WAKATI Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, ikisema kuwa hakuna rushwa kwenye kashfa ya ununuzi wa rada kutoka nchini Uingereza, nchi hiyo imeweka bayana kwamba uamuzi wake hauizuii Tanzania kuwapeleka mahakamani na kuwashitaki watuhumiwa wa ufisadi wa sakata hilo.
Msimamo wa Uingereza unakuja siku chache baada ya Rais Kikwete na mawaziri wake, Benard Membe wa Mambo ya Nje na Mathias Chikawe wa Utawala Bora, kudai kuwa serikali hiyo iliyokuwa ikichunguza kashfa hiyo imebaini kuwa hakukuwa na rushwa katika ununuzi wa rada.
Hata hivyo, katika tamko lake la Agosti 6 mwaka huu, Uingereza kupitia ubalozi wake nchini, iliweka bayana kuwa bado iko pamoja na Serikali ya Tanzania katika kusaidia mapambano dhidi ya ufisadi.
“Serikali ya Uingereza daima imekuwa wazi kuwa itashirikiana na mamlaka za Tanzania katika uchunguzi na kuwashtaki kwa kutumia sheria za Tanzania wale wote waliohusika katika ufisadi wa rada ya BAE System,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Kwamba Ubalozi wa Uingereza nchini unajua kuwa vyombo vya habari vimelikomalia suala la rada juu ya kama kuna uwezekano wa kuchukua hatua za kisheria kuhusiana na sakata zima.
“Serikali ya Uingereza inapenda kuweka wazi kuwa mapatano kati ya Ofisi ya Uingereza inayoshughulika na Ufisadi Mkubwa (SFO) kwa upande mmoja na BAE System kwa upande mwingine, hayana nguvu za kisheria katika nchi zingine, na kwa maana hiyo hayaizuii Serikali ya Tanzania kuwapeleka mahakamani na kuwashitaki wanaotuhumiwa na ufisadi huo,” ilisema.
Kwamba ripoti ya Kamati ya Bunge la Uingereza inayoshughulikia Maendeleo ya Kidunia (IDC) kuhusu ufuatiliaji wa jinai ya wizi wa fedha ya Novemba 15, 2011, iliunga mkono wazo la Serikali ya Tanzania la kutaka kuwapeleka mahakamani watu wote waliojihusisha na wizi unaohusiana na manunuzi ya kifisadi ya rada.
Vilevile, IDC inaona kuwa ni jambo jema kuwapa cha mtema kuni watu wote wanaojihusisha na wizi wa mamilioni ya fedha za umma.
Kwa mantiki hiyo, Uingereza inaendelea kuahidi kuwa kila wakati itakuwa tayari kufanya kazi bega kwa bega na Serikali ya Tanzania katika kupambana na ufisadi kwa ujumla wake.
Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge (CCM), kwa muda mrefu amekuwa akitajwa ndani na nje ya chama chake kuhusika na kashfa ya ununuzi wa rada kutoka Kampuni ya BAE System.
Chenge, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, anatajwa kuhusika kutoa ushauri wa kisheria wakati huo akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ushauri ambao unatajwa kuzingatiwa katika hatua za uamuzi.
Mwingine anayehusishwa na kashfa hiyo ni aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT) Dk. Idriss Rashid.
Pamoja na hao, wanatajwa wafanyabiashara wenye asili ya India, lakini ambao wanaishi/walipata kuishi Tanzania, Tanil Somaiya, ambaye alikuwa akimiliki kampuni ya uwakala wa simu ya Shivacom na Sailesh (Shailesh) Vithlani kuwa watu wa kati wa biashara hiyo.
“Kama Uingereza waliochunguza kashfa hiyo wamefika mahala wanasema kulikuwa na makosa ya uchapaji tu, mtu wenu mnamfikisha mahakamani kwa ushahidi upi?” alihoji Rais Kikwete wakati akizungumza na wahahariri wa vyombo vya habari hivi karibuni.
Mchakato wa ununuzi wa rada iliyoligharimu taifa dola milioni 46, unatajwa kuanzia kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair kuwa ndiye aliyemshawishi aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo, Benjamin Mkapa, kununua rada hiyo kutoka Kampuni ya BAE-Systems.
Wakati huo aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa, Clare Short, alikataa katakata Tanzania, moja kati ya nchi masikini kabisa duniani, kutumia kiasi hicho kununua rada.
Hata hivyo, chenji hiyo ya rada, zaidi ya sh bilioni 75 zimerejeshwa nchini baada ya hati ya makubaliano baina ya pande zinazohusika kusainiwa.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment