Tarehe 27 Julai 2012 kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani niliitaka Serikali itoe maelezo maelezo kuhusu taarifa zilizotolewa bungeni tarehe 13 Aprili 2012 kuwa wafanyakazi ikiwemo wa migodini kupitia vyama vyao walihusishwa kutoa maoni yaliyopelekea kufutwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits); suala ambalo Chama Cha Wafanyakazi wa Migodini (TAMICO) kililikanusha.
Hata hivyo, Waziri wa Nishati na Madini wakati wa majumuisho ya Hotuba yake tarehe 28 Julai 2012 hakutoa majibu yoyote bungeni kuhusu suala hilo hali ambayo imesababisha migongano kuendelea katika migodi mbalimbali kuhusu madai hayo hali ambayo kwa taarifa nilizozipata tarehe 1 na 2 Agosti 2012 inaweza kusababisha migomo migodini.
Naendelea na mawasiliano na wadau mbalimbali wa sekta ya madini na kesho tarehe 3 Agosti 2012 nitatoa kauli ya kina kuhusu hatua za ziada ambazo kwa nafasi ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini na mbunge nitachukua kuhusu hali hiyo.
Ikumbukwe kwamba tarehe 27 Julai 2012 nilieleza bungeni kuwa ufafanuzi uliotolewa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwa barua yenye Kumb. Na. AE/164/334/Vol II/2 umekataliwa katika migodi mbalimbali na kuhoji Wizara ya Nishati na Madini imechukua hatua gani kuepusha migogoro iliyoanza kujitokeza baina ya wafanyakazi wa migodini na serikali kufuatia kupitishwa kwa vifungu husika vya sheria vyenye kuagiza mafao kutolewa baada ya kufikisha umri wa hiyari wa kustaafu wa miaka 55 au umri wa lazima wa miaka 60.
Kwa upande mwingine kufuatia kushamiri kwa migogoro baina ya wafanyakazi na wawekezaji katika sekta ya madini, Kambi Rasmi ya Upinzani ilipendekeza Wizara ya Nishati na Madini iweke mfumo wa mashauriano na Wizara nyingine ili kuharakisha utatuzi wa migogoro husika. Aidha, nilieleza wimbi la malalamiko ya wafanyakazi walioachishwa katika migodi wa Bulyankulu, Mgodi wa Geita, Mgodi wa North Mara Kampuni ya Caspian katika mgodi wa Mwadui Shinyanga , masuala ambayo yanahitaji ushirikiano wa wizara na mamlaka mbalimbali katika kuyashughulikia.
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
03/08/2012
No comments:
Post a Comment