Friday, August 31, 2012

Ujumbe wa Freeman Mbowe wabadili wengi Houston

Mwenyekiti wa Taifa Chadema Bwana Freeman Mbowe akiwa ameongozana na Mbunge wa mbeya mjini bwana Joseph Mbilinyi (Sugu) wametembelea jiji la Houston Texas USA kuanzia tarehe 24 hadi 26 August. Ujio huu ni mwaliko wa Tawi la Chadema Houston TX .

Tawi la Chadema Houston linaonekana kuwa tishio kwa uhai wa CCM sio Houston pekee bali USA. Wanachadema wa Houston ambao ni wengi wanaojiamini, wenye malengo na nia ya dhati kuikomboa Tanzania kisiasa, kiuchumi na kijamii wamekuwa mstari wa mbele kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya kiuchumi nchini Tanzania kwa kushiriki moja kwa moja.

Ujio huu wa Mbowe ambao uliingiza wanachama wapya zaidi ya 100 kwenye idadi ya wanachadema wa Houston, ulifana sana. Mkutano huu uliofanyika kwenye hotel ya Marriot Westchase Houston TX ulifanyika kwa utulivu na furaha kubwa sana.

Mkutano huu ulihudhuriwa na watanzania wengi na kuvunja rekodi ya mkutano wowote wa kisiasa ambao umewahi kufanyika Houston TX kwa historia ya uwepo wa Watanzania jijini hapa.

Mwenyekiti Mbowe akiwa anajiamni aliweza kuwafanya Watanzania kutokwa na machozi kwa jinsi alivyokuwa akielezea ugumu wa maisha, ubovu wa elimu, afya, barabara nk waliyonayo/walivyonavyo watanzania kila siku. Mwenyekiti aliwaasa watanzania kuacha kulalamika badala yake kuwa chanzo cha ufumbuzi kwa kushirikiana na Chadema.

Mwenyekiti aliwaambia Watanzania hawa kuwa Chadema inawahitaji Diaspora kwa uwingi wao ili kupeleka nchini ujuzi wao, elimu, utamaduni wa kuwajibika, kuaminiwa, na kila chema walichojifunza kutoka nje. Bwana Mbowe aliwahakikishia watanzania kuwa chadema kinaingia ikulu mwaka 2015 kwani kinafanya na kimefanya maandalizi ya kutosha.

Wakiwa na hamu ya kushiriki moja kwa moja kusaidia mabadiliko haya ya kisiasa na kiuchumi Tawi la Chadema Houston liliahidi kutoa pikipiki mia ishirini na sita (126), gari la kampeni na vifaa mbali mbali vya computer utaalamu na wataalamu wake kutumika katika njanja mbali mbali ili kusaidia chama na watanzania kwa ujumla.

Mbunge wa Mbeya Joseph Mbilinyi kwa upande wake alisema, Chadema inawataka na kuwahitaji sana, inawathamini sana diaspora na wakazi wa Houston kama watanzania wote ndio maana imewafuata. Alisema, Chadema hakitaki kumwacha mtu yeyote nyuma kwenye kujenga nchi hususani pale itakapochukua dola 2015.

Akiongea kwa kujiamini Sugu alisema anajua kazi kubwa iliyofanywa na watanzania na sasa walioko nje nao wanaletewa neno la ukombozi kwa ajili ya nchi yetu.

Naye Mwenyekiti wa Tawi Bwana Fue Fue akiongea na wananchi aliwaasa kuwa wasiwe waoga kwani makamanda wa Chadema wamepitia mengi ila bado wanasonga mbele. Aliwaambia watanzania wenzake kuwa hakuna wa kuisaidia Tanzania isipokuwa Watanzania wenyewe. Alisisitiza ujasiri, kujiamini na kufanya kwa vitendo. Akiongea kwa msisitizo alisema uongozi ulioshindwa hauwezi tena kuaminiwa, kwa miaka 50 sasa serikali ya CCM imeshindwa na imeishiwa ubunifu hivyo kuwa na ugumu wa kuweza hata kutambua matatizo halisi ya Mtanzania. Lazima kubadili uongozi mzima ili kuweza kusonga mbele kiuchumi, ni kazi yetu kufanya hivyo na wajibu wetu kuindoa CCM madarakani, alisema bwana Fue Fue

Mbowe aliwaaga watanzania kwa kuwaambia Chama kina wahitaji na kinathamini sana mchango wao.

Watanzania wengi walimsifia Mbowe kwa uwezo wake wa kuongea kujenga hoja na kujibu maswali ya Watanzania na kumaliza kiu yao. Mkutano huo ulichukua takribani masaa manne.

Majibu ya watanzania ni kuwa wengi wamehamasika na kukubali kushiriki moja kwa moja kwenye kuikomboa nchi.

No comments:

Post a Comment