Monday, August 27, 2012

Polisi wazuia maandamano ya CHADEMA


WAKATI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kikitarajia kufanya mkutano mkubwa mjini Morogoro kuhitimisha operesheni yake ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) iliyodumu kwa wiki tatu, Jeshi la Polisi mkoani hapa limejiingiza tena kwenye msuguano na chama hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, amewakatalia CHADEMA kufanya maandamano wakati wakielekea kwenye uwanja wa mkutano wao leo katika viwanja vya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege na kuwashirikisha viongozi wa juu wa chama hicho.
Agosti 4, mwaka huu, Kamanda Shilogile alizua tafrani wakati CHADEMA wakianza mikutano yao mkiani hapa, baada ya kuizuia akidai hawana askari wa kutosha kwani maonesho ya wakulima Nanenane yalikuwa yakiendelea.
Hata hivyo, maelezo hayo yalipingwa vikali na viongozi wakuu wa CHADEMA na kushinikiza kufanya mikutano hiyo kwa nguvu kwani ilikuwa imeruhusiwa kihalali na jeshi hilo, jambo lililosababisha kufanyika majadiliano baina ya pande hizo na muafaka kupatikana.
Lakini katika hatua inayoonesha kama kutaka kuibua upya msuguano huo, jana Kamanda Shilogile, alieleza sababu za kuzuia maandamano hayo kuwa ni udogo wa barabara za mji wa Morogoro, na kwamba leo ni siku ya kazi, hivyo yanaweza kuleta usumbufu kwa wananchi.
Wakati Shilogile akitoa kauli hiyo, Mkuu wa Operesheni  Sangara, Benson Kigaila, alisema watafanya maandamano hayo kwa vile walishakubaliana na jeshi hilo kabla ya kuwageuka.
Badala yake Shilogile alisema wataruhusu watu wasiozidi 50 kupita kwa wakati mmoja pasipo kuwa na ishara ya kuonesha kama wanaelekea katika maandamano.
“Sisi tumewaambia viongozi wao watapanda magari, lakini wananchi watafute njia ya kufika huko na si kwa maandamano, hilo hatuwezi kuruhusu,” alisema Shilogile.
Alipoulizwa makubaliano yaliyofikiwa awali baina yao na CHADEMA juu ya kupanga njia ya kupita kwa maandamano hayo, Shilogile alisema hakukuwa na makubaliano ya namna hiyo.
Hata hivyo, Kigaila alisema wanachojua wao ni kwamba mikutano yao ipo kisheria, na kwamba wameshatoa taarifa kama inavyotakiwa hata kufikia hatua ya kukubaliana kwenda kupanga njia ya kupita.
Alisema sababu alizotoa Shilogile hazina mashiko kwa kuwa barabara za Morogoro ni sawa na za miji mingine, na kwamba ndani ya mkoa huo kulishafanyika maandamano mengine tofauti na ya CHADEMA.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment