Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (SACP), Michael Kamuhanda, amesema hawatakuwa na sababu ya kuzuia mikutano ya CHADEMA baada ya shughuli za sensa kumalizika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamuhanda alisema tangu siku ya kwanza CHADEMA walipoingia mkoani humo hali ya utulivu ilikuwa ni nzuri na hakukuwa na matatizo yoyote mabaya waliyosababisha.
“Tunajua watafanya mkutano wao Septemba 2, mwaka huu, wilayani Mufindi, hatuna sababu ya kuzuia hilo labda ijitokeza sababu ya kiusalama, kwa kuwa hata Dk. Slaa nimezungumza naye na akaniambia wako salama na amefurahia walivyopokewa kifalme katika mkoa huu,” alisema Kamuhanda.
Akizungumzia sababu ya kuimarisha ulinzi, Kamanda Kamuhanda alisema hatua hiyo inatokana na hali halisi ya kisiasa kwa sasa na kwamba polisi wana wajibu wa kuchukua tahadhari kuhakikisha usalama unakuwepo.
Alipoulizwa kama jeshi hilo linatumiwa na viongozi wa CCM katika kuhakikisha mikutano ya CHADEMA haifanikiwi, Kamuhanda alisema si kweli kwani hata baadhi ya viongozi wa CCM wakiwamo wabunge wa mkoa huo hajawahi kukutana nao.
Tangu kuingia kwa viongozi kadhaa wa CHADEMA mkoani Iringa, jeshi hilo limekuwa katika tahadhari kubwa kwa hofu kuwa wanaweza kufanya mikutano kabla ya sensa ya watu na makazi kumalizika.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment