serikali ya CCM imeshindwa kuwaondolea wananchi matatizo mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa huduma za afya, maji pamoja kuboresha hali ya kilimo ili kuwapeleka katika neema katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru huku akiwataka wakazi wa Hembeti kujitafakari kwa kina chama hicho kimewafikisha wapi.
Alisema mkoa wa Morogoro umefunga ndoa na CCM, hali inayowafanya wasiwe na sauti ya moja kwa moja huku matatizo yao yakiongelewe na wabunge wa vyama vya upinzani kutoka maeneo mengine.
“Ninyi mmefunga ndoa isiyo na faida na CCM kwani mna matatizo mengi sana ikiwemo ya kilimo, lakini waliowaoa hawawasemei kule bungeni badala yake wabunge wa Chadema kutoka sehemu nyingine, ndiyo wanawasemea. Sasa tumekuja kuwaunganisha na wengine katika kuikomboa Tanzania," alisema Mbowe.
Alisema ni makosa makubwa kwa wananchi kufikiria kuwa CCM ndiyo baba yao au mama yao na kuwataka wainyime kura katika uchaguzi mbalimbali na kuiweka Chadema na kwamba kama Chadema kitashindwa kusimamia maslahi ya wananchi, nacho kiwekwe pembeni.
“Hata mimi Mbowe kesho nikiona Chadema haiendani na mahitaji ya wananchi katika kuwaondoa kwenye umaskini, sitakuwa na sababu ya kuendelea kuwa mwana-Chadema, nitatoka, ninyi mnang’anga’nia CCM, kwani ni baba yenu au mama yenu?,” Alihoji Mbowe huku akishangiliwa na wananchi hao.
Kwa upande wake, Ntagazwa aliyewahi kushika nafasi nyingi serikalini, alisema yeye ni mfano tosha kwa wananchi hao baada kutoka CCM kutokana na sera mbaya za kushindwa kuwasaidia wananchi na kuamua kujiunga na Chadema.
“Mimi nilishakuwa Naibu Waziri wa Fedha na Waziri wa Mazingira katika Serikali ya CCM, lakini nimeamua kutoka na kuingia Chadema baada ya kuona hakuna mikakati ya kusaidia wananchi hasa ninyi wa vijijini. Hivyo mnangoja nini, jiungeni na Chadema tuing'oe CCM madarakani,” alisema Ntagazwa.
Awali, akiwa katika vijiji vya Kambala Hembeti na Mkindo kunakokaliwa na jamii ya wafugaji na wakulima, alisema migogoro ya ardhi nchi inakuzwa makusudi na watawala kwa kuwa wana maslahi nayo.
Alisema watendaji na watawala wa Serikali ya CCM badala ya kuwakutanisha wakulima na wafugaji kuondoa tofauti zao, wao hutumia fursa hiyo kuchukua fedha kwa mmoja wao na kisha kuacha
uhasama miongoni mwa wafugaji na wakulima.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Hamad Yusuph, alisema sababu ya serikali kushindwa kutataua matatizo ya wakulima na wafugaji ipo siku nchi itaingia kwenye machafuko.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, amejikuta akidondosha machozi mbele ya hadhara baada kuelezwa namna ambavyo wake na mabinti za wanaume wafugaji wanavyokamatwa kisha kupelekwa rumande na kutendewa vitendo vibaya ikiwa ni sehemu ya chanzo cha mapato.
Dk. Slaa alitoa machozi hayo wakati akizungumza na wafugaji katika vijiji mbalimbali vya kata ya Msowero na Dumila wilaya ya Kilosa na Gairo ikiwa ni sehemu ya mikutano ya Operesheni Sangara-M4C inayoendelea katika maeneo mbalimbali mkoani Morogoro.
Akiwa katika Kijiji cha Msowero, Dk. Slaa alidondosha machozi baada ya mfugaji mmoja kusimulia namna ambavyo wake na mabinti zao wanavyokamatwa kisha kupelekwa rumande na kufanyiwa vitendo vibaya, ambavyo alisema haviwezi kusimulika ili kuwa chambo kwa waume au baba zao watoe fedha kwa wakamataji hao.
Alisema vitendo hivyo vinafanywa na baadhi ya askari wasiokuwa waaminifu, wakishirikiana na mgambo na viongozi wa serikali za vijiji katika maeneo mbalimbali ya wafugaji.
Akizungumzia vitendo hivyo, Dk. Slaa alisema Serikali inastahili kubeba lawama zote kwa sababu imeamua kufumbia macho tatizo la wafugaji na wakulima kugombana.
“Jana nikiwa Kilosa pale mjini, nilifuatwa na kiongozi mmoja wa wafugaji, na kunieleza vitendo hivyo vinavyofanywa na hao waliotajwa. Hii ni nchi gani sasa kama wafugaji nao wanakosa haki zao na kufanyiwa unyama?, Alihoji Dk. Slaa.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwataka wafugaji kukiunga mkono Chadema ili kiwatetee na kuondokana na unyanyasaji huo.
Nipashe
ARUTA KONTUNUA, MAPAMBANO YAENDELEE MPAKA DOLA ISIKWE NA CHADEMA. WALA MSIOGOPE USHINDE NI WA KWENU KAZA UZI, NENDA KILA KIJIJI,MTAA, TANZANIA NZIMA. MWANZO NI MZURI
ReplyDelete