Endapo mpango huo utafanikiwa unalenga pia kupambana na makundi ya kifisadi ndani ya chama hicho ukiunda safu mpya ndani ya chama kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa vya habari, ingawa CCM inachagua viongozi wake kwa kuzingatia kanuni na taratibu zake, lakini inaelezwa kuwa, kasi na mikakati ya CHADEMA kwa namna fulani ni kati ya vigezo vinavyotumika kujenga hoja, pamoja na mambo mengine, dhidi ya mtandao wa mafisadi ndani ya CCM.
Lakini wakati vigezo kadhaa vikitumika kwa chama hicho kikongwe kujinusuru angalau na taswira chafu mbele ya umma, mtandao wa kundi la wasio wadilifu ambao wamepewa jina la mafisadi nao umekwishapanga safu yake na kinachoendelea sasa ni kuzidi kupenyeza fedha ili watu hao washinde nyadhifa mbalimbali za uongozi.
Taarifa zinafichua kuwa, sasa kuna kambi ya wazalendo na kambi ya mafisadi ndani ya chama hicho katika wakati huu wa mchuano wa kupata uongozi mpya.
Hali hiyo ya mpambano kuelekea kilele cha uchaguzi wa CCM imegusa viongozi kadhaa, kuanzia wale wanaotajwa kukosa uadilifu na hata baadhi ya viongozi wa sasa, kila mmoja akichambuliwa kwa kadiri ya mwenendo wake na akipimwa kwa kuzingatia vigezo kadhaa, ikiwamo kasi ya kisiasa nje ya chama hicho, kasi ambayo bila shaka, inahusisha CHADEMA.
Nafasi ya Katibu Mkuu
Katika nafasi hii, inaelezwa kuwa kundi la wazalendo bado linaendelea kumshawishi Mwenyekiti wa Kampeni za mgombea urais wa CCM, mwaka 1995, 2005 na 2010 na mlezi wa chama hicho kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Kinana, ateuliwe kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa CCM.
Hata hivyo, inadaiwa ya kuwa Kinana bado hana majibu ya moja kwa moja ya kukataa au kukubali majukumu hayo.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, kama Kinana atakubali uteuzi huo ataweza kuwaunganisha wanaCCM wenye kutaka chama hicho kurejea katika misingi yake. Lakini pia kama atakubali, anatajwa kuweza kuweka masharti kadhaa yanayoweza kutafsiriwa kuwa ni magumu kutekelezwa na viongozi wengine wa chama hicho.
Kwa muda mrefu, Kinana amekuwa akitajwa kupingana na viongozi wa chama hicho wanaozongwa na kashfa, akiwa ni kati ya wanaoshinikiza baadhi ya viongozi wenye tuhuma ama kujiondoa au kuondolewa ndani ya chama hicho.
Ushawishi kwa Kinana kuwa Katibu Mkuu wa CCM unatokana na kile kinachoelezwa na baadhi ya wanaCCM kwamba, Katibu Mkuu wa sasa, Wilson Mukama, licha ya kuteuliwa mahsusi kushika wadhifa huo ili kutekeleza kile kilichopata kupendekezwa na kamati aliyoiongoza kuhusu mabadiliko ndani ya CCM, hajafanya vizuri sana katika kusimamia mabadiliko hayo.
Katika mapendekezo ya Kamati ya Mukama, msemo maarufu wa kujivua gamba uliibuka lakini usimamizi wake umekuwa ukikosa msukumo uliostahili.
Baadhi ya wanaCCM wanasema, Mukama alipaswa kuonyesha msimamo katika utekelezaji wa kile alichokiamini na kilichopendekezwa na kamati yake na kama baadhi ya viongozi wenzake wa juu walikuwa wakimkwamisha, basi alipaswa kujiuzulu.
Licha ya Mukama kuonekana kutakiwa kustaafu na Kinana kushawishiwa kuchukua nafasi hiyo, kundi la wanaCCM walioko katika tuhuma za ufisadi linatajwa kuhakikisha hapati nafasi hiyo.
Inaaminika kuwa Kinana ni kikwazo kwa kundi hilo na hasa kutokana na msimamo wake wa kupinga matumizi ya fedha katika uchaguzi wa chama hicho, sambamba na tabia ya kulindana miongoni mwa viongozi serikalini.
Mikakati inatajwa kufanywa kumchafua Kinana, ikiwa ni pamoja na kuhusisha baadhi ya vyombo vya habari nchini. Mikakati hiyo imepangwa kutekelezwa kabla ya Novemba, mwaka huu.
Makamu Mwenyekiti CCM
Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti, wito sasa unatolewa kwa Pius Msekwa anayeshikilia nafasi hiyo kwa sasa astaafu.
Msekwa amekuwa katika nyadhifa kuanzia wakati wa TANU, ambako baada ya chama hicho kujibadili kuwa CCM akawa Katibu Mkuu Mtendaji wa chama hicho kilichoshiriki harakati za Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika.
Msekwa anatajwa kutomudu kasi ya sasa ya ushindani wa kisiasa nchini inayochochewa kwa namna fulani na CHADEMA. Taarifa zilizopo zinaeleza kuwa kundi la wazalendo ndani ya CCM linaendeleza ushawishi ili nafasi hiyo ichukuliwe na aliyepata kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Mangula.
Mangula anasifiwa katika kubuni na kusimamia mikakati ya kisiasa, akiwa na uwezo mkubwa wa kusimamia bila kutetereka kanuni za chama hicho, ambazo hakuna sehemu zinazopoeleza kuhusu viongozi watuhumiwa wa ufisadi kutetewa na chama.
Bado haijulikani utayari wa Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete, ambaye ni yeye ndiye anayepaswa kuamini katika utendaji wa Mangula ili hatimaye mwanasiasa huyo aliyemwachia ‘kijiti’ cha Katibu Mkuu CCM, Yusuf Makamba, apewe nafasi hiyo ya makamu mwenyekiti.
Itikadi na Uenezi
Katika nafasi hii ya Katibu wa Itikadi na Uenezi, ambayo kwa sasa inashikiliwa na Nape Nnauye, vyanzo vyetu vya habari vinaeleza kuwa kati ya wanaopendekezwa kuchukua nafasi hii kutoka katika makundi ya kisiasa ndani ya CCM ni pamoja na William Ngeleja au Martin Shigela.
Nape anatajwa kuendelea kutetewa na wazalendo ndani ya chama hicho lakini wanaompinga wanadai ni kijana mwenye msimamo usiowafurahisha baadhi ya watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi.
Kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi, msimamo ambao ni mtaji mbele ya vijana na Watanzania kwa ujumla, inaaminika kwamba Ngeleja ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Sengerema na aliyepata kuwa Waziri wa Nishati na Madini, kabla ya kuundwa upya kwa Baraza la Mawaziri miezi kadhaa iliyopita, na Shigela ambaye ni Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM, wachukue nafasi ya Nape.
Hata hivyo, tofauti na Nape ambaye bado hajawa na rekodi ya kuzorota kisiasa na hasa katika usimamizi na ufuatiliaji, ikiwa ni pamoja na kukabili wimbi la siasa nje ya chama chake, Shigela anatajwa kushindwa kuinua Umoja wa Vijana wa CCM.
Kwa mujibu wa maelezo ya wanaCCM kadhaa ambao hawakutaka kuandikwa majina yao gazetini, Shigela akiwa mtendaji mkuu wa UVCCM anatajwa kuwa ameufanya umoja huo kutokuwa tishio la kisiasa kwa vyama vya upinzani na hata yeye binafsi, si mwanasiasa mwenye umahiri unaotishia vyama vingine kisiasa.
Kwa Shigela kupewa nafasi hiyo ya Katibu wa Itikadi na Uenezi, inaelezwa kuwa ni sawa kuzorotesha idara ya itikadi na uenezi ya chama hicho.
Shigela kwa baadhi ya wanaCCM anatajwa kutokuwa mbunifu na inadaiwa UVCCM kwa sasa inaomba hata fedha kwa ajili ya kugharimia mikutano na semina zake licha ya kuwa na vitega uchumi kadhaa.
Kwa namna fulani, Ngeleja naye anatajwa kuwa ni sawa na kijana ambaye uteuzi wake utadhoofisha idara hiyo, ikiaminika kwamba, ameondolewa serikalini kutokana na jamii kumtazama kwa jicho la kutokuwa mchapa kazi.
Katibu wa Uchumi na Fedha
Nafasi hii kwa sasa inashikiliwa na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba.
Mwigulu anatajwa kutofanya kazi yake ya masuala ya uchumi vizuri lakini akionyesha umahiri katika uwanja wa siasa za moja kwa moja, akipata kuongoza kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge, Igunga, mkoani Tabora kwa mafanikio ingawa katika kampeni za ubunge Arumeru Mashariki, alianguka.
Bado idara yake ya uchumi inakabiliwa na changamoto nyingi, chama chake kikiwa hakijabuni vyanzo vipya vya mapato, huku matumizi ya ruzuku yakizidi kupanuka, hasa baada ya chama hicho kuanzisha mikoa mipya ya kisiasa. Hata hivyo, Mwigulu anatajwa kutokuwa na madhara kwa mtandao wa mafisadi ndani ya CCM.
Naibu Katibu Mkuu-Bara
Nafasi hii inashikiiwa na John Chiligati ambaye ni mbunge. Chiligati anatajwa kutokuwa mzigo katika safu ya uongozi wa chama hicho. Ni mwanasiasa mzoefu ambaye hata hivyo, wanaCCM wenzake wanamtafasiri kama anayeanza kuachwa nyuma na changamoto za kisiasa nchini, hususan na mazingira ya kisiasa nje ya CCM. Anatajwa kuwa mzito katika kuamua, kinyume na hali halisi katika siasa za wakati huu.
Katibu wa Mambo ya Nje
Nafasi hii inashikiliwa na Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba, ambaye kutokana na uteuzi wake wa kuwa Naibu Waziri na kwa kuzingatia taratibu mpya za CCM, hatapaswa kurejeshwa katika nafasi yake hii ya chama.
Katika uongozi wake ndani ya CCM, Januari anatajwa kutokuwa na misimamo yenye kueleweka, hakuwa akieleweka kuwa anaamini katika nini. Mazingira hayo ya kutokueleweka yanamhusisha na sifa zisizohitajika katika kutafuta viongozi wanaoweza kuipigania imani ya chama hicho kwa hali na mali.
Ukiondoa udhaifu huo kwa kiongozi kutojulikana unasimamia nini, Januari anatajwa kupanua shughuli za Idara yake ya Mambo ya Nje, jambo ambalo linatajwa kupaswa kuendelezwa na atakayeshika nafasi hiyo baadaye mwaka huu.
No comments:
Post a Comment