MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), ameahidi kuziandikia mamlaka husika za serikali ili zitoke ofisini na kwenda kukagua ubovu wa baadhi ya barabara katika jimbo hilo.
Mnyika alitoa kauli hiyo baada ya kufanya ziara juzi katika kata za Kimara, Mabibo na Makuburi na kujionea ubovu wa barabara za Kimara-Mavurunza-Bonyokwa, Ubungo Maziwa-Kisiwani Darajani-Mabibo External na Makuburi-Kibangu-Makoka, ambazo amesema zinahitaji kufanyiwa matengenezo ya haraka.
“Barabara ya Kimara-Mavurunza-Bonyokwa ambayo tayari Wizara ya Ujenzi imekubali kuihudumia leo nitawasilisha barua kwa Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dare es Salaam kutaka hatua zake kwa hali mbovu ya barabara hiyo,” alisema.
Alisema kuwa mwaka 2011 barabara hiyo ilifanyiwa matengenezo ya kawaida, lakini kwa sasa imeharibika tena kutokana na mvua zilizonyesha, hali inayoathiri pia hatua za kupunguza msongamano kwenye barabara ya Morogoro hasa wakati huu wa ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo haraka (DART) kwa kuwa barabara hiyo hutumika kama njia mbadala.
Kuhusu barabara Ubungo Maziwa-Kisiwani Darajani-Mabibo External, alimkumbusha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kufuatilia kutoka Mfuko wa Barabara fedha za ujenzi wa daraja kwa dharura kwa kuwa kwa hali ya sasa na uzito wa magari yanayopita, linaweza kuvunjika na kusababisha maafa.
Kuhusu barabara ya Makuburi-Kibangu-Makoka, alieleza kuwa matengenezo yanasubiri malipo ya fidia ya nyumba yafanyike, kwani zimebaki sh milioni 64.
“Manispaa ya Kinondoni inapaswa kulitolea kauli kwa kuwa lilipaswa kukamilika katika mwaka wa fedha ulioisha. Mpaka Mei 3, mwaka huu, jumla ya sh milioni 122 zilikuwa zimeshalipwa kama fidia, hivyo Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Manispaa ya Kinondoni zinapaswa kuharakisha malipo ili kuepusha gharama za fidia kuongezeka,” alisema Mnyika.
Alibainisha malipo yangefanyika kwa wakati mwaka 2010 gharama za fidia zingekuwa sh milioni 80, lakini sasa zimeongezeka na kufikia zaidi ya milioni 180.
Pamoja na hayo, amesema wakati anasubiri serikali kutekeleza hayo, ameweka utaratibu kwa kushirikiana na madiwani kwa ajili ya kuunganisha wananchi wa maeneo husika na wadau wengine, ili kufanya matengenezo madogo kupunguza kero.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment