KWA kuamini kuwa walimu ndio kundi kubwa linaloongoza kwa ajira za watumishi wa serikalini na ndiyo kundi kubwa ambalo wananchi pia wanadhani ndio mawakala wakubwa wa chama tawala basi leo hii tusome safu hii.
Walimu kwa kiasi kikubwa wameifanya jamii kuwa na mtazamo tofauti kuwa ndio wanaoongoza kusimamia vituo vya kupigia kura kila uchaguzi mkuu unapofanyika,wanaaminiwa na serikali kutokana na taaluma yao kwa umakini wa kusimamia chaguzi na kuhesabu kura kwa usahihi.
Katika jambo lolote zito la kitaifa walimu ndio washiriki wakubwa pamoja wanafunzi wao. Ni wazi kuwa huwezi kuwasha Mwenge wa Uhuru bila ya kuwepo kwa vijana waliofundishwa na walimu kucheza halaiki na burudani nyingine.
Ndio wanaowafundishwa wanafunzi maana ya kuwasha Mwenge huku wakiimba kuwa uangaze ndani na nje ya mipaka yake, ulete amani pasipo na matumaini na kwa maana hiyo pale ambapo hakuna matumaini ya maisha bora ni nadra kwa amani kustawi.
Walimu ndio kimbilio la kada mbalimbali, naweza kusema kundi hili lina idadi kubwa ya watumishi ambayo ni zaidi ya 160,000 nchi nzima. Hawa ndio wasimamizi kwenye chanjo za kitaifa, sensa, ndio wanaojipanga barabarani na wanafunzi wao kwa ajili ya kuwapokea viongozi wa kitaifa ingawa kwa kificho hivi sasa bado wanafanya hivyo.
Walimu ndio wanaoongoza kwa kuishi kwenye nyumba mbovu na madarasa kuu kuu huko vijijini na hao hao ndio wanaoonekana kuongoza kwa usomi katika maeneo wanayoishi na ili kila jambo lifanikiwe vema ndio washauri wakuu na waasisi wa amani katika maeneo yao ya kazi.
Mambo hayo yote yanamfanya mwalimu kuwa na sura ya pekee katika mwonekano wa watumishi wa umma na ndio kundi ambalo pengine linahesabika kuwa ni kada ya watumishi wanyonge, wale waliokosa mahali pa kwenda wakaamua kukimbilia ualimu.
Licha ya kuwepo kwa mtazamo huo hasi ikumbukwe kuwa mwalimu ndiye msingi na mafanikio ya kila mtu aliyefikia hapo alipo na ndio msingi wa taaluma ya aina yoyote ile, ili uwe daktari lazima uanzie kwa mwalimu, ili uwe rubani lazima uanzie kwa mwalimu na kila aina ya utaalamu mwalimu anahusika sana.
Na ili chama chochote cha siasa kifanikiwe kushika au kulitetea dola lake lazima kijijengee uhusiano mkubwa na mzuri na walimu, hawa ndio washawishi wakubwa hasa maeneo ya vijijini ambako kada hiyo ya utumishi imezagaa kila kona ya nchi.
Mwalimu kwa upeo wake anasikilizwa sana na watu anaoishi nao mijini, vijijini na kuaminiwa kwao huifanya jamii iiamini serikali yao na chama kilichoshika dola. Kwa muktaba huu wa kuaminiwa kwa kundi hilo watu wenye mtazamo tofauti hubaki na imani kuwa walimu kwa kiasi kikubwa ni mawakala wa chama tawala.
Wengi walikuwa na mawazo hayo huko nyuma kuwa haiwezekani kuwaamini sana walimu wakati wa uchaguzi mkuu wakihofiwa kuwa wanafanya kazi ya kukilinda chama tawala ili kishinde uchaguzi kwa hila na njama za walimu na hiyo ndiyo kasoro kubwa na iliyoendelea kuwatia doa walimu.
Kadiri siku zinavyozidi kwenda uhusiano kati ya walimu na serikali unazidi kupungua na kupungua kwake kunatokana na mahitaji ya walimu kuzidi kuongezeka, wanahitaji mishahara minono, wanahitaji posho za kufundishia masomo ya sayansi na sanaa, wanahitaji walipwe posho za mazingira magumu, hayo yote ndiyo madai ya msingi ya walimu.
Madai hayo yanaanza kuitisha serikali ambayo siku zote ilikuwa ikiamini kuwa walimu ni kundi la watu watulivu, wasikivu,wavumilivu na kundi ambalo mara kadhaa limekuwa likitishia kugoma ili kudai haki zao lakini halijawahi kujiingiza kwenye mgomo uliosababisha wanafunzi wakose masomo yao darasani.
Ndiyo maana nasema kuwa kwa migomo hii na kwa matamko ya serikali kuhusu mgomo na kukataa kabisa kuwatimizia angalau ombi moja kati ya matatu ya msingi hali hiyo inazalisha ombwe kubwa kati ya walimu na serikali.
Ni wazi kuwa serikali inaposhindwa kusikiliza kilio cha walimu na kuingilia uhuru wa mahakama katika kutoa haki kunawazidishia walimu ukiwa na upweke wa kisaikolojia kwa maana inakuwa vigumu kuitumikia sawa sawa serikali waliyoifikisha mahali ilipo, mahali ambapo sasa inakiri wazi kuwa madai ya walimu hayalipiki.
Kwa kuwa madai ya walimu hayalipiki, ikubalike wazi kuwa urafiki mkubwa uliokuwepo kati ya walimu na chama tawala unazidi kupungua na urafiki huo ukipungua ni wazi kuwa wanakiweka rehani chama tawala na chama tawala kikiwekwa rehani basi bila shaka hata serikali iliyopo ikielekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2015 wana kitu cha kujiuliza.
Maombi ya walimu kwa msingi huo yamekuja mapema mno na kama wangekuwa wanasukumwa na nguvu za kisiasa kama inavyodhaniwa sasa, kwa kufikiria huko walimu hawatendewi haki hata kidogo ni dhahiri kwamba wanachokipigania walimu ni haki yao ya msingi hawajakurupuka.
Mgomo wa madaktari uliotangulia hali kadhalika nao hawakukurupuka, walikuwa wanadai haki zao za msingi na jinsi ya kuboreshewa mazingira mazuri ya kazi, ukiunganisha na mgomo huu wa walimu sura ya kisiasa ndani yake ni porojo tupu kwani muda huu si wa siasa isipokuwa ni muda wa malumbano ya wanasiasa wenyewe kwa wenyewe katika soko la kutafuta umaarufu wa kisiasa.
Naamini ingekuwa migomo hiyo yote ule wa madaktari na walimu kama ingefanyika mwanzoni mwa mwaka 2015 moja kwa moja ingehusishwa na utashi wa kisiasa kwa kuwa ingelenga kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuu, sasa haya madai ya mwaka 2012 wapi na wapi na mwaka 2015 hapo kuna kitu cha kujifunza.
Kwa hali ya sasa ambayo zama za teknolojia na utandawazi ulioenea kila kona wanafunzi wa shule za msingi hawawezi kukosa akili ya kuandamana kwenda kwenye ofisi za wakuu wa wilaya na mikoa eti kwa kufanya hivyo watakuwa wameshawishiwa na walimu wao waliogoma si kweli hata kidogo hawajashawishiwa, wanafunzi wa sasa wa sayansi na teknolojia si wale wa enzi za Mwalimu Nyerere.
Wanafunzi wa sasa wanajonea jinsi kaka zao wakiandamana wakiiomba serikali iwalipe fedha zao walizokopa za masomo ya elimu ya vyuo vya juu hapa nchini, wanaona jinsi wanavyoshika mabango wakitanda nje ya ofisi za bodi ya mikopo, wanafunzi hawa wa shule za msingi na sekondari haya yote wanayaona hapo hakuna siasa.
Jambo la msingi lazima serikali na chama tawala kilichoshika dola vijiweke mahali salama na kujipambanua wazi kuwa dhana ya ufisadi na ubadhirifu mkubwa wa mali za umma hakuwezi kuiweka salama serikali katika mikono ya walimu ambao muda wote imekuwa kada ya kutumiwa tu kadiri mwajiri wao anavyojisikia na kuzidi kuwa na malimbikizo makubwa ya madai ya walimu.
Mgawanyo wa rasilimali za nchi na ukosefu wa uwazi wa kutosha katika utoaji wa ajira, upendeleo na nguvu ya wanasiasa kuonekana muhimu zaidi, hali hiyo inadhoofisha nguvu kazi nyingine na hapo ndipo mwanya wa utengano kati ya walimu na serikali unapozidi kupanuka na ukipanuka ni wazi kuwa chama tawala kinawekwa rehani.
Wanacholilia walimu na kada nyingine za utumishi ni maisha bora, hawa walimu zaidi ya 160,000 nchi nzima wanapoamua kugoma wanaendelea zaidi kuitia doa serikali ambayo badala ya kutatua migogoro hiyo imekuwa ya kwanza kukimbilia mahakamani, kitendo cha kukimbilia mahakamani si suluhu, itafutwe njia ya kumaliza migomo, Tanzania si maskini.
Christopher Nyenyembe
No comments:
Post a Comment